Van Nistelrooy, wasaidizi wa Ten Hag waondolewa United

Muktasari:
- Amorim aliyewasili leo Jiji Manchester amefanya mazungumzo na Ruud na kumweleza ukweli kwamba anataka kufanya kazi na benchi lake la ufundi ambalo amehama nalo kutoka Sporting Lisbon.
London, England. Kocha msaidizi wa Manchester United Ruud van Nistelrooy ameondoka kwenye kikosi hicho muda mchache baada ya kufanya kikao na kocha Ruben Amorim na kumwambia hayupo katika mipango ya benchi lake la ufundi.
Van Nistelrooy ambaye ameiongoza Man United katika mechi nne kama kocha wa muda baada ya kuondoka kwa Erik ten Hag awali aliripotiwa kuwa huenda angeendelea kuwepo kutokana na kazi nzuri aliyoifanya katika mechi hizo, hata hivyo mambo yamekuwa tofauti.
Amorim aliyewasili leo Jiji Manchester amefanya mazungumzo na Ruud na kumweleza ukweli kwamba anataka kufanya kazi na benchi lake la ufundi ambalo amehama nalo kutoka Sporting Lisbon.
Ruud ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa Man United kati ya mwaka 2001 hadi 2006, kabla ya kuajiriwa kama kocha msaidizi Julai mwaka huu chini ya Erik ten Hag mara kadhaa amewahi kusema kuwa angetamani kuendelea kuitumikia timu hiyo hata baada ya Amorim kuwasili.
Katika mechi nne za michuano yote ambazo Ruud ameiongoza Man United ameiwezesha kupata ushindi mara tatu na kutoa sare moja yakiwa ni mafanikio makubwa zaidi kwa Man United msimu huu.
Mbali na huyo, pia kocha huyo amewaeleza Rene Hake ambaye alikuwa msaidizi wa pili wa Ten Hag, kocha wa makipa Jelle ten Rouwelaar, mchambuzi wa viwango Pieter Morel kuwa hawezi kufanya nao kazi, lakini anawashukuru kwa mambo mengi waliyofanya.
Baada ya kocha huyo Mreno kumaliza mazungumzo yake na makocha hao, uongozi wa Man United umetoa taarifa ya maneno 100 ya kumuaga Ruud Van.
"Manchester United inapenda kuwataarifu kuwa Ruud van Nistelrooy ameondoka klabuni. Ruud ataendelea kuheshimika kama gwiji wa klabu hii kutokana na mchago wake alioutoa kwa kipindi alichokuwa hapa, anakaribishwa kwenye timu hii muda wowote," ilisema taarifa hiyo ya United.
Amorim mwenye miaka 39, anatarajiwa kuanza kazi kwenye timu hiyo ambayo haina matokeo mazuri msimu huu akiwa anapewa nafasi kubwa ya kufanya mambo mazuri kwenye timu hiyo.
Taarifa zinasema kuwa malengo ya United msimu huu ni kutwaa ubingwa wa Europa na kumaliza ndani ya nne bora kwenye Ligi Kuu England.
Amorim ametua United akiwa na wasaidizi wake watano ambao ni, Carlos Fernandes, Adelio Candido, Emanuel Ferro, kocha wa makipa Jorge Vital na daktari wa michezo Paulo Barreira.