Twiga kujiuliza kwa Burundi Cecafa

Muktasari:
- Nyota wa Uganda, Sylivia Kabene anaongoza kwenye chati ya ufungaji akiwa mabao matatu, akifuatiwa na Opah Clement (Tanzania) na Martha Emedot wa Kenya ambao kila mmoja amefunga mabao mawili.
Dar es Salaam. Timu ya taifa ya Wanawake Twiga Stars leo inatarajia kushuka dimbani kuvaana na Burundi katika michuano ya CECAFA Senior Women Championship 2025 inayoendelea kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Twiga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Sudan Kusini uliopata kwenye mechi ya kwanza, wakati Burundi ikiwa ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Kenya.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya timu yake kocha Mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shime alisema anaamini mchezo huo utakuwa mgumu na anawataka wachezaji wake kucheza kwa nidhamu, kasi na umoja kama walivyofanya kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Burundi.
"Burundi ni timu nzuri na tunafahamiana kwa sababu tumekuwa tukicheza nao, mechi ya kwanza waliwafunga Uganda si jambo dogo, hivyo hatuwezi kuwabeza hata kidogo. Tutahakikisha tunaingia kwa tahadhari kubwa na kutafuta matokeo mapema," alisema Shime.
Kwa upande wa kocha wa Burundi, Niyungeko Alain, alisema wanafahamu ubora wa Tanzania lakini mechi hiyo wataitumia kurekebisha matokeo waliyopata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Kenya ambao walipoteza.
"Naweza kusema tuna kazi ya ziada ya kupata ushindi leo licha ya ugumu wa mchezo wenyewe, Tanzania ina wachezaji wazuri ambao wanaweza kukufunga muda wowote nimewaambia wachezaji wangu wacheze kwa tahadhari na kutumia makosa watakayofanya Stars."
Juzi Kenya ukiwa mchezo wao wa kwanza wa mashindano waliondoka na pointi tatu mbele ya Burundi huku mchezo wa jioni Uganda ikiitandika Sudan Kusini mabao 5-0.
Nyota wa Uganda, Sylivia Kabene anaongoza kwenye chati ya ufungaji akiwa mabao matatu, akifuatiwa na Opah Clement (Tanzania) na Martha Emedot wa Kenya ambao kila mmoja amefunga mabao mawili.