Liverpool bado mechi mbili, Man United, Spurs zaambulia vipigo

Muktasari:
- Liverpool sasa inahitaji pointi sita sawa na kushinda michezo miwili ijihajikikishie Ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya West Ham United katika mwendelezo wa Ligi Kuu England, Liverpool sasa ina kibarua chepesi iwe bingwa ikihitajika kushinda mechi mbili tu kati ya sita ilizobakiza.
Mohamed Salah ambaye ametoka kuongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuwatumikia majogoo wa Jiji la Liverpool, ameendelea kuonyesha kiwango bora baada ya kutoa pasi ya bao la kwanza lililofungwa na Luis Diaz katika dakika ya 18.

Baada ya kutoa pasi ya bao, Mohamed Salah hadi sasa amehusika katika mabao 45 ambapo amefunga mabao 27 na kutoa pasi za mwisho 18 katika michezo 32 ya Ligi Kuu aliyocheza.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Liverpool ikiwa mbele kwa bao moja hadi kipindi cha pili kilipoanza Liverpool iliruhusu bao katika dakika ya 86 baada ya beki, Andy Robertson kujifunga na kufanya matokeo yawe 1-1.
Liverpool iliendelea kufanya mashambulizi hadi ilipofika dakika ya 89 ambapo beki, Virgil Van Dijk alifunga bao la pili kwa kupiga kichwa mpira wa kona uliopigwa na Alexis Mac Allister na kuihakikishia timu yake kupata pointi tatu huku ikiongeza tofauti ya pointi 13 dhidi ya Arsenal yenye pointi 63 inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Baada ya kufunga bao la ushindi beki wa Liverpool, Virgil Van Dijk amekuwa mlinzi wa kati ambaye amefunga mabao mengi kuliko mwingine tangu ajiunge na timu hiyo, Septemba 2015.
Michezo ambayo Liverpool inahitajika kushinda ili iwe bingwa, inaweza kupungua endapo wapinzani wao wa karibu katika mbio za Ubingwa, Arsenal ikipoteza dhidi ya Ipswich Town kwenye mchezo ujao wa Ligi kuu England.

Katika michezo mingine ya EPL iliochezwa leo Tottenham ilikubali kipigo cha mabao 4-2 kutoka kwa Wolverhampton.
Chelsea ikiwa darajani, Stamford Bridge imelazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi Ipswich Town huku ikishuka hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 54 wakati Ipswich yenyewe imesalia katika nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa pointi 21.

Mchezo mwingine ni ule uliochezwa kwenye uwanja wa St. James Park ambapo imeshuhudiwa Newcastle United ikipeleka msiba mzito kwa Manchester United baada ya kuifunga mabao 4-1.
Mabao ya Sandro Tonali katika dakika ya 24, Bruno Guimaraes dakika ya 77 pamoja na Harvey Barnes ambaye amefunga mawili katika dakika ya 49 na 64 yametosha kuipa ushindi Newcastle United huku bao la kufutia machozi la United likifungwa na Alejandro Garnacho katika dakika ya 37.

Baada ya ushindi huo Newcastle United imesogea hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 56 ikiishusha Manchester City yenye pointi 55 hadi nafasi ya tano huku Manchester United ikishika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 38.