Weah aanika mbinu ya kupunguza ubaguzi wa rangi katika soka
Muktasari:
- George Weah amewahi kuwa Rais wa Jamhuri ya Liberia kwa kipindi cha miaka sita kuanzia 2018 hadi 2024 na amewahi kuzichezea Monaco, PSG na AC Milan.
Rais na nyota wa zamani wa Liberia, George Weah amesema kuwa matukio ya ubaguzi wa rangi kwenye soka yatapungua ikiwa wachezaji wataacha kuitana kwa majina na kuanza kuonyesha umoja.
Weah amesema kuwa kama wanasoka watakaribiana na kukumbatiana nyakati za mechi, itakuwa ni rahisi kukabiliana na matukio ya ubaguzi wa rangi kwa vile mashabiki wanawatazama wao kama kioo.
Mshindi huyo wa zamani wa Tuzo ya Ballon d'Or ameyasema hayo katika Mkutano wa Jopo la Sauti za Wachezaji la Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ulioketi Rabat, Morocco, mwishoni mwa wiki iliyomalizika.
"Nilichokuja kufanya hapa ni ili ulimwengu ujue kwamba hakuna haja ya ubaguzi wa rangi. Ni lazima tufurahie mchezo huo mzuri, tutembee pamoja uwanjani, tuimbe pamoja na tunaposhindwa, tunajaribu tena. Huu ndio mchezo unahusu kufurahia.
"Nadhani kilicho muhimu ni sisi kusahau kuitana majina na kukumbatiana na kufanya tuwe marafiki. Ndivyo ulimwengu unavyohusika. Vita si nzuri. Ubaguzi wa rangi ni ugonjwa. Hatuwezi kuendelea kuunga mkono ubaguzi wa rangi katika maeneo ya umma, hasa uwanjani ambapo kila mtu anatakiwa kufanya kazi pamoja, kufurahia pamoja, [hivyo], kufurahia mema ya mchezo," amesema Weah,
Rais wa FIFA, Gianni Infantino amesema kuwa Shirikisho hilo limejipanga kikamilifu kusaidiana asasi za wachezaji katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
"Katika FIFA, tumejidhatiti kujitolea kuimarisha zaidi ustawi wa wachezaji na mazingira ya kazi duniani kote kwa kutekeleza hatua madhubuti na za maana kwa nia ya kuboresha soka kwa siku zijazo. Hili linadhihirika kupitia uwekezaji mkubwa ambao FIFA itakuwa ikifanya kupitia Mfuko vya FIFA kwa Wachezaji na kupitia fursa nyingine za kushiriki kupitia vyombo mbalimbali ya FIFA, pamoja na mipango mingine muhimu iliyokubaliwa katika mkutano huu wa awali wa Jukwaa la Mashauriano la Wachezaji la FIFA.
"Tungependa kushukuru vyama vyote vya wachezaji ambavyo vimekaribia FIFA ili kushiriki katika majadiliano ya wazi. FIFA inataka kufanya kazi na wale wote wanaopenda kwa dhati maendeleo na mazungumzo ya heshima - milango yetu iko wazi kila wakati kwa maoni yote yanayoheshimu maadili haya. Hii ni harakati ya kweli kwa wachezaji na tunafurahi kwa hilo.
"Tunajivunia kuwasikiliza wachezaji, kusikia sauti na wasiwasi wao, na kufanya kazi pamoja kama timu moja chini ya mwavuli wa FIFA ili kufanya mchezo kuwa bora zaidi, mkubwa na wa kimataifa zaidi," amesema Infantino.