Twiga Stars inapenya hivi WAFCON
Muktasari:
- Sare ya 1-1 iliyopata juzi dhidi ya mabingwa watetezi Afrika Kusini imeipa matumaini timu hiyo kufuzu hatua hiyo baada ya mwaka 2010 kumaliza mkiani ikiwa bila ya pointi.
Timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania 'Twiga Stars' leo inahitaji ushindi wa pointi tatu dhidi ya Ghana ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu robo fainali ya Fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) yanayoendelea nchini Morocco.
Mechi hiyo ya mwisho kwenye kundi C itapigwa Uwanja wa Stade Municipal de Berkane na Tanzania inahitaji ushindi pekee ili kufuzu na kuandika historia kwenye michuano hiyo.
Sare ya 1-1 iliyopata juzi dhidi ya mabingwa watetezi Afrika Kusini imeipa matumaini timu hiyo kufuzu hatua hiyo baada ya mwaka 2010 kumaliza mkiani ikiwa bila ya pointi.
Msimamo wa kundi hadi sasa uko wazi Afrika Kusini iko kileleni na pointi nne sawa na Mali zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa sawa na Tanzania na Ghana zenye pointi moja kila timu.
Stars ikishinda mchezo dhidi ya Ghana, itafikisha pointi nne huku ikisubiri matokeo ya mchezo kati ya Afrika Kusini na Mali, ambazo zote zina pointi nne baada ya mechi mbili.
Hivyo, Stars inaweza kupita kama "Best Loser". Kwenye muundo wa kawaida wa mashindano ya timu 12, kuna makundi matatu (A, B, C), kila kundi likiwa na timu nne.
Timu mbili za juu kutoka kila kundi zinafuzu moja kwa moja kwenda robo fainali, na timu mbili bora zilizomaliza nafasi ya tatu pia zinaingia hatua hiyo. Hivyo, Stars ikishinda kwa kufikisha pointi nyingi au kwa tofauti nzuri ya mabao, itakuwa na nafasi hiyo, kwani jumla ya timu nane zinafuzu hatua inayofuata.
Pia, Stars itategemea matokeo ya mchezo kati ya Afrika Kusini na Mali. Kama zitatoka sare, kila timu itafikisha pointi tano na Tanzania itafuzu kama timu bora ya tatu.
Kama mabingwa watetezi Banyana Banyana wataibuka na ushindi, watafikisha pointi saba huku Mali ikibaki na pointi nne sawa na Tanzania. Hivyo, Stars itahitaji ushindi wa mabao mengi dhidi ya Ghana ili kufuzu moja kwa moja kwa tofauti ya mabao.
Kama Mali itashinda, itafikisha pointi saba, na Afrika Kusini (ambayo imeruhusu bao moja tu) itakuwa nafasi ya pili. Katika hali hii, Tanzania inaweza kufuzu kama itashinda kwa mabao mengi dhidi ya Ghana.
Katika mechi mbili zilizopita, Stars imecheza vizuri dhidi ya Mali licha ya kuruhusu bao moja, na pia dhidi ya Afrika Kusini ambapo licha ya kuwa pungufu uwanjani, waliweza kuhimili presha ya mchezo.
Kuelekea mechi ya mwisho ambayo ndiyo muhimu zaidi, Stars inapaswa kushambulia mapema. Ghana imeshindwa kushinda mechi zote na imeruhusu mabao matatu, hivyo inaonekana kuwa na udhaifu kwenye safu ya ulinzi.
Kocha wa Stars, Bakari Shime alisema mchezo wa Ghana ni kama fainali kwao hivyo ili kufuzu wanapaswa kushinda mchezo huo.
"Ni mchezo wa fainali kwetu ambao lazima tushinde dhidi ya Ghana na tupate alama nne maandalizi yamekwenda sawa na tunaamini tutafanya vizuri kwenye kile tulichoelekezana mazoezini."