Tanzania ilivyotisha kwenye Soka 2024
Muktasari:
- Mafanikio ya Taifa Stars kufuzu kwa mara ya nne kwenye michuano ya AFCON ni hatua nyingine muhimu mwaka huu. Timu hiyo imeonyesha ukuaji mkubwa, safari hii ikiongozwa na kocha mzawa, Hemed Suleiman 'Morocco'
Mwaka 2024 umekuwa wa kihistoria kwa maendeleo ya soka nchini Tanzania, ukionyesha ukuaji mkubwa wa mchezo huo kupitia mafanikio ya klabu na timu za taifa.
Tangu mwanzo wa mwaka, tumeshuhudia hatua za kujivunia kutoka kwa Simba na Yanga kwenye michuano ya kimataifa, rekodi za Taifa Stars, na maendeleo ya vijana kupitia timu kama Ngorongoro Heroes.
Aidha, tukio kubwa la Tanzania kushirikiana na Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa mashindano ya CHAN 2025 linaendelea kudhihirisha kwamba soka la Tanzania limeingia katika enzi mpya ya mafanikio.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, ametoa pongezi kubwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuimarisha michezo, akisema msaada wake umekuwa msingi wa maendeleo haya.
Tukianza na mafanikio ya klabu, Simba na Yanga walitengeneza historia ya kipekee kwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa pamoja. Huu ulikuwa ni ushahidi wa dhamira yao na uwekezaji wa muda mrefu wa klabu hizo, zikiweka Tanzania kwenye ramani ya soka ya kimataifa.
Rais Wallace Karia amezipongeza klabu hizi kwa kuwa mabalozi wa nchi, akisema: “Mafanikio haya yanaimarisha jina la Tanzania katika soka la Afrika, lakini hayawezi kufanikishwa bila mazingira mazuri ambayo serikali imeyajenga.”
Mafanikio ya Taifa Stars kufuzu kwa mara ya nne kwenye michuano ya AFCON ni hatua nyingine muhimu mwaka huu. Timu hiyo imeonyesha ukuaji mkubwa, safari hii ikiongozwa na kocha mzawa, Hemed Suleiman 'Morocco'.
SIMBA,YANGA KIMATAIFA
Kwa mara ya kwanza Machi mwaka huu, Simba na Yanga ziliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabigwa Afrika kwa pamoja ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya nchi hii.
Simba ilifuzu hatua hiyo, baada ya kuichapa Jwaneng Galaxy mabao 6-0 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, huku Yanga ikifanikiwa kufuzu wiki moja nyuma kwa kuifumua CR Belouizdad mabao 4-0, kwenye uwanja huohuo.
Kufuzu kwa timu zote ilikuwa ni jambo la kujivunia kwa kila Tanzania
kwa kuwa ndiyo nchi pekee ambayo ilifanikiwa kupeleka timu mbili robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huo.
Timu hizo ziliweka rekodi ya kumaliza hatua ya makundi zikiwa zimefunga mabao mengi zaidi kuliko nyingine zote, baada ya kila moja kufunga mabao tisa.
Zikifuatiwa na Belouizdad, Mamelodi Sundowns na Asec Mimosas ambazo kila moja ilifunga mabao saba, Espérance de Tunis ilifuzu ikiwa imefunga mabao sita sawa na TP Mazembe.
Rekodi nyingine ambayo iliwekwa na timu hizo mbili ndiyo pekee ambazo zimeshinda michezo miwili tu ya hatua ya makundi, lakini zikapenya kwenda robo fainali.
Simba ilishinda nyumbani dhidi ya Wydad Casablanca 2-0 na Jwaneng Galaxy mabao 6-0, huku Yanga ikishinda dhidi ya CR Belouazdad 4-0 na Medeama 3-0.
TAIFA STARS YAFUZU AFCON
Novemba mwaka huu, Taifa Stars iliandika historia kwa kufuzu kucheza AFCON kwa mara ya nne baada ya kuifunga Guinea bao 1-0 lililofungwa na Simon Msuva dakika ya 61 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Taifa Stars ilifuzu kwa kumaliza nafasi ya pili wakiwa na alama 10 huku DR Congo ikiongoza kundi ikiwa na alama 12 wakati Guinea akiwa na alama 9 katika nafasi ya tatu.
Safari ya Tanzania kwenye AFCON ilianza mwaka 1980, ambapo Taifa Stars ilifuzu kwa mara ya kwanza chini ya kocha wa kigeni, Slawomir Wolk kutoka Poland. Licha ya kuwa mara ya kwanza, timu hiyo ilijitahidi kupambana, lakini ushindani wa kipindi hicho ulikuwa mgumu zaidi.
Miaka 39 ilipita kabla ya Taifa Stars kurejea kwenye mashindano haya ya kifahari mwaka 2019, safari hii chini ya Emmanuel Amunike kutoka Nigeria.
Mwaka 2023, chini ya Adel Amrouche wa Algeria, Taifa Stars ilirejea tena kwenye michuano ya AFCON. Hata hivyo, mafanikio ya mwaka huu yameweka historia, kwani hii ni mara ya kwanza kwa timu kufuzu chini ya mwongozo wa kocha mzawa. Hemed Suleiman 'Morocco'.
TWIGA STARS YAPANGIWA VIGOGO
Desemba mwaka huu, timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ ilifahamu kundi na wapinzani wake katika fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake (Wafcon) 2024 zitakazifanyika mwakani kuanzia Julai 5 hadi Julai 26 huko Morocco.
Katika droo ya upangaji wa makundi hayo ambayo ilifanyika Casablanca, Morocco, Twiga Stars ilipangwa kundi C na timu za Afrika Kusini, Ghana na Mali.
Hii ni mara ya pili kwa Twiga Stars kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake ambapo ya kwanza ilishiriki katika fainali za 2010 zilizofanyika Afrika Kusini ambapo ilimaliza ikiwa imeshika mkia kwenye kundi lake ikitoka sare mechi moja na kupoteza mbili.
NGORONGORO WAMO
Oktoba mwaka huu, Tanzania ilijikatia tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Uganda katika mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA U20 kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge Jijini Dar es Salaam.
haukuwa ushindi mwepesi kwa Ngorongoro Heroes inayofundishwa na Kocha mzoefu, Charles Boniface Mkwasa anayesaidiwa na Kally Ongala na Juma Kasema kocha wa makipa kwani ililazimika kutoka nyuma baada ya beki Brian Toto Majub kuanza kuifungia Hippos dakika ya 46.
Winga wa KVZ ya Ligi Kuu ya Zanzibar, Sabri Dahary Kondo aliirejesha mchezoni Ngorongoro kwa bao lake zuri la kusawazisha dakika ya 73 ambalo lilisindikizwa nyavuni na kipa wa Hippos, Abdu Magada na dakika 90 zikamalika timu hizo zikiwa zimefungana 1-1.
Shujaa wa Tanzania alikuwa mshambuliaji wa JKU ya Ligi Kuu ya PBZ Zanzibar, Jammy Suleiman Simba aliyeifungia Ngorongoro Heroes bao la ushindi dakika ya 119 na kuamsha shangwe kubwa kwa mamia ya mashabiki waliojitokeza Uwanja wa KMC.Hata hivyo vijana hao walitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuifunga Kenya mabao 2-1.
WENYEJI WA CHAN
Septemba mwaka huu, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilithibitisha rasmi Kenya, Uganda na Tanzania kuwa wenyeji wa mashindano ya CHAN 2024, huku fainali hizo zikipangwa kuanza Februari 1 na kumalizika Februari 28, 2025.
Katika kikao cha kamati ya utendaji ya CAF kilichofanyika jijini Nairobi, Rais wa CAF, Patrice Motsepe, alithibitisha tarehe rasmi za mashindano hayo na kutoa pongezi kwa nchi zote tatu kwa maandalizi yao.
Mashindano ya CHAN (Shirikisho la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani) yatashirikisha wachezaji wanaocheza soka la ndani pekee, jambo linalolenga kukuza vipaji na kutoa fursa kwa wachezaji wanaojitokeza ndani ya bara la Afrika.
Kulingana na Rais wa CAF, Patrice Motsepe, mashindano haya ni fursa adhimu kwa wachezaji wa Kenya, Uganda, na Tanzania kuonyesha uwezo wao mbele ya mashabiki wa nyumbani na soko kubwa la kimataifa.
Motsepe alisisitiza kuwa CHAN itachangia sana kuimarisha soka katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, huku akitoa pongezi kwa jitihada za marais wa Kenya, Uganda, na Tanzania katika kuandaa mashindano haya makubwa.
“Nchi hizi tatu zina historia na shauku kubwa ya mpira wa miguu, na nina uhakika mashindano ya mwaka huu yatakuwa bora zaidi na yenye mafanikio kuliko yaliyowahi kufanyika,” alisema Motsepe katika hotuba yake.
PIGO KATIKA SOKA
Februari mwaka huu, familia ya soka ilipata pigo la aliyekuwa Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa ambaye alifariki dunia katika hospitali ya Wilaya ya Temeke alipokuwa akipatiwa matibabu wakati wa uhai wake.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabiti Zakaria amethibitisha taarifa za kifo cha Mwankenwa.
Mwankenwa alihudumu Azam kwa miaka 16 tangu timu hiyo ilipopanda daraja mwaka 2008.