Watani wa jadi wategwa fainali FA

Muktasari:
- Kwa upande wa Simba, itakutana na Mbeya City iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa Championship. Huku Simba ikiwa nafasi ya pili kwenye ligi, na itacheza nyumbani kwenye mchezo huu muhimu.
Dar es Salaam. Droo ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) imechezeshwa huku timu mbili za Championship, Stand United na Mbeya City zikipangiwa kucheza dhidi ya timu kongwe za Ligi Kuu Bara, Yanga na Simba, hata hivyo wababe hao wakipenye vingingi viwili wanakutana fainali.
Katika droo hiyo iliyofanyika jana Alhamisi, Yanga itakuwa mwenyeji wa Stand United iliyopo nafasi ya tatu katika msimamo wa Championship baada ya kucheza mechi 25.
Kwa upande wa Simba, itakutana na Mbeya City iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa Championship.
Huku Simba ikiwa nafasi ya pili kwenye ligi, na itacheza nyumbani kwenye mchezo huu muhimu.
Timu nyingine zinazocheza hatua hiyo ni JKT Tanzania dhidi ya Pamba Jiji ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara, zilipokutana mechi ya kwanza zilitoka suluhu na bado hazijarudiana mzunguko wa pili. Pia Singida Black Stars itaikaribisha Kagera Sugar, mechi nyingine inayozikutanisha timu za ligi kuu.
Ili kupatikana timu zitakazocheza nusu fainali, mshindi kati ya Yanga na Stand United atakutana na mshindi kati ya JKT Tanzania na Pamba Jiji kwenye mchezo wa nusu fainali.
Nusu fainali nyingine itakuwa mshindi baina ya Simba na Mbeya City dhidi ya Singida Black Stars na Kagera Sugar, hii ikiwa ina maana kuwa kama Simba na Yanga zitapenya kwenye hatua ya robo fainali na nusu fainali basi zinaweza kukutana kwenye hatua ya fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa nchini.
Michezo ya robo fainali inatarajiwa kupigwa kati ya Aprili 10 hadi 14 mwaka huu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, amesema: "Zimepangwa tarehe hizo itategemeana na ratiba za timu nyingine ambazo zitakuwa na michezo mingine."
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa JKT Tanzania, Jemedari Said Kazumari alisema: "Utakuwa mchezo mgumu kwani timu zote zinacheza Ligi Kuu ambapo mechi ya kwanza ya ligi tulitoka suluhu, kabla ya kurudiana inatakiwa Pamba itufuate kwa ajili ya robo fainali ya FA, tunatarajia ushindani mkali na tunaamini tutafika mbali."
Mabingwa wa FA tangu mwaka 2015.
2015/16 Yanga
2016/17 Simba SC
2017/18 Mtibwa Sugar
2018/19 Azam FC
2019/20 Simba SC
2020/21 Simba
2021/22 Yanga
2022/23 Yanga
2023/24 Yanga