Vital’O, Yanga ugumu uko hapa

Muktasari:
- Leo, Yanga SC itakabiliana na Vital’O ya Burundi katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikicheza Uwanja wa Azam Complex saa 10:00 jioni.
Dar es Salaam. Matumaini makubwa ya Watanzania leo yapo kwa Yanga ambayo kuanzia saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Azam Complex itakabiliana na Vital’O ya Burundi katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Kwanza ni rekodi nzuri ya ubabe ambayo imekuwa nayo dhidi ya Vital’O ambayo imekuwa ikipata matokeo mazuri pindi timu hizo zikutanapo katika mashindano tofauti.
Vital’O imekuwa na unyonge kwa Yanga na kuthibitisha hilo, mechi ya mwisho ambayo zilikutanisha timu hizo mwaka 2008 ambayo ilikuwa ni ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Vital’O ilipoteza kwa mabao 2-0.
Lakini ubora wa kikosi cha Yanga ndio unafanya wengi wawe na matumaini makubwa kwa Yanga kuwa itamaliza kazi katika mechi ya leo ambayo itahesabika iko ugenini kwa kupata ushindi wa idadi kubwa ya mabao ambao utaipa kazi nyepesi katika mechi ya marudiano itakayochezwa mwishoni mwa wiki ijayo.
Uwepo wa kundi kubwa la wachezaji wenye uwezo binafsi ambao wameunganishwa vyema na kocha Miguel Gamondi na kutengeneza timu tishio, unaifanya Yanga kuwa na uhakika wa matokeo mazuri katika idadi kubwa ya michezo lakini pia kuipa nguvu ya kuamini kwamba inaweza kutamba katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Idara za kiungo na ushambuliaji ndio zinampa uhakika wa hali ya juu Gamondi kutokana na uwezo wa kuamua mchezo kwa kufunga mabao ambao wachezaji wake tofauti wameuonyesha hivi karibuni kuanzia katika mechi za kujipima nguvu kabla ya msimu kuanza na zile za mashindano.
Hilo linaweza kuthibitishwa na mechi tano zilizopita ambazo zote Yanga imeibuka na ushindi ambapo mabao yake 12 yamefungwa na nyota watano tofauti jambo ambalo linaweza kuiumiza kichwa Vital’O katika kupanga nani wa kumdhibiti ili iishangaze Yanga.
Mabao hayo 12 ya Yanga katika mechi 12 zilizopita, yamefungwa na Stephane Aziz Ki aliyepachika manne, Prince Dube aliyefunga matatu, Clement Mzize aliye na mawili huku Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli wakifumania nyavu mara mojamoja na moja likiwa la kujifunga.
Kocha wa Vital’O, Sahabo Paris alisema kuwa wameitazama vizuri Yanga na wamejipanga kukabiliana nayo.
“Tulishawasoma katika mechi waliyocheza dhidi ya Azam na Simba na tunajua mbinu gani ambazo tutatumia dhidi yao,” alisema Paris.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa wanaupa uzito mkubwa mchezo huo dhidi ya Vital’O.
“Kwenye haya mashindano huwa hakuna timu nyepesi na malengo ya klabu ni kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo tunapaswa kufanya vizuri katika mechi hii ya kwanza. Wachezaji wangu wako vizuri na tayari kwa mchezo ambao naamini hauwezi kuwa rahisi,” alisema Gamondi.
Baada ya mechi hiyo ya Yanga, kuanzia saa 12:00 jioni, Coastal Union itakuwa ugenini kukabiliana na Onze Bravos ya Angola wakati kesho kutakuwa na mechi ya timu tatu za Tanzania ambazo ni Azam FC itakayoikaribisha APR ya Rwanda katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Azam Complex wakati huo JKU ikikabiliana na Pyramids huko Misri kwenye Ligi ya Mabingwa huku Uhamiaji ikiwa na kibarua dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya katika Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa huko Benghazi, Libya.
Hesabu za kikubwa
Malengo ambayo timu tatu za Tanzania zimejiwekea katika mashindano hayo yanadhihirisha ukubwa na kupanda kwa thamani kwa soka la Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.
Yanga inaingia ikiwa na lengo la kutinga hatua ya nusu fainali kama ambavyo watani wao Simba ambao hawajaanzia raundi ya kwanza, wameliweka katika Kombe la Shirikisho Afrika ambalo inashiriki.
Wakati Simba na Yanga zikiwa na malengo ya nusu fainali, Azam FC yenyewe imeweka hatua ya makundi kama lengo lao kuu katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni wazi kwamba kutinga hatua ya makundi litakuwa ni jambo la kipekee na kihistoria kwa Coastal Union, JKU na Uhamiaji lakini kama zitashindwa kufika, hakuna ambaye ataweza kuzibebesha lawama.
Fedha miguuni mwao
Ni mashindano ambayo yanaweza kuziingizia kiasi kikubwa cha fedha timu sita za Tanzania ikiwa zitafanikiwa kufuzu hatua ya makundi au kuenda za juu zaidi ya hiyo.
Kiasi kikubwa cha fedha hizo kinatokana na zawadi ambayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) linatoa kwa timu zinazoingia hatua ya makundi, kisha robo fainali, nusu fainali na fainali.
Kitendo cha kutinga tu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kinaihakikishia timu kiasi cha Dola 700,000 (Sh1.9 bilioni) na ile inayoingia hatua ya robo fainali inavuna Dola 900,000 (Sh2.4 bilioni).
Bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika anapata kiasi cha Dola 4 milioni (Sh10.8 bilioni) na mshindi wa pili anapata kitita cha Dola 2 milioni (Sh5.4 bilioni).
Bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika anapata kiasi cha Dola 2 milioni (Sh2.7 bilioni) wakati waliotwaa ubingwa walipata Dola 1 milioni (Sh2.7 bilioni).
Timu inayoishia hatua ya nusu fainali inapata Dola 750,000, Dola 550,000 kwa inayoishia robo fainali na timu inayotolewa katika hatua ya makundi ya mashindano hayo inapata kifuta jasho cha Dola 400,000 (Sh1 bilioni).