Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SPOTI DOKTA: Shabiki fanya haya kujikinga na kiribatumbo

Muktasari:

  • Kule kimataifa usiku wa juzi Jumanne na jana Jumatano katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kulikuwa na mechi kali za 16 bora ikiwamo ile ya Manchester City na Real Madrid ambapo wenyeji walilala 2-3.

Katika Ligi Kuu Bara kwenye mechi za wiki hii ilishuhudia Yanga na JKT Tanzania zikitoka 0-0. Na juzi Jumanne, Simba nayo ilicheza ikifanikiwa kuibamiza Tanzania Prisons mabao 3-0 na kukaa kileleni ikiwa na pointi 47.

Kule kimataifa usiku wa juzi Jumanne na jana Jumatano katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kulikuwa na mechi kali za 16 bora ikiwamo ile ya Manchester City na Real Madrid ambapo wenyeji walilala 2-3.

Jicho la kitabibu lilitazama mechi hizo zote katika upande wa watazamaji yaani mashabiki ambao walikuwa wakishangilia na kupaza sauti kuzipa hamasa timu zishinde. Katika utafiti kuona kwa macho kulikuwa na idadi kubwa ya mashabiki ambao walivaa jezi za timu huku wakionyesha kuwa na viribatumbo au vitambi.

Kiribatumbo ni kiashiria mojawapo cha uzito uliozidi au unene na ndiyo maana wataalamu wa afya hupima mzunguko wake kama moja ya njia ya kutathimini tatizo la unene. Unene ni ishara kuwa mwili haushughulishwi na kazi ngumu au mazoezi ndio maana kuna mrundikano wa mafuta mengi mwilini.

Tofauti na wachezaji ambao miili yao ni mikakamavu kutokana na kuwa na shughuli ngumu mara kwa mara kiasi kwamba hakuna unene wala viribatumbo. Nikweli mtazamaji wa soka anakwenda uwanjani kushangilia timu ambapo wachezaji wake wote hakuna ambaye ana kiribatumbo. Hii ni ishara kuwa mazoezi ndio njia rahisi ya kuondoa kiribatumbo.

Kiribatumbo ni matokeo ya ulaji holela wa vyakula na kutoushughulisha mwili na mazoezi au kazi zinazoutembeza. Kuendelea kuwepo kwa unene kunatuweka katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo ya moyo na mishipa ya damu.

Leo katika kona hii nitaeleza namna rahisi ya kuondoa kiribatumbo kwa wale mashabiki wa michezo ili waweze kujikinga na tatizo la unene ambalo ndilo kihatarishi namba moja kupata magonjwa yasiyoambukiza.

JINSI YA KUKIKABILI

Kufanya mazoezi mepesi na udhibiti wa ulaji holela wa vyakula hasa vinavyonenepesha ambavyo ni pamoja na vile vyenye mafuta mengi, sukari na wanga mwingi. Ulaji wa vyakula visivyokobolewa mfano mikate ya ata ambayo unapoila humfanya mtu kujisikia kuwa ameshiba, lakini pia uwepo mashudu ambayo huwa hayana wanga yapokuongeza ujazo. Hivyo husaidia kumpunguzia wanga ambayo huchangia kunenepa na kupata kitambi.

Vilevile ulaji wa vyakula vya nyuzinyuzi kama mbogamboga hasa zile mbichi. Pale unapoitazama sahani yako yenye mduara wa nyuzi 360 ya mlo mkuu iwe na chakula robo wanga, robo protini na nusu iwe ni mbogamboga na matunda.

Utahitaji kuwa na mwenendo na mtindo bora wa maisha kwa kutenga muda mwingi wa mazoezi mepesi ambayo yanahitaji dakika 150 kwa wiki yaani sawa na dakika 30 kwa siku katika siku tano. Kwa wenye viribatumbo ambao ni wanywaji pombe ni muhimu kuacha au wakishindwa wapunguze kiasi angalau kuwa mnywaji wa mwishoni mwa wiki na sio kila siku.

Kwa upande wa mazoezi sio kila zoezi lina matokeo makubwa katika kudhibiti kiribatumbo. Yapo mazoezi ambayo huhitaji kwenda vituo vya mazoezi ambayo yanaonyesha kuwa na matokeo makubwa katika kudhibiti tatizo hili. Mazoezi mepesi yanasaidia kuufanya mwili kushughulisha viungo vingi hivyo kuchoma mafuta yaliyorundikana ikiwamo eneo la kitambi.

Lakini, inashauriwa ili kuweza kuchoma mafuta ya ziada ni pale utakafanya mazoezi mepesi kwa muda wa dakika 30 kuendelea. Ni muhimu kabla ya mazoezi yoyote lazima mwili uandaliwe kwa mazoezi ya viungo kwanza ili kuweka tayari  viungo kufanya mazoezi kwa ufanisi.

Zoezi la kukimbia kidogokidogo ni zuri ambalo linaweza kuwafaa vijana zaidi. Watu wazima pengine kukimbia ni changamoto wanaweza kufanya zoezi la kutembea, lakini kwa mtindo wa kutupa mikono kama vile watembeavyo askari. Mtindo huo husaidia kushughulisha maeneo mengi ya mwili ikiwamo misuli ya eneo la tumbo. Tumia 'app' za simu kutazama zoezi la kutembea hatua 10,000 kwa siku.

Kuruka kamba ni moja ya zoezi rahisi lenye matokeo makubwa katika kukabiliana na kiribatumbo. Tafiti zinaonyesha zoezi hilo likifanywa kwa ufanisi linasaidia kupunguza tatizo kwa haraka. Zoezi lingine ni kuogelea. Pale unapofanya zoezi hilo linahusisha utendaji wa misuli mingi ikiwamo ile ya tumbo.

Ili kukabiliana na tatizo hilo kwa umaridadi zaidi inahitaji pia kufanya mazoezi yanayolenga moja kwa moja kushughulisha misuli ya tumbo ambayo utayafanya ukiwa umetulia. Ili kuleta matokeo chanya zaidi mazoezi mepesi yanaweza kuchanganywa na ya viungo ambayo yanalenga kuishughulisha misuli ya tumbo.

Pia tumia mbinu ya muda mwingi na mara kukaza misuli ya tumbo hata unapokuwa katika kazi zako za kila siku inasaidia kuishughulisha misuli ya tumbo. Unaweza kutumia dakika 30-60 kufanya mazoezi mepesi na dakika 10 yale ya moja kwa moja ya tumbo. Baada ya mazoezi yoyote ni muhimu pia kutumia dakika tano za mazoezi ya kuupoza mwili.

Kwa mtazamaji anaweza kujiunga na vikundi vya ukimbiaji na mabonanza ya michezo au kushiriki mara kwa mara katika mbio za marathoni.

Pakua video mbalimbali au app zinazoonyesha aina hiyo ya mazoezi ya kuondoa kiribatumbo. Fika katika huduma za afya kwa ushauri na jenga utamaduni wa kuchunguza afya angalau miezi sita mara moja.

CHUKUA HII

Kinga ni bora kuliko tiba. Chukua hatua mapema kwa kuanza kufanya mazoezi mepesi na kudhibiti ulaji holela wa vyakula. Vilevile epuka mienendo na mitindo mibaya ya maisha ikiwamo ulevi na utumiaji tumbaku.