Singida BS, Simba heshima imetawala

Muktasari:
- Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 37 na Singida Black Stars inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 33.
Dar es Salaam. Homa ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Singida Black Stars na Simba kesho kwenye Uwanja wa Liti, Singida inazidi kupamba moto baada ya makocha wa timu hizo kila mmoja kusema anaheshimu ubora wa mpinzani wake.
Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo mkoani Singida, kocha Ramadhan Nsanzurwimo wa Singida Black Stars na Fadlu Davids wa Simba kila mmoja amesifu ubora wa kikosi cha mwenzake, wote wakitabiri mechi itakuwa ngumu.
“Utakuwa mchezo mgumu na sisi tumejiandaa kutokana na ubora wa Simba. Tuna ubora kwenye kikosi chetu, tunajua Simba inakuja na maswali ya kutuuliza na sisi tutawajibu na sisi tuna maswali yetu ya kuwauliza. Ni mechi inayohitaji umakini sana.
“Tunaiheshimu Simba lakini hatuiogopi. Kutokana na wachezaji tulionao na timu yetu na tuko nyumbani, tuko na vitu vyote ambavyo tunaweza kuvitumia ili tushinde vita hii. Pointi tatu zitakuwa na umuhimu sana,” amesema Nsanzurwimo.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids amesema wanafahamu wanacheza na timu imara, hivyo wamejiandaa vyema kwa ajili ya mechi hiyo.
“Tunajua tunakutana na timu nzuri sana yenye wachezaji wazuri na inayofundishika. Ni timu ambayo inafunga na ina ubora kote katika eneo la kuchezea. Lakini hatutakiwi kufikiria ni kwa namna gani tunaweza kuwadhibiti kufunga ila tunafikiria zaidi kufunga dhidi yao.
“Hauwezi kuchezesha kikosi kilekile kwenye kila mechi. Ni ngumu kumwambia mchezaji acheze kila mechi na akupe kiwango kilekile. Jambo la muhimu kwetu ni kuhakikisha tunajitahidi kuwa na mwendelezo,” amesema Davids.
Timu hizo mbili zinakutana huku Simba ikiwa na mwendelezo bora zaidi wa kufanya vizuri kwenye ligi ingawa Singida Black Stars nayo mambo yanaonekana kuiendea vizuri.
Katika mechi tano zilizopita za Ligi, Simba imepata ushindi mara zote huku Singida Black Stars ikipata ushindi mara tatu, kutoka sare moja na kupoteza mechi moja.
Simba ikipata ushindi katika mechi ya leo itafikisha pointi 40 ambazo zitaifanya iendelee kuongoza msimamo wa ligi na Singida Black Stars ikipata ushindi itapanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 36.
Uwanja wa nyumbani umekuwa silaha ya Singida Black Stars, kwani ikiwa huko imepoteza mechi moja tu kwenye Ligi kati ya nane, wakishinda mechi tano na kutoka sare mbili.
Simba nayo imekuwa tishio ugenini msimu huu kwani imeshinda mechi zote sita ilizocheza ugenini msimu huu.