Serikali ya Awamu ya tano ilivyofuta ufalme wa Manji

Mwenyekiti na Mfadhili wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji. Picha na Maktaba

Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu Tanzania, Yusuf Manji (49) amezikwa jana Florida nchini Marekani, akiacha historia ya kuwa miongoni mwa wawekezaji wakubwa waliowahi kutokea nchini.

Heshima na jina lake, lisingekuwa kitu kipya katika masikio ya Watanzania wengi nyakati hizo, hiyo ilitokana na utajiri wake, kadhalika kujihusisha kwake na uwekezaji katika mpira wa maguu.

Manji aliyefariki dunia juzi nchini Marekani, alikuwa mmoja kati ya wafanyabiashara wenye uwekezaji wa takriban Dola 700 milioni za Marekani (zaidi ya Sh1.8 trilioni) katika kampuni yake ya Quality Group Limited (QGL).

Katika nyakati zake, Klabu ya Soka ya Yanga ilistawi, ikifurahia mfululizo wa ushindi katika Ligi Kuu, ingawa dhamira yake ya kujenga uwanja wa klabu hiyo halikuwahi kutimia.

Ni katika nyakati hizo, Manji aligeukia siasa na kuwa Diwani wa Mbagala Kuu, Dar es Salaam lakini upepo wake ulianza kubadilika mara tu ilipoingia madarakani Serikali ya Awamu ya tano.

Awamu hiyo iliyoongozwa na Hayati John Magufuli, ilianza kwa kuonyesha msimamo wa kupinga ufisadi na uzembe, huku akiahidi kukomesha hali hiyo na kurejesha uwajibikaji.

Utawala wa Magufuli ulianzisha uchunguzi mkali katika sekta mbalimbali, ukiwa na lengo la kuondoa ufisadi na usimamizi mbovu.

Hatimaye uchunguzi huo ulimfikia Yusuf Manji na kampuni yake ya QGL. Madai yaliibuka kuhusu ukwepaji wa kodi na mbinu zisizo sahihi za biashara ikiwa ni pamoja na zabuni ya kusambaza sare za jeshi.

Serikali kupitia maagizo ya Magufuli, ilianzisha uchunguzi wa shughuli za kifedha na kibiashara nchini, ikijumuisha himaya ya Manji.

Wakati huo ndipo utajiri wake ulianza kuingia katika mashaka, baada ya uchunguzi kubaini makosa ya kibiashara, ukwepaji wa kodi na hata kusababisha mfanyabiashara huyo kuingizwa hatiani.

Mwaka 2017, katika moja ya kesi hizo kubwa, kampuni yake ya Farm Equipment ilifungiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akidaiwa zaidi ya Sh12 bilioni, ambazo hazikuwa zimelipwa.

Kwenye siasa ambako aliingia nako kukawa tatizo, kwani kutokana na changamoto za kisheria, akiwa rumande alipoteza nafasi yake kama Diwani, baada ya kushindwa kuhudhuria vikao sita vya baraza la madiwani mfululizo.

Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo alisema Manji amevunja kifungu cha 8, kifungu cha 25(5) (a) (b) cha sheria ya Serikali za mitaa ya mwaka 1982 na kanuni za manispaa.

Hata hivyo, uamuzi huo ulifanyika wakati Manji akiwa rumande kwa miezi kadhaa akisubiri kusikilizwa kwa mashitaka ya kiuchumi na usalama wa Taifa yaliyokuwa yakimkabili enzi za utawala wa Hayati Magufuli.

Licha ya kuachiliwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuondoa mashitaka hayo, bado hali ilikuwa mbaya kwa Manji baada ya Magufuli kumfutia umiliki wa shamba lake la ekari 714 Kigamboni, Dar es Salaam.

Vyombo vya habari, ambavyo hapo awali vilijaa habari za umahiri wa biashara na misaada yake kwa kijamii, vikageuka kumwandika kuhusu ripoti za uchunguzi na changamoto zinazomkabili.

Hali ilizidi kuwa mbaya kutoka pande zote. Taasisi za udhibiti zilimtaka kuzingatia sheria, wanahisa walihitaji hakikisho la uimara wake na umma ulifuatilia kwa karibu habari hizo.

Mfanyabiashara ambaye aliwahi kuwa na nguvu alijikuta akijikunyata kwenye vita ya kisheria na kukabiliana na changamoto nyingi ili kuokoa sifa na masilahi yake ya biashara.

Manji na timu yake ya kisheria walijitahidi kujitetea, wakipinga madai hayo na kusisitiza dhamira yao ya kufanya kazi ndani ya mipaka ya sheria.

Hata hivyo, hali ya kisiasa haikuwa na huruma na msimamo wa Serikali kuhusu uwajibikaji haukuacha nafasi ya maafikiano.

Kadri siku zilivyokuwa zikisonga, himaya ya QGL iliyokuwa haiwezi kuguswa ilianza kusambaratika. Vita ya kisheria iligusa rasilimali, shughuli za biashara zilipungua kutokana na uchunguzi uliokithiri na mtazamo wa umma ulitetereka.

Historia ya Yusuf Manji kama mwekezaji mkubwa wa biashara ilibadilika na kuwa mfanyabiashara anayepitia nyakati ngumu, akipambana kulinda urithi wake.

Baadaye ulifika wakati kama maji unaweza kusema yameshamwagika. Alikabiliwa na changamoto za kisheria zinazoongezeka, msukosuko wa kifedha, na mabadiliko ya kisiasa, aliamua kujiondoa kwenye biashara zake.

Himaya ya QGL, ambayo hapo awali ilikuwa nguzo ya mandhari ya biashara ya Tanzania, ilipitia mabadiliko na kugawanywa wakati mwanzilishi wake alipokabiliana na athari za mabadiliko ya kisiasa yaliyobadilisha bahati zake.

Baada ya kipindi akiwa nje ya nchi, Manji alirejea Tanzania, akikaa chini kwa utulivu, ambapo mara ya mwisho alionekana hadharani Aprili 22 mwaka huu kwenye mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga iliyofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.


Atakavyokumbukwa

Baadhi ya wananchi na wanasiasa wameeleza Manji atakavyokumbukwa, wakisema enzi za uhai wake alipitia misukosuko mbalimbali katika siasa na biashara.

Wananchi na wanasiasa hao walieleza hayo wakati wakizungumza na Mwananchi kuhusu maoni yao kutokana na kifo cha Manji.

Mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza alisema Manji ni miongoni mwa watu au wafanyabiashara waliotikiswa katika utawala wa Serikali ya awamu ya tano, chini ya Hayati John Magufuli.

“Manji alikuwa ni miongoni mwa watu wasiotikiswa, lakini katika utawala wa awamu ya tano alitikiswa ndipo watu walipoona alama ya utawala wa Hayati Magufuli utakavyokuwa. Alikuwa na nguvu na mfanyabiashara mkubwa na maarufu alikuwa karibu na Serikali hasa za awamu ya tatu na nne.

“Kwanza alikuwa akiogopwa na wabunge hadi wanasheria, lakini alipoingia Hayati Magufuli alimtikisa hadi watu wakashtuka na kuona rangi halisi na kiongozi huyo, kwa sababu mfanyabiashara huyo alikamatwa na kupimwa mkojo,” alisema Kaiza.

Mwaka 2017, Machi alikamatwa na kufikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya aina ya heroini. Katika kesi hiyo, Manji alilazimika kuchukuliwa sampuli ya mkojo ili kubaini kama anatumia dawa hizo.

Hata hivyo, katika uchunguzi ulibaini mkojo huo una dawa aina ya benzodiazepines anazozitumia mfanyabiashara huyo kutuliza maumivu makali au kukosa usingizi.

Naye, meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob aliyewahi kufanya kazi pamoja na Manji wakiwa wajumbe wa jiji la Dar es Salaam, kabla halijavunjwa alisema atamkumbuka mwanasiasa huyo namna alivyowekeza katika kata ya Ubungo.

“Ingawa hakudumu sana katika udiwani, lakini namkumbuka alikuwa mfanyabiashara mkubwa aliyewekeza katika kata yangu ya Ubungo, lakini alipata misukosuko mingi. Manji unaweza kumweka katika makundi yote mfanyabiashara na mwanasiasa,” alisema.


Manji ni nani

Yusuph Manji alizaliwa Oktoba 14, 1975 katika Jiji la Dar es Salaam, Tanzania

Mwaka 1995 alianzisha Kampuni ya Quality Group Limited iliyofahamika Tanzania na Afrika kwa kusambaza bidhaa mbalimbali.

Alisoma shahada ya uhasibu kutoka Chuo cha Hofstra kilichopo jiji la New York, Marekani.

Mwaka 2015, alichaguliwa kuwa Diwani wa Mbagala Kuu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Aliiongoza Yanga kwa miaka mitano akiingia madarakani 2012 na kujiuzulu 2017.

Anakumbukwa na WanaYanga kwa kutwaa mataji manne ya ligi kuu, Ngao ya Jamii na Kombe la Kagame na kuwasajili wachezaji wakubwa kama Kelvin Yondani, Juma Kaseja na Emannuel Okwi.

Amefariki dunia Juni 29, 2024 Jimbo la Florida nchini Marekani alipokuwa akipatiwa matibabu akiwa na umri wa miaka 49.

Enzi za uhai wake alifanikiwa kupata watoto wawili.