Twiga Stars yaendeleza dozi CECAFA, yaipiga Burundi 6

Muktasari:
- Twiga Stars ndio timu pekee ya Ukanda wa CECAFA ambayo itashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024 zitakazofanyika Morocco kuanzia Julai 5 hadi Julai 26 mwaka huu.
Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ imeendelea kuwa tishio katika mashindano ya timu za taifa za Wanawake ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Burundi katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ushindi huo mnono wa Twiga Stars leo, umekuja ikiwa ni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya ufunguzi.
Katika mchezo wa leo, Twiga Stars ilionyesha mapema dalili ya kupata ushindi kutokana na kiwango bora ilichoonyesha kuanzia filimbi ya kuanza mchezo ilipopulizwa ikimiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi za mabao.
Mabao sita yaliyoifanya Twiga Stars itambe katika mechi ya leo yalifungwa na Opah Clement aliyepachika mawili na mengine yamepachikwa na Clara Luvanga, Stumai Abdallah, Diana Lucas na Jamila Rajabu.
Matokeo hayo yameifanya Twiga Stars iongoze msimamo wa mashindano hayo ikifikisha pointi sita huku ikiwa na mabao 10 na haijaruhusu nyavu zake kutikiswa.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime amesema kuwa amefurahishwa na matokeo na kiwango ambacho wamekionyesha.
“Niwapongeze wachezaji wangu kwa kazi ambayo wameifanya. Ilikuwa ni mechi nzuri niwapongeze wachezaji wangu. Tulikuwa na nafasi nzuri kwenye mchezo kwa vile tumeshinda lakini kwa upande mwingine hatukuwa na nafasi nzuri na tutaenda kufanyia kazi.
“Kila siku tunapocheza mechi kama hii, kazi yetu ni kuorodhesha mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo huu na tunaenda kuyafanyia kazi,” amesema Shime.
Twiga Stars sasa inahitajika kupata ushindi wa aina yoyote katika mechi mbili zilizosalia dhidi ya Uganda na Kenya ili itwae ubingwa wa mashindano hayo.