Twiga Stars yapaa viwango FIFA

Muktasari:
- Twiga Stars itashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake (Wafcon) zitakazochezwa Morocco, Julai 5-26 mwaka huu ni imefuzu hatua ya mwisho ya mashindano ya kuwania kufuzu fainali hizo mwaka 2026.
Timu ya Taifa ya soka ya wanawake Tanzania ‘Twiga Stars’ imepanda kwa nafasi saba katika viwango vya soka duniani kwa wanawake vya Shirikisho la mpira wa miguu duniani (Fifa) mwezi Machi 2025.
Kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake (Wafcon) 2024 na pia kutinga raundi ya mwisho ya kuwania kufuzu fainali hizo kwa mwaka 2026 kunaonekana kuibeba Twiga Stars ambayo imepanda kutoka nafasi ya 145 iliyokuwepo katika chati iliyopita ya Desemba 13, 2024 hadi nafasi ya 138 mwezi huu.
Kupanda huko kwa Twiga Stars kumetokana na ongezeko la pointi 41 ambalo imelipata ambapo ilipokuwa nafasi ya 145 ilikuwa na pointi 1046 na sasa ina pointi 1087.
Neema hiyo ya kupanda kwa nafasi saba haijaikuta Twiga Stars pekee kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati bali pia timu ya taifa ya wanawake ya Kenya ‘Harambee Starlets’ ambayo imeruka kutoka nafasi ya 149 hadi nafasi ya 142.
Ethiopia licha ya kuporomoka kwa nafasi nne kutoka ya 124 hadi 128, inaendelea kuongoza kwa upande wa Afrika Mashariki na Kati ikifuatiwa na Tanzania huku Kenya ikiwa nafasi ya tatu mtawalia.
Nafasi ya nne ipo Uganda ambayo kwa mujibu wa chati mpya ya Fifa, imeendelea kuwepo katika nafasi ya 148 iliyokuwepo awali na hiyo inaonekana kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na kutolewa kwa Uganda katika mashindano ya kuwania kufuzu fainali za Wafcon 2026.
Kwa mara ya kwanza katika historia, timu ya taifa ya wanawake ya Djibouti imeingia katika chati ya viwango vya ubora kwa soka la wanawake ya Fifa ambapo ipo katika nafasi ya 195 ikiziacha kwenye mataa Eritrea, Mauritania, Chad, Libya na Sudan ambazo hazipo.
Kwa mujibu wa chati hiyo, timu inayoongoza kwa ubora Afrika ni Nigeria ikifuatiwa na Afrika Kusini na nafasi ya tatu ipo Morocco wakati nafasi ya nne kuna timu ya Zambia na Ghana inashika nafasi ya tano.
Hakujawa na mabadiliko katika kilele cha chati hiyo ya viwango vya ubora kidunia kama ilivyo kwa nafasi ya pili, tatu na ya nne mtawalia.
Marekani inaendelea kuongoza ikifuatiwa na Hispania, Ujerumani na England ingawa nafasi ya tano inashikiliwa na Japan iliyopanda kwa nafasi tatu.
Viwango vipya vya soka la wanawake vya Fifa vitatolewa tena Juni 12 mwaka huu.