Timu za Tanzania zinafeli hapa kwenye usajili

Muktasari:

  • Tetesi zimekuwa nyingi kuzihusisha timu hizo namna zinavyokuwa na uhitaji mkubwa wa wachezaji wanaokwenda kuzipambania timu zao ambazo msimu ujao zitaiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya kimataifa

Dar es Salaam. Wakongwe ndani ya Ligi Kuu Bara, Simba na Yanga wanateswa na ugonjwa mmoja ambao kila kinapofika kipindi cha usajili, kuna eneo linaguswa mara kwa mara. Ukiachana na wakongwe hao, Azam pia ni miongoni mwa timu zinazopitia changamoto hiyo.

Hivi sasa ni kipindi cha usajili wa dirisha kubwa lililofunguliwa Juni 15 mwaka huu na kutarajiwa kufungwa Agosti 15, 2024, litakuwa wazi kwa takribani miezi miwili ambapo timu za Ligi Kuu Bara, Ligi ya Championship, First League na Ligi Kuu Wanawake zinahusika kuimairisha vikosi vyao.

Tetesi zimekuwa nyingi kuzihusisha timu hizo namna zinavyokuwa na uhitaji mkubwa wa wachezaji wanaokwenda kuzipambania timu zao ambazo msimu ujao zitaiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya kimataifa. Yanga na Azam zitacheza Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Simba ikiwa Kombe la Shirikisho sambamba na Coastal Union.

Jambo kubwa ambalo linazitesa timu hizi na nyinginezo zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ni eneo la ushambuliaji. Kwa misimu mingi kila kinapofika kipindi cha usajili, timu hizo basi zitasajili mtu wa eneo hilo, kama siyo mmoja basi zaidi yake, hii inamaamisha kwamba bado kuna shida kubwa hapo.


YANGA

Mwanzoni mwa msimu uliopita 2023-2024, Yanga ilipata pigo kubwa baada ya kuondoka kwa mshambuliaji wao kinara, Fiston Mayele ambaye alihudumu kikosini hapo kwa misimu miwili ambapo ule wa mwisho alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara. Kabla ya Mayele hajaja Tanzania, kulikuwa na Heritier Makambo. Hawa wote ni raia wa DR Congo. Lakini hapo kati Yanga ilipitia wakati mgumu sana kumpata mshambuliaji kinara kwani iliwahi kuwa na Ditram Nchimbi, Wazir Junior, Yacouba Songne, Michael Sarpong, Sadney Ukihrob, Kalengo Maybin, Juma Balinya na David Molinga walioonekana kushindwa kuifanya kazi yao vizuri. Hiyo ni kabla ya ujio wa Mayele msimu wa 2021-2022.

Makambo alipocheza Yanga msimu mmoja 2018-2019, akajiunga na Horoya AC ya Guinea, kisha 2021-2022 akarejea Yanga ambapo hakuwa tena na makali kama mwanzo. Wakati anarejea akakutana na Mayele ambaye naye alikuwa ndiyo kwanza ametua. Yanga wakawa na safu nzuri ya ushambuliaji ambapo ilibaki kidogo Mayele aibuke mfungaji bora baada ya kuzidiwa bao moja na George Mpole aliyemaliza kinara kwa mabao 17.

Msimu uliofuatia kwa maana ya 2022-2023 Mayele akafunga mabao 17 sawa na Saidi Ntibazonkiza 'Saido' na wote kuwa wafungaji bora.

Hivi sasa Yanga bado haijatangaza usajili wake rasmi, lakini imeripotiwa kwamba imefanya makubaliano na mshambuliaji raia wa Ghana, Jonathan Sowah anayetajwa kwenda kuchukua mikoba ya Joseph Guede ambaye inaonekana uamuzi wa kuondolewa kwake kikosini hapo kumeleta mvutano mkubwa kwa viongozi.

Mbali na Sowah, Prince Dube naye anatajwa kumalizana na timu hiyo akitokea Azam alipovunja mkataba wake.

Ikumbukwe kwamba, katika usajili wa dirisha kubwa mwanzoni mwa msimu uliopita, Yanga ilimsajili Hafiz Konkoni raia wa Ghana kuja kuziba pengo la Mayele, hakucheza sana akaondolewa dirisha dogo na nafasi yake ikachukuliwa na Guede ambaye alikuja kuwaka mbele ya safari akamaliza ligi na mabao sita. kikosini hapo pia kuna Clement Mzize ambaye bado ana muda mwingi wa kuendelea kuonyesha uwezo wake.


AZAM

Katika usajili wa dirisha dogo msimu uliopita mshambuliaji Mcolombia, Franklin Navarro alitua kikosini hapo kwenda kuongeza nguvu akichukua nafasi ya Idriss Mbombo huku dirisha kubwa mwanzoni mwa msimu akiingia Alassane Diao ambaye ameshindwa kuonyesha kiwango bora.

Lakini kuelekea msimu ujao, tayari ametua Mcolombia mwingine, Jhonier Blanco. Hawatakuwa na Prince Dube. Pia ameingia Adam Adam.


SIMBA

Jean Baleke na Moses Phiri waliondoka kipindi cha dirisha dogo msimu uliopita 2023-2024. Kuondoka kwa Baleke, ilionekana kama timu hiyo imekosea kwani alikuwa ndiye kinara wa mabao kikosini hapo akifunga nane ndani ya Ligi Kuu. Phiri manne.

Nafasi zao dirisha dogo wakaingia Pa Omar Jobe na Freddy Michael Kouablan ambao mashabiki wengi wa Simba wamewakataa kutokana na kushindwa kuvaa viatu vya walioondoka. Freddy alipambana akamaliza ligi na mabao sita.

John Bocco ambaye msimu uliopita haukuwa mzuri kwake kutokana na majeraha kumuweka nje muda mrefu amepewa mkono wa kwaheri.

Taarifa zilizopo hivi sasa Simba ipo katika maboresho ya eneo lao la ushambuliaji ikitua kwa Steven Mukala raia wa Uganda. Pia kuna kiungo mshambuliaji Joshua Mutale anayekwenda kuchukua nafasi ya Saidi Ntibazonkiza aliyeagwa akiwa amemaliza ligi na mabao 10 akiibuka kinara kikosini hapo.

Ifahamike kuwa, siyo kwamba maeneo mengine hayafanyiwi marekebisho, bali katika ushambuliaji ndiyo kunaonekana kuna shida kubwa kwani hata takwimu za ufungaji zinajieleza.

Msimu uliopita, kinara wa mabao alikuwa Stephane Aziz Ki aliyefunga 21 akifuatiwa na Feisal Salum (18), kumbuka hawa wote ni viungo. Mshambuliaji aliyekuwa na mabao mengi ni Wazir Junior akiwa na kikosi cha KMC alifunga 12. Takwimu hizo zinaonyesha wazi kwamba tatizo la kuwa na mshambuliaji hodari ndani ya ligi yetu ni ishu ya wote lakini pia viongozi nao wanatajwa kuchangia hilo.

Katika sakata la Guede pale Yanga, licha ya kwamba ameingia dirisha dogo, lakini amefanya kazi nzuri ya kufunga mabao akimaliza na sita sawa na Clement Mzize aliyeanza mwanzoni mwa msimu.

Guede anataka kuondolewa kama ripoti zinavyosema ingawa Kocha Miguel Gamondi anatamani kuendelea naye. Baleke aliondolewa Simba akiwa kinara wa mabao na hadi ligi inamalizika hakuna mshambuliaji asilia kikosini hapo aliyekaa juu kwa mabao zaidi yake. Mchezaji kama huyo unamuondoa unahitaji wa aina gani?

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat', amesema wamekuwa wakifanya usajili kulingana na ripoti ya mwalimu na kuimarisha eneo ambalo linaonekana kuwa na shida.

"Usajili unafanyika kulingana na sehemu ambayo inaonekana kutokuwa imara na hiyo inatokana na ripoti ya kocha," alisema Popat.