Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga raha, ikiendeleza ubabe kwa Dodoma Jiji

Muktasari:

  • Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 36.

Dar es Salaam. Yanga imeendeleza historia yake tamu dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Ligi Kuu baada ya leo kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Ushindi huo umeifanya Yanga ifikishe idadi ya mechi tisa ilizocheza na Dodoma Jiji kwenye ligi bila kupoteza ambapo katika mara tisa ambazo timu hizo zimekutana, Yanga imeshinda mechi nane na zimetoka sare moja.

Ikitumia vyema makosa ya mara kwa mara ambayo safu ya ulinzi ya Dodoma Jiji iliyafanya katika mechi ya leo, Yanga ambayo ilitawala kwa muda mrefu, ilionyesha dalili za kumaliza mechi mapema kipindi cha kwanza baada ya kumaliza dakika 45 za mwanzoni ikiwa na uongozi wa mabao 3-0.

Mzize ndiye alitangulia kuifungia Yanga bao katika mechi ya jana katika dakika ya 19 akimalizia kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Pacome Zouzoua.

Dakika 16 baadaye, Aziz Ki aliipatia Yanga, bao la pili kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na refa Ahmed Arajiga katika kile alichoamini Prince Dube alifanyiwa faulo ndani ya eneo la hatari na kipa wa Dodoma Jiji, Mohamed Hussein.

Hata hivyo, picha za marudio ya luninga zinaonyesha kuwa kipa huyo ambaye alionyeshwa kadi ya njano kwa tukio hilo, hakumgusa Dube.

Dakika ya 37, Mzize aliipatia Yanga bao la tatu ambalo lilidumu hadi muda wa mapumziko akiunganisha kwa mguu wa kulia pasi ya Mudathir Yahaya ambaye alinasa mpira uliiokolewa vibaya na kipa Hussein wa Dodoma Jiji.

Hakukuwa na utofauti mkubwa katika kipindi cha pili kwani Yanga iliendelea kutawala mchezo ikipiga pasi nyingi na kutengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao, juhudi ambazo zilizaa matunda katika dakika ya 62 walipopata bao la nne na la mwisho kupitia kwa Prince Dube ambaye aliunganisha vyema kwa mguu wa kulia pasi ya Mudathir ambaye kwa mara nyingine alinasa mpira uliiokolewa na kipa Hussein.

Bao hilo lilimfanya Dube afikishe idadi ya mabao saba aliyohusika nayo katika mechi nne zilizopita za Yanga katika mashindano tofauti akifunga sita na kupiga pasi moja ya mwisho.

Katika mechi ya jana, Yanga ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Mzize, Dickson Job, Khalid Aucho na Aziz Ki ambao nafasi zao zilichukuliwa na Farid Musa, Duke Abuya, Bakari Mwamnyeto na Salum Abubakar.

Dodoma Jiji iliwatoa Zidane Seleli, Paul Peter, Iddi Kipagwile na Daud Milandu ambao nafasi zao zilichukuliwa na Paul Obata, Yassin Mgaza, Ibrahim Ajibu na Lulihoshi Heritier.

Kupoteza mchezo wa leo, kumeifanya Dodoma Jiji ibaki katika nafasi yake ya 12 kwenye msimamo wa ligi na pointi zake 16.