Yanga yashusha mashine mpya

MASHABIKI wa Yanga wana kila sababu ya kucheka tu kwa sasa. Kwanza wameimaliza ile vita ya Ditram Nchimbi baada ya kupata leseni kama ilivyo kwa Adeyum Saleh na Tariq Seif, lakini pia ITC ya straika wao mwili jumba, Yikpe Gnamein bado kidogo tu itue nchini.

Lakini katikati ya shangwe hilo, mabosi wa klabu hiyo wameshusha mashine nyingine kali kutoka Zambia ambaye katika tizi la saa mbili akiwa na kikosi cha Yanga jana asubuhi ilitosha kuwakuna mabosi wa klabu hiyo, huku beki Lamine Moro akisisitiza atawafaa kama ataisainishwa mkataba.

Unaambiwa Yanga haikutaka kusikia tena hadithi kama za winga wa Msumbiji Luis Miquissone waliyekaribia kumnasa lakini ghafla Simba wakatibua dili kwa fedha zao nyingi.

Walichofanya ni kumshusha straika mmoja anayejua kutumia mguu wa kushoto kwa ufundi mkubwa kuja kujaribiwa kidogo katika kujiridhisha kisha wamsajili.

Straika huyo ni anatajwa kuwahi kuitumikia Buildcon ya Zambia, amefahamika kwa jina moja tu la Eric na jana asubuhi na jioni alikuwa mazoezi ya timu hiyo, huku akionyesha uwezo mkubwa katika kumiliki mpira, kupiga chenga, kugawa vyumba na kupiga mashuti mbele ya mabeki katili wa Jangwani.

Yanga, iliyopanga kutimka kwenda Morogoro, iliahirisha mpango huo wa kwenda Moro na kuweka ratiba yao ya mazoezi ikiwa na usiri mzito lakini Mwanaspoti likayanasa na kumshuhudia straika huyo mwenye mwili wa kawaida tu akifanya vitu vyake kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria huku ulinzi ukiwa mkali mithili kuna kiongozi wa nchi eneo hilo.

ALIVYOKIWASHA

MAZOEZINI

Akiwa mazoezini licha ya kutofunga bao, mshambuliaji huyo alionyesha kuwa hatari kwa kuwa na mbinu nyingi za kuwakimbia mabeki kwa chenga za akili akitumia silaha yake ya mguu wa kushoto.

Mbali na mbinu zake hizo jamaa ameonyesha pia umahiri katika kucheza kwa ushirikiano akitoa pasi safi na kibaya zaidi kwa Simba ambacho hawatopenda kukisikia ni jinsi alivyo hana uchoyo katika kutoa pasi za mabao maeneo ambayo angeweza hata kufunga.

Uwezo huo Mwanaspoti lilishuhudia mabosi wa klabu hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla aliyefuatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Salim Rupia wakitingisha kichwa wakionyesha kumkubali Mzambia huyo huku wakiongea kwa sauti ya kunong’ona.

LAMINE AKOLEZA

Inaelezwa beki Lamine Moro aliyezusha taharuki ya kukosekana kwenye mchezo dhidi ya Simba amewaambia mabosi wa klabu hiyo kwamba jamaa anajua wala hana shaka naye endapo watamalizana naye.

Mghana huyo inaelezwa aliwahi kukutana na straika huyo alipokuwa Buildcon ambayo Mwanaspoti linafahamu kuwa klabu hiyo tayari imeshawachukua waliokuwa makocha wawili wa Yanga Mwinyi Zahera na msaidizi wake Noel Mwandila.

“Lamine amewaambia viongozi wenzetu na hata makocha kwamba anamjua huyu jamaa ni mchezaji mzuri na atasaidia timu na taarifa za huko mazoezini sio mbaya ngoja tusubiri mpaka kesho (leo) tutajua taarifa kamili kwa kuwa hata mwenyekiti Msolla alikuwepo na amemuona,” alisema moja wa mabosi wa klabu hiyo.

Wakati Lamine akimpigia chapuo mshambuliaji huyo, beki huyo amezusha utata juu ya kuwepo katika mchezo baina ya Simba kutokana na taarifa za kuwa na kadi tatu za njano, ingawa Yanga wanasisitiza ana kadi mbili pekee.

ITC YA YIKPE

Katika hatua nyingine Hati ya Kimataifa ya Uhamisho (ITC) ya straika mwenye mwili jumba, Yikpe Gnamien, imesaliwa na muda mchache kabla ya kutua mikononi mwa Yanga kutoka Gor Mahia ya Kenya.

Mmoja wa viongozi wa Yanga alilidokeza Mwansspoti walishawasilisha maombi ya kibali kwa Yikpe ili aliwahi pambano la Jumamosi dhidi ya Simba na kuna matumaini ya kuipata baada ya Gor Mahia kuelezwa haina hiyana na mchezaji wao huyo aliyewafungia mabao mawili katika KPL.

“Nadhani kabla ya Jumamosi tunaweza kuipata kwani, tulishatuma maombi yetu kwa TFF na kuna dalili nzuri kwa Gor Mahia kuiachia,” alisema kiongozi huyo.