Ulaya mechi kibao zinapigwa

Muktasari:
- Real Madrid imeshinda 12, sare nane na vichapo 18 katika mechi 38 za ugenini ilizocheza na klabu za Italia
ROME, ITALIA. Usiku wa Ligi ya Mabingwa Ulaya unarudi tena, lakini macho ya wengi yakuwa huko Stadio di Bergamo usiku wa leo Jumanne kwenda kuwashuhudia mabingwa watetezi Real Madrid kama watakuwa na maajabu watakapovaa na vinara wa Serie A, Atalanta BC.
Kwa Real Madrid hakuna namna nyingine katika mchezo huo zaidi ya ushindi kama kweli inahitaji kuendelea kubaki kwenye mchakamchaka huo ambao umekuwa kwenye mtindo mpya kabisa msimu huu ili kutetea ubingwa wao.
Kwenye michuano hiyo ya Ulaya msimu huu, Real Madrid hali yao ni mbaya, ikiwa imevuna pointi sita tu kwenye mechi tano za kwanza, ikishika nafasi ya 24 kwenye msimamo, ambao ni nafasi ya mwisho kabisa ya timu inayoweza kushindania kwenye mchujo wa kuingia raundi inayofuata.
Wapinzani wao wa usiku wa leo, Atalanta wenyewe wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo huo, wakivuna pointi 11 kwenye mechi zao tano za kwanza.
Atalanta hakuna kificho kwamba ni moja ya timu zilizopo kwenye kiwango bora kabisa Ulaya kwa sasa, ambapo chama hilo bila shaka litaingia kwenye uwanja wake wa nyumbani likisaka ubshindi wa tisa mfululizo kwenye michuano yote msimu huu, baada ya kutokea kuwachapoa AC Milan 2-1 kwenye mchezo wa Serie A, Ijumaa iliyopita na hivyo kushika usukani wa ligi hiyo ya Italia kwa kukusanya pointi 34 katika mechi 15.
Kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kikosi hicho cha Gian Piero Gasperini kipo vizuri, kikivuna pointi 11 katika mechi tano, ambapo imeshinda tatu na kupoteza mbili, hivyo kushika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo. Atalanta, ambao ni mabingwa wa Europa League, wakimalizana na Real Madrid usiku wa leo, watakuwa na kibarua kingine cha kuwakabili miamba wengine wa La Liga, Barcelona, Januari 29. Na kipute chao cha kuwakabili Real Madrid kitakuwa cha kutaka kulipa kisasi baada ya kuchapwa 2-0 kwenye UEFA Super Cup, Agosti mwaka huu.
Real Madrid inaingia kwenye mchezo huo ikitokea kushinda 3-0 dhidi ya Girona kwenye La Liga, matokeo ambayo yameendelea kuwaacha kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, pointi mbili nyuma ya vinara Barcelona, huku vijana hao wa Carlo Ancelotti wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, Los Blancos haina maajabu, ikishinda mechi mbili tu kati ya tano na kuchapwa mara tatu, ikiwamo mechi zao mbili zilizopita ilipocheza na AC Milan na Liverpool. Itakapomalizana na Atalanta itabakiza mechi mbili dhidi ya Red Bull Salzburg na Brest.
Real Madrid imeshinda 12, sare nane na vichapo 18 katika mechi 38 za ugenini ilizocheza na klabu za Italia. Safari hii itakuwaje?
Real Madrid imefuzu kwenye hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika misimu 28 iliyopita, hivyo ikishindwa kufanya hivyo msimu huu itakuwa mara yao ya kwanza katika muda huo.
Mechi nyingine za Ligi ya Mabingwa Ulaya zitakazopigwa leo Jumanne, Dinamo Zagreb itakuwa nyumbani kucheza na Celtic, wakati Liverpool itasafiri hadi Hispania kwenda kuwakabili Girona, huku vijana wa Xabi Alonso, Bayer Leverkusen watakuwa wenyeji wa Inter Milan kwenye moja ya vipute vya kibabe katika kwenye michuano hiyo.
Brest watakuwa na shughuli pevu ya kucheza na PSV, wakati Brugge itakuwa nyumbani kucheza na Sporting Lisbon, huku RB Leipzig ikiwa na kasheshe mbele ya vijana wa Unai Emery, Aston Villa na Salzburg watamaliza ubishi na PSG wakati Shakhtar Donetsk wapo nyumbani kumuuliza maswali Vincent Kompany na jeshi lake la Bayern Munich.
Mchakamchaka utaendelea kesho Jumatano, ambapo Atletico Madrid ya Diego Simeone itakuwa na kazi nzito mbele ya Slovan Bratislava, Lille ikikipiga na Sturm Graz, huku AC Milan ikiwa na shughuli mbele ya FK Crvena Zvezda, Benfica itakipiga na Bologna, huku Feyenoord ikicheza na Sparta Prague, wakati vijana wa Mikel Arteta, Arsenal watakuwa nyumbani Emirates kucheza na AS Monaco, buku kasheshe zito litakuwa huko Ujerumani kwenye Uwanja wa Signal Iduna Park, ambapo Burussia Dortmund watakuwa na kibarua kizito mbele ya Barcelona.
Manchester City ya Pep Guardiola itakuwa na mtihani mzito wa ugenini kwenye kukipiga na Juventus huko Italia, wakati Wajerumani, VfB Stuttgart watakuwa nyumbani kumalizana na Young Boys. Kazi ipo.
Vikosi vinavyotarajiwa kipute cha Atalanta na Real Madrid;
Atalanta BC: Carnesecchi; Djimsiti, Hien, Kolasinac; Bellanova, De Roon, Ederson, Ruggeri; De Ketelaere, Retegui, Lookman
Real Madrid: Courtois; Vazquez, Tchouameni, Rudiger, F Garcia; Valverde, Bellingham, Modric; Rodrygo, Mbappe, Vinicius