Yanga haishikiki mbio za ubingwa ikiichapa Tabora United

Muktasari:
- Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 61 ilizokusanya katika michezo 23.
Yanga imezidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya leo, Aprili 2, 2025 kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Ukurasa wa mabao ya Yanga umefunguliwa kuanzia dakika ya 21, baada ya beki wa kulia wa timu hiyo, Israel Mwenda kufunga kwa mkwaju wa moja kwa moja wa faulo nje ya eneo la 18, pigo ambalo lilipatikana baada ya mshambuliaji, Prince Dube kufanyiwa madhambi na Andy Bikoko wa Tabora United.
Wakati Tabora ikipambana kusawazisha bao hilo, Clement Mzize alipachika la pili katika dakika ya 57 na baadaye Prince Dube alifunga bao la tatu na la mwisho katika dakika ya 68.
Mabao hayo ya Dube na Mzize yamewafanya nyota hao kufikisha mabao 11 kila mmoja kwenye Ligi Kuu msimu huu, nyuma ya Jean Charles Ahoua wa Simba mwenye mabao 12.
Matokeo hayo yameifanya Yanga ifikishe pointi 61 na kuzidi kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi lakini pia imelipa kisasi cha kufungwa mabao 3-1 na Tabora United katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi iliyochezwa Novemba 7, 2025 katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Hicho kimekuwa ni kipigo cha kwanza kwa kocha wa Tabora United, Genesis mangombe ambaye alianza kuinoa timu hiyo kuanzia Machi 28.
Ushindi kwa Yanga umekifanya kikosi hicho kufikisha michezo 13, mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 3-1, dhidi ya Tabora United, Novemba 7, 2024, ikishinda 12, huku mmoja tu ukimalizika kwa sare.
Kikosi cha Tabora United: Jean-Noel Amonome, Kelvin Pemba/ Abdallah Seseme, Banele Junior/ Ibrahim Hamad Hilika, Shafih Maulid, Emmanuel Chilekwu, Nelson Munganga/ Shedrack Asiegbu, Emmanuel Mwanengo/ Yassin Mustafa, Andy Bikoko, Joseph Akandwanaho/ Ramadhani Chobwedo, Offen Chikola, Heritier Makambo.
Kikosi cha Yanga: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Hamad 'Bacca'/ Bakari Mwamnyeto, Duke Abuya, Maxi Mpia Nzengeli/ Jonathan Ikangalombo, Mudathir Yahya/ Salum Aboubakar 'Sure Boy', Prince Dube/ Farid Mussa, Pacome Zouzoua, Clement Mzize/ Shekhan Ibrahim Khamis.
Mechi ya kwanza kwa siku ya leo imechezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambayo wenyeji Pamba Jiji FC wamelazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo FC.
Namungo ilitangulia kupata bao kupitia kwa Jacob Massawe katika dakika ya 22 na Pamba Jiji ilisawazisha katika dakika ya 38 kupitia kwa mshambuliaji Abdullaye Camara.
Katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, wenyeji Fountain Gate wamekutana na kipigo kizito nyumbani wakifunga mabao 3-0 na Singida Black Stars ambayo imepata mabao yake kupitia kwa Jonathan Sowah, Frank Kwabena na Emmanuel Kwame.
Kwingineko kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, wenyeji KMC wameibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Tanzania Prisons.
Mabao ya KMC katika mechi hiyo yamefungwa na Shaban Chilunda aliyefumania nyavu mara mbili na lingine moja limefungwa na Ibrahim Elias na kwa upande wa Tanzania Prisons, mabao yao yamepachikwa na Haruna Chanongo.