Waarabu wamuweka Fernandes mtegoni

Muktasari:
- Mkataba wa Bruno Fernandes na Manchester United utafikia tamati Juni 30, 2027.
Al Hilal ya Saudi Arabia imechoka kumsubiria kiungo aa Manchester United, Bruno Fernandes na sasa imemtaka hadi mwishoni mwa mwezi huu aamue kama atajiunga nao au atabakia kwenye klabu yake.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30 amekuwa akiwindwa na Al Hilal kwa miaka ya hivi karibuni na timu hiyo ya Saudi Arabia iko tayari kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa Manchester United na mchezaji mwenyewe ili kumshawishi ajiunge nao.
Al Hilal iko tayari kuilipa Man United kiasi cha Pauni 100 milioni (Sh364 bilioni) na kumlipa nyota huyo wa Ureno mshahara wa kiasi cha Pauni 700,000 (Sh2.5 bilioni) kwa wiki.
Mwezi ujao, Al Hilal itashiriki fainali za Kombe la Dunia la klabu na inataka kuwa na Fernandes ikiamini atakuwa msaada mkubwa kwao kufanya vyema katika mashindano hayo.
Al Hilal inaamini kuwa haitokuwa shida kwa Manchester United kumuachia Fernandes kwa vile inahitajika kuweka sawa vitabu vyake vya mapato na matumizi baada ya kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Man United ambayo imefungwa bao 1-0 na Tottenham Hotspur katika fainali ya Europa League juzi Jumatano, imekosa kiasi cha Pauni 100 milioni (Sh364 bilioni) kwa kutofuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa vile bingwa wa Europa League anafuzu moja kwa moja kushiriki mashindano hayo.
Pia Manchester United inatakiwa kulipa kiasi cha Pauni 10 milionj kwa kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas kwa kutofuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kama mkataba wa udhamini baina yao unavyoainisha.
Miamba hiyo ya England pia itajikuta ikipata fedha ndogo za zawadi kutoka Ligi Kuu England kutokana na kumaliza katika nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Sababu hizo zinaiaminisha Al Hilal kuwa itaweza kumnasa Fernandes kwani inaonekana Manchester United itakuwa tayari kumfungulia milango nyota huyo wa Ureno pamoja na wengine baadhi ili ijiweke sawa kiuchumi.
Na kauli ya Bruno Fernandes baada ya mechi ya fainali ya Europa League inaonekana kuwapa hamu zaidi Al Hilal kumsajili ambapo kiungo na nahodha huyo wa Man United amesema kama klabu itakuwa tayari kumuuza, yeye yuko tayari kwa hilo.
“Kama klabu inahisi ni wakati wa kuachana kwa sababu wanataka kuingiza fedha, ndio kama ilivyo,” amesema Fernandes