Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yaukataa unyonge kwa Yanga

Muktasari:

  • Simba wametamba kuwa hawako tayari kuendeleza unyonge dhidi ya Yanga katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Fadlu Davids na nahodha wake Mohammed Hussein wametamba kuwa hawako tayari kuendeleza unyonge dhidi ya Yanga wakati timu hizo zitakapokutana kwenye mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mchezo huo utaanza saa 1:00 usiku ukitanguliwa na mchezo wa Azam na Coastal Union utakaochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni.

Simba ilipoteza mechi mbili mfululizo zilizopita dhidi ya Yanga ambazo zote ilikuwa kwenye Ligi Kuu ikifungwa mabao 5-1 katika mzunguko wa kwanza na ikipoteza kwa mabao 2-1 katika mzunguko wa pili.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa leo Agosti 7, 2024, Fadlu na Mohammed Hussein ‘Zimbwe’ wamesema kuwa hawako tayari kurudia makosa ya nyuma.

“Tunaichukulia mechi hii kama mechi nyingine. Tunajua kwamba Yanga ina miaka mitatu na kocha wao ana mwaka mmoja katika projekti yao na sisi tuna wiki nne hii ni mechi ambayo itatuonyesha tupo wapi.

“Sio rahisi kuwaingiza wachezaji 14 kwenye timu kwa wakati mmoja. Vipaji vingi na kuviweka pamoja. Ni mechi ambayo tunahitaji kushinda. Nina uzoefu wa mechi za ‘derby’ (watani wa jadi). Hii bila shaka ni moja ya mechi kubwa za watani wa jadi ndani ya Afrika.

Fadlu amesema Yanga sio tu wana wachezaji wazuri lakini pia wana kocha aliyeshiba mbinu huku akisisitiza umakini katika mchezo huo.

“Yanga ni timu iliyonolewa vizuri. Sio tu wana wachezaji wazuri lakini wana kocha aliyeshiba mbinu na katika mechi zao za maandalizi walikuwa na mbinu tofauti za kukabiliana na wapinzani tofauti. Tutakuwa makini na ubora wao.

“Kama tutakuwa na balansi nzuri nina uhakika tutafunga mabao na kupata ushindi,” amesema Davids.

Beki na nahodha wa Simba, Zimbwe amesema kuwa hawana hofu na mechi hiyo dhidi ya Yanga.

 “Wachezaji wapya nafikiri hawatambui ukubwa wa mechi lakini sisi wachezaji tuliokuwepo tunatambua ukubwa wa mechi kwa hiyo kuelekea katika mechi hiyo tunaamini kwa yale ambayo tumewaeleza wenzetu wataingia katika mfumo wetu kujua kwamba ni mechi kubwa na ni muhimu sana katika nchi yetu.

“Sio mara ya kwanza kucheza na watani zetu na ukizingatia msimu uliopita hatukuwa na matokeo mazuri dhidi yao. Kuwa hiyo tuna mwalimu mpya nafikiri mbinu zake ndio zitatufanya katika mchezo wa kesho zitatusaidia kupata matokeo mazuri,” amesema Zimbwe.

Msimu uliopita Simba ilitwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga katika fainali kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya dakika 90 za mchezo huo kumalizika kwa suluhu.