Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Azam vs JKT ni vita ya ulinzi, ushambuliaji

Ni takribani siku kumi zimepita tangu Azam FC icheze mechi ya Ligi Kuu Bara ambapo leo inaingia tena uwanjani kupambania pointi.

Azam ambayo ni mwenyeji wa mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar saa 1:00 usiku, inakutana na JKT Tanzania, timu ambayo siku tatu zilizopita ilicheza na Simba, ikapoteza kwa bao 1-0 la dakika za jioni kupitia mkwaju wa penalti.

JKT Tanzania imekuwa na kiwango kizuri katika kujilinda ikishika nafasi ya nne kwa timu zilizoruhusu mabao machache (9) baada ya Simba (5), Yanga (6) na Azam (7), unaweza kuwa mtihani mwingine kwa Azam ambayo nayo suala la kufunga ipo vizuri. Hivyo tunakwenda kushuhudia vita ya walinzi wa JKT Tanzania na washambuliaji wa Azam.

Ndani ya Azam, Feisal Salum ndiye mchezaji aliyehusika na mabao mengi (11) katika ligi msimu huu akifunga manne na asisti saba. Ni mchezaji wa kuchungwa zaidi na JKT Tanzania. Si yeye tu, hata Nassor Saadun ambaye ni mshambuliaji wa kikosi hicho mwenye mabao manne, ni mchezaji hatari.

Eneo la ushambuliaji la Azam mbali na nyota hao wawili, pia Idd Seleman mwenye mabao mawili na asisti mbili, amekuwa msumbufu kwa wapinzani kama ilivyo kwa Gibril Sillah aliyefunga matatu.

Azam inakutana na JKT Tanzania ikiwa na kumbukumbu ya kutoka suluhu katika mchezo wa duru la kwanza msimu huu ambao ulihitimisha safari ya kocha Youssouph Dabo aliyempisha Rachid Taoussi.

JKT Tanzania imeonyesha kuwa timu ngumu kufungika katika michezo mitano iliyopita ya ligi ikiruhusu bao moja tu dhidi ya Simba tena kwa mkwaju wa penalti. Safu hiyo inaongozwa na kipa, Yakoub Suleiman akisaidiana na mabeki David Bryson, Edson Katanga na Wilson Nangu.

Ugumu huo umemfanya Taoussi kusema kwamba ataingia uwanjani na mpango mbadala kuhakikisha anaifungua ngome hiyo ili kupata ushindi usiokuwa na presha.

Timu hizo zinakutana huku rekodi baina yao katika mechi tisa zilizopita za ligi tangu mwaka 2018 zikiibeba zaidi Azam, ikiwa imeshinda mara sita, JKT Tanzania haijawahi kushinda huku tatu zikiisha kwa sare.

Licha ya Azam kubebwa na rekodi, lakini kocha Taoussi aliyepata nafasi ya kuwaona maafande hao katika mchezo dhidi ya Simba kuna vitu amegundua na atatumia kama njia ya kuikabili JKT kwa hesabu kali.

“Nimeona uwezo wa JKT katika mchezo uliopita, ni timu yenye ngome imara, lakini Azam tunahitaji ushindi katika mchezo huu ili kuendelea kupigania malengo tuliyonayo. Tutatumia mbinu mbalimbali kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Taoussi.

Kocha wa JKT Tanzania, Ahmed Ally, alisema: “Azam ni timu kubwa na tunawaheshimu, lakini sisi tumejiandaa na tuna lengo la kupata matokeo mazuri. Hatutakubali kupoteza mchezo huu. Tumefanya maandalizi mazuri na tuna imani ya kupata matokeo bora.”

Kwa sasa Azam ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33 sawa na Singida Black Stars iliyopo ya nne zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, ilihali JKT Tanzania ni ya nane ikivuna pointi 19.