Slot kuiga mavitu ya Arsenal EPL

Muktasari:
- Licha ya Liverpool kuwa mbele ya Arsenal kwa pointi 13, ikiwa karibu kutwaa ubingwa, bado kuna udhaifu kwenye timu yao kwenye baadhi ya maeneo.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot anaamini ni suala la muda tu kabla ya timu yake kufikia kiwango cha Arsenal kwenye kuwa tishio katika mipira ya kutengwa.
Licha ya Liverpool kuwa mbele ya Arsenal kwa pointi 13, ikiwa karibu kutwaa ubingwa, bado kuna udhaifu kwenye timu yao kwenye baadhi ya maeneo.
Kwa mujibu wa tovuti ya WhoScored, Liverpool imefunga mabao sita pekee kutokana na mipira ya kutengwa msimu huu ikiwa ni timu ya nne kufunga mabao machache ya aina hiyo.
Kwa upande mwingine, Arsenal wamefunga mabao 13 kutokana na mipira ya kutengwa, na wamekuwa miongoni mwa timu hatari zaidi kwa kipindi cha misimu michache iliyopita katika aina hiyo ya mipira.
Hata hivyo, Slot anaamini uwezo wa Arsenal katika eneo hilo unatokana na muda mrefu ambao makocha wake wameutumia kuwafundisha wachezaji na kujenga mbinu za kufanikiwa katika hilo.
Akizungumza baada ya ushindi mwembamba dhidi ya Leicester, kocha wa Liverpool alisema:
“Msimu huu kazi tuliyoifanya hadi sasa ni kubwa, tumejaribu kuboresha baadhi ya maeneo lakini nafikiri ni kawaida kwa benchi la ufundi lililokuwa na timu kwa miezi sita au 10, kutokuwa na usahihi kwenye maeneo yote,”
“Arsenal ina uwezo mzuri wa kupiga na kufunga kutokana na mipira ya kutengwa kwa sababu wamekuwa na makocha wao hawa kwa muda mrefu hivyo wamepata muda mwingi wa kuelekeza na kuandaa mbinu. Kawaida huwa tunaanza na jinsi timu itakavyocheza, itakavyozuia na mwisho ndio tutaangalia mbinu za kupiga mipira ya kutengwa.”
“ Mikel Arteta amefanya kazi kwa muda mrefu na sasa timu hiyo ni nzuri katika kila sehemu ya na wanaonekana kuwa mabingwa wa dunia katika mipira ya kutengwa.”
Kocha mkuu wa Arsenal, Arteta, hapo awali alisifia sana kocha wa mipira ya kutengwa wa Arsenal, Nicolas Jover ambaye ndio amefanya mabadiliko makubwa na kuifanya timu iwe hatari katika mipira ya aina hiyo.