Stars ni kufa au kupona AFCON
Muktasari:
- Nigeria na Uganda zitaumana kwenye Uwanja wa Fez, ili kuamua timu moja ya kuifuata Nigeria na ile itakayopenya kupitia kapu ya mshindwa bora (best looser) kutinga hatua ya 16 Bora.
Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ina dakika 90 ngumu usiku wa leo mbele ya Tunisia.
Timu hiyo inayoshiriki fainmali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa mara ya nne tangu mwaka 1980, inahitaji ushindi mbele ya wapinzani wao katika mechi ya mwisho ya Kundi C itakayopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Rabat, mjini Rabat Moroco.
Ni ushindi pekee ndio unaweza kuifanya Stars yenye pointi moja kundini ikishika nafasi ya tatu ili isalie Morocco, la sivyo itafungasha virago kurudi nyumbani kama ilivyokuwa kwa Botswana, Gabon na Guinea ya Ikweta zilizoaga mapema michuano ya ya 35 tangu ilipoasisiwa mwaka 1957.
Stars ilianza kwa kupioteza mechi ya kwanza ya kundi hilo dhidi ya Nigeria kwa mabao 2-1, kisha kulazimishwa sare ya 1-1 na Uganda, hali iliyoifanya iwe na kibarua kizito leo kwani inahitaji ushindi wa aina yoyote kama inataka kusonga mbele kuingia 16 Bora. Tanzania haijawahi kupata ushindi katika miaka yote iliyoshiriki michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Katika fainali za kwanza za mwaka 1980 kule Nigeria, Stars ilipoteza mechi mbili kwa vipigo vya 3-1 kutoka kwa Nigeria na 2-1 kutoka Misri, kisha ikatoka sare ya 1-1 na Ivory Coast, wakati fainali za 2019 ilipoteza zote mbele ya Senegal (2-0_ Kenya (3-2) na Algeria (3-0) na zile zilizopita za Ivory Coast ilipoteza 3-0 kwa Morocco, kisha kutoka sare ya 1-1 na Zambia na kutoka sululu na DR Congo na kote kuanza hatua hiyo ya makundi.
Stars inavaana na Tunisia katika muda mmoja ambao Nigeria iliyofuzu mapema kuingia 16 bora ikiungana na Misri na Algeria kutoka makundi ya B na C itakuwa na kibarua cha kufunga hesabu za mechi za makundi dhidi ya Uganda inayoburuza mkia ikiwa na pointi moja katika Tanzania isipokuwa zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Nigeria na Uganda zitaumana kwenye Uwanja wa Fez, ili kuamua timu moja ya kuifuata Nigeria na ile itakayopenya kupitia kapu ya mshindwa bora (best looser) kutinga hatua ya 16 Bora.
Kwa mechi ya Stars ni ya kufa au kupona kwa Tanzania kwani ikipoteza au kutoka sare itakuwa imehitimisha ushiriki wao wa fainali hizo za 35 tangu kuasisiwa kwa michuano mwaka 1957.
Ni mechi ambayo kocha Miguel Gamondi anapaswa kuingia uwanjani kwa mbinu na mipango madhubuti kama kweli anataka kuivusha Stars hatua inayofuata na kuwa kocha wa kwanza kufanya hivyo katika AFCON akiwa na timu hiyo ya Tanzania. Stars inatakuiwa kuchrza kwa nidhamu na utuliovu mkubwa na kuepuka makosa kama yaliyojitokeza katika mechi mbili zilizopita ambazo ziliigharimu timu hiyo mbele ya Nigeria na Uganda.
Tunisia ni timu inayocheza soka kwa nidhamu kubwa ya kiulinzi, mpangilio mzuri wa kati na mashambulizi ya kushtukiza. Wanajua kulinda matokeo na wamezoea mechi za presha. Kwa Stars, changamoto kubwa itakuwa kuvunja ukuta wao bila kupoteza umakini nyuma, kwani katika mechi zote mbili zilizopita imeruhusu mabao.
Ilipoteza kwa mabao 2-1 kwa Nigeria baada ya kusawazisha bao mara baada ya kipindi cha pili, lakini hata katika mechi ya Uganda licha ya kutangulia kupata bao la penalti mapema kipindi cha pili iliruhusu bao la kusawazisha kwa wapinzani wao dakika ya 80 kisha ikanusurika kipigo baada ya Uganda kupoteza penalti dakika za majeruhi.
Ingawa Tunisia iliyoanza michuano kwa ushindi mnono wa mabao 3-1, ni timu inayofungika kwani katika mechi ya pili dhidi ya Nigeria ilikubali kulala mabao 3-2 na kuifanya iwe moja ya timu zilizoruhusu mabao mengi kundini, ikifungwa manne kama ilivyo kwa Uganda, wakati Tanzania imefungwa matatu kama ilivyo kwa Nigeria.
Huenda kikosi kilichocheza na Uganda, ndicho kinachoweza kuanza mbele ya Tunisia kwa maana ya Zuberi Foba kukaa langoni, huku Haji Mnoga na Mohammed Hussein wakacheza kama mabeki wa pembeni huku Ibrahim Bacca na Bakar Mwamnyeto wakasimama beki ya kati na viungo wakiwa ni Alphonce Mabula, Dismas Novatus na Feisal Salum, huku Kelvin John akasimama kama mshambuliaji akisaidiwa na Simon Msuva na Tarryn Allarakhia.
Hata hivyo, kocha Gamondi ana nyota wengine ambao anaweza pia kuanza nao kama ataamua kufanya mabadiliko akiwamo Seleman Mwalimu, Charles M'Mombwa, Idd Seleman 'Nado' na Yusuf Kagoma ambaye ni mzoefu zaidi kwa eneo la kiungo, mbali na wachezaji wengine wa akiba akiwamo nahodha Mbwana Samatta na Shomary Kapombe, ambao walianzia benchi mechi iliyopita dhidi ya Uganda.
Mabeki wa Stars wanapaswa kuwa makini na washambuliaji Elias Achouri mwenye mabao mawili hadi sasa, Hazem Mastouri na Sebastian Tounekti ambao ni wasumbufu na wanaocheza kwa kasi, mbali na viungo na mabeki wanaopandisha mashambuli kama Montassar Talbi na Ali Abdi wenye bao moja kila mmoja.
Rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana mara mbili tangu mwaka 2020 zilipokuwa katika kundi moja la mechi za kufuzu AFCON ambapo Tunisia ilishinda mechi ya nyumbani kwa bao 1-0 na kulazimisha sare ya 1-1 ugenini, kuonyesha kuwa ni timu zisizochekana sana, japo kwa viwango vya soka vya FIFA Tunisia ipo juu zaidi.
Mapema kocha Gamondi alisema mechi ya leo ni ngumu kutokana na ubora wa Tunisia, lakini watashuka uwanjani kupambana kuhakikisha wanamaliza vyema mechi za makundi, huku akionyesha kusononeshwa na matokeo ya sare dhidi ya Uganda kwa vile timu ilionekana ilikuwa ikiandika historia ya kupata ushindi wa kwanza katika AFCON.
Mfungaji kinara wa michuano ya AFCON kwa Tanzania, Simon Msuva naye alisema imani yake ni kwamba AFCON kwao bado haijaisha hadi pambano hilo liiishe dhidi ya Tunisia akiwaomba Watanzania waiombee dua njema na kuibuka na ushindi wakati wakiombea pia wapinzani wao Uganda wachemshe kwa Nigeria.
Mbali na mechi hizo za Kundi C, pia leo kuna mechi nyingine mbili zitakazopigwa kuanzia saa 4:00 usiku za Kundi A ambaopo Comoros itavaana na Mali ya kipa Diarra Djigui anaidakia Yanga, huku Zambia itakuwa na kibarua mbele ya wenyeji Morocco inaoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne baada ya mechi mbili za awali.
Mali yenyewe ina pointi mbili ikishika nafasi ya pili kama ilivyo kwa Zambia na inahitaji ushindi ili kutinga hatua inayofuata, huku Comoros ikihitaji ushindi na kusikilizia matokeo ya wenyeji dhidi ya Chipolopolo, kwani kama Zambia itapoteza kwa Morocco na Comoros kuifunga Mali hizo mbili zitafuzu 16 Bora na kinyume chake inaaga.