Stars yaambulia sare kwa Ethiopia

Muktasari:
- Taifa Stars imetoka sare ya 0-0 dhidi ya Ethiopia katika mechi ya kwanza ya kufuzu AFCON 2025.
Dar es Salaam. Timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ imeshindwa kuanza vyema mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 baada ya kutoka suluhu na Ethiopia kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi H uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam leo.
Licha ya Stars kuanza kwa kushambulia ikionyesha kuhitaji kupata ushindi ilikosa utulivu pindi ilipokaribia lango la wapinzani na katikati mwa uwanja jambo lililoifanya Ethiopia kuonyesha kutokuwa na wasiwasi.
Kukosa huko utulivu kuliifanya Taifa Stars kutokuwa na madhara langoni mwa Ethiopia hasa katika kipindi cha kwanza.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza Taifa Stars ilipiga mashuti matatu tu ambayo hayakulenga lango kutokana na umakini wa walinzi wa Ethiopia ambao uliinyima nafasi ya kupachika bao nyavuni.
Stars pamoja na kutokuwa na madhara mbele, eneo lake la ulinzi lililiongozwa na kipa Ally Salim lilicheza vyema na kutowapa fursa wapinzani kupata bao.
Katika kipindi hicho cha kwanza, changamoto kubwa ilikuwa ni eneo la kiungo lililokuwa na Feisal Salim, Himid Mao na Novatus Dismas ambalo lilishindwa kuendana na kasi ya Ethiopia ambayo ilitawala eneo hilo.
Hadi filimbi ya mapumziko ilipopulizwa hakuna timu ambayo ilipata bao.
Kipindi pili Taifa Stars ilikianza taratibu kwa kujaribu kuifungua Ethiopia lakini bado ilionekana kukosa ubunifu katika mwa uwanja.
Pamoja na kuingia kwa kasi wakisaka bao wapinzani wao pia walionyesha utulivu kwa kuwaheshimu na kucheza mpira wa kujilinda na kushambukia kwa pamoja.
Mabadiliko ya wachezaji watatu yaliyofanywa kwa kuwatoa Nickson Kibabage, Himid Mao na Edwin Balua nafasi zao zilichukuliwa na Pascal Msindo, Mudathir Yahya na Wazir Junior yaliongeza uhai kikosini na kuifanya Stars ambayo ilibadili aina ya uchezaji.
Mashambulizi iliyofanya yalisaidia kupata kona mbili kipindi cha pili ambazo hata hivyo hazikuzaa matunda kwani uimara wa kipa na mabeki wa Ethiopia ulikuwa wa hali ya juu.
Hakukuwa na mabadiliko yoyote katika matokeo ya mchezo hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa.
Matokeo hyo yameifanya Taifa Stars kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi H la kuwania kufuzu Afcon.
Baada ya mechi dhidi ya Ethiopia, Septemba 10, Taifa Stars itakuwa ugenini huko Ivory Coast kuvaana na Guinea.
KIKOSI CHA STARS
Ally Salim, Nickson Kibabage, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, Dickson Job, Feisal Salum, Himid Mao, Clement Mzize, Mohammed Hussein, Lusajo Mwaitenda, Edwin Balua na Novatus Dismas