Wenger amsifu Carrick
Muktasari:
- Wenger, ambaye kwa miaka mingi alikuwa na ushindani mkali na Manchester United, hakuwa na maneno mafupi ya kumsifu Carrick na benchi lake la ufundi.
London, England. Aliyekuwa kocha wa Arsenal, Arsène Wenger, juzi amempongeza vikali Michael Carrick kwa kuandaa mpango kamili wa mchezo uliowawezesha Manchester United kuwashinda wapinzani wao na vinara wa ubingwa, Arsenal, katika Uwanja wa Emirates.
Siku 12 tu, tangu ateuliwe kuchukua nafasi ya Ruben Amorim kama kocha mkuu hadi mwisho wa msimu, Carrick ameonyesha uwezo mkubwa wa kiufundi kwa kuwazidi ujanja Pep Guardiola na Mikel Arteta katika mechi mbili mfululizo na kuiongoza United kupata ushindi wa pili mfululizo.
Wenger, ambaye kwa miaka mingi alikuwa na ushindani mkali na Manchester United, hakuwa na maneno mafupi ya kumsifu Carrick na benchi lake la ufundi.
“Nadhani kuna jambo linaendelea ndani ya timu hii ya Man United, ukitazama namna walivyowashinda Man City na jinsi walivyowashinda Arsenal leo,” Wenger alisema kupitia beIN Sports.
“Walicheza kwa kushawishi sana na pia Arsenal waliporudi na kusawazisha hadi 2-2, mara nyingi timu ya nyumbani ndiyo hushinda mechi kama hiyo.
“Lakini United walipata tena nguvu ya kufunga bao la tatu na kushinda 3-2 ugenini kwenye mechi kubwa. Lazima nimpongeze Carrick. Ameunda kitu fulani.”
Arsenal bado wanaongoza msimamo wa ligi, wakiwa mbele kwa pointi nne baada ya kucheza mechi 23, lakini Wenger ameona dalili za udhaifu katika timu hiyo ambazo Carrick na United walizifichua.
“Unapofungwa mabao matatu nyumbani ni vigumu kushinda,” Wenger aliongeza.
“Mabao yaliyofungwa na pande zote yalionyesha kidogo namna timu hizo mbili zilivyocheza.
“Michezo ya Man United imejengwa vizuri, kuna mshikamano mzuri, lakini michezo ya Arsenal iliamuliwa zaidi na nguvu na mapambano, hasa kwenye kona iliyosababisha bao la pili.
“Bao la kwanza pia halikutokana na uchezaji safi. Walijituma sana Arsenal, lakini walikosa kidogo uvumilivu na mshikamano wa kiufundi, hasa kipindi cha kwanza.”
Wenger aliendelea kusema: “Ninaamini Carrick amepata fomula nzuri inayotoa uwiano mzuri kati ya uimara wa ulinzi na kiwango kizuri cha kiufundi.
“Ni mara ya kwanza nilihisi mabeki wa kati wa Arsenal walikuwa na wasiwasi zaidi na hawakuwa imara kama kawaida.”
Hofu za Wenger ziliungwa mkono na nahodha wake wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira, ambaye alikuwa mchambuzi wa Sky Sports.
“Wanahitaji kurudi kwenye misingi, wajieleze, wacheze kwa uhuru na wasonge mbele,” Vieira alisema kuhusu Arsenal.
“Kulikuwa na wachezaji wengi ambao hawakucheza vizuri leo.
“Ilikuwa ni mechi ya lazima kushinda. Walihitaji kutuma ujumbe kwa timu nyingine zote kwenye ligi.”