Ngao ya Jamii msimu huu tusubiri kuona ubabe wa Simba, Yanga

Muktasari:
- Zikimalizika mechi za nusu fainali, Agosti 11 ni kusaka mshindi wa tatu sambamba na fainali ya kumtafuta bingwa ambaye atakabidhiwa taji linaloshikiliwa na Simba waliolibeba msimu uliopita baada ya kuichapa Yanga kwa penalti 3-1 pale Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Agosti 8, 2024 ni ufunguzi wa msimu wa soka 2024-2025 hapa nchini ambapo zinachezwa mechi za Ngao ya Jamii kuanzia hatua ya nusu fainali, kisha mshindi wa tatu ikifuatiwa na fainali. Ni ubabe tu unasubiriwa kuonekana katika mechi hizo za maamuzi.
Ngao ya Jamii ya sasa ni kama ilivyokuwa msimu uliopita inashirikisha timu nne zilizomaliza nafasi nne za juu katika ligi. Mfumo wake ni kwamba nusu fainali ya kwanza ni kati ya timu iliyomaliza nafasi ya pili (Azam) dhidi ya nne (Coastal Union), kisha ile ya pili ni bingwa (Yanga) dhidi ya aliyeshika nafasi ya tatu (Simba).
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) wamepanga mechi hizo kuchezwa siku moja. Azam dhidi ya Coastal Union itaanza saa 10 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, Zanzibar, kisha Yanga dhidi ya Simba itapigwa saa 1 usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Zikimalizika mechi za nusu fainali, Agosti 11 ni kusaka mshindi wa tatu sambamba na fainali ya kumtafuta bingwa ambaye atakabidhiwa taji linaloshikiliwa na Simba waliolibeba msimu uliopita baada ya kuichapa Yanga kwa penalti 3-1 pale Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Rekodi zinaonyesha kwamba, tangu mwaka 2001 ambapo zilianza kuchezwa mechi za Ngao ya Jamii, Simba inaongoza kubeba taji hilo mara nyingi ambazo ni 10, inafuatia na Yanga ikichukua mara saba, kisha Mtibwa Sugar na Azam zilizochukua mara moja. Mbali na hapo, hakuna timu nyingine iliyowahi kushinda Ngao ya Jamii.
Kuelekea mechi hizo za nusu fainali ya Ngao ya Jamii, hapa kuna uchambuzi wake na rekodi kadhaa zilizowekwa huko nyuma na kinachotarajiwa kutokea mwaka huu.
Yanga vs Simba
Mpaka sasa zimechezwa fainali 19 za Ngao ya Jamii kuanzia 2001, huku ikionyesha mwaka 2004, 2006, 2007 na 2008 haikuchezwa, ikaendelea 2009 hadi sasa.
Mara ya kwanza zinaanza kuchezwa mechi hizo, Yanga iliichapa Simba mabao 2-1, wafungaji wa Yanga ni Edibily Lunyamila na Ally Yusuph 'Tigana' huku la Simba likifungwa na Steven Mapunda 'Garincha'. Mara ya mwisho mwaka jana Simba iliifunga Yanga 3-1 kwa penalti baada ya dakika tisini matokeo kuwa 0-0.
Simba na Yanga katika Ngao ya Jamii zimekutana mara tisa huku rekodi zikionyesha Simba imeshinda mechi tano na Yanga ikishinda nne.
Yanga inakumbuka misimu mitatu nyuma iliifunga Simba mara mbili mfululizo 2021 na 2022 kabla ya Simba kulipa kisasi mwaka 2023.
Mchezo huu wa Simba dhidi ya Yanga utakuwa ni wa nne mfululizo tangu 2021, hivyo ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa ikizingatiwa kwamba katika Kipindi hicho Yanga imeshinda mbili na Simba moja, safari hii Simba itataka kushinda ili kuweka mzani sawa kwenye mambo mawili.
Kwanza kubeba taji lao la 11 la Ngao ya Jamii na kuikimbia zaidi Yanga, kisha kushinda ili nayo iwe imeshinda mara mbili katika nne walizokutana hivi karibuni ndani ya michuano hiyo.
Yanga yenyewe inataka kuendeleza ubabe mbele ya Simba kwani tangu mara ya mwisho ipoteze katika Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao hao, wakaja kushinda mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara 2023-2024 tena kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-2. Ile ya kwanza ilikuwa Simba 1-5 Yanga kisha Yanga 2-1 Simba.
Ukiangalia vikosi vya timu zote mbili vina mabadiliko ya wachezaji, lakini Simba ndiyo ina maingizo mapya mengi ambayo yamefika 14, wakati Yanga wachezaji wapya ni saba.
Majembe mapya ya Simba yanayotarajiwa kuibeba timu hiyo raia wa kigeni nane ambao ni Valentin Nouma, Chamou Karabou, Charles Ahoua, Debora Mavambo, Augustine Okejepha, Joshua Mutale, Steven Mukwala na Moussa Camara.
Wazawa ni Kelvin Kijiri, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Awesu Awesu, Omary Omary na Valentino Mashaka. Lameck Lawi alikuwa wa kwanza kutambulishwa lakini usajili wake umezua utata, hata hivyo hayupo kambini ametimkia Ulaya.
Wachezaji saba wapya wa Yanga ni Khomeny Abubakari, Chedrack Boka, Clatous Chama, Aziz Andabwile, Duke Abuya, Prince Dube na Jean Baleke. Wazawa wawili pekee kwenye listi hiyo Khomeny na Andabwile.
Usajili wa pande mbili kwa timu hizo ndiyo unaufanya mchezo huu kusubiriwa kwa hamu kwani Simba inaamini imeimarisha kikosi chao wakati Yanga ikitamba imefanya maboresho kidogo tu yanayoweza kuwapa tena furaha.
Simba na Yanga mwaka huu kwao itakuwa ni mara ya 15 kushiriki Ngao ya Jamii. Simba ikiwa imeshinda Ngao ya Jamii 10, imepoteza nne, wakati Yanga imeshinda saba na kupoteza saba.
Wakati ratiba inapangwa na kuonyesha Yanga itacheza dhidi ya Simba, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema Ngao ya Jamii kwake si kipaumbele sana kulinganisha na michuano mingine hivyo anaitumikia kama sehemu ya maandalizi.
“Kwangu mimi mashindano ya Ngao ya Jamii sio muhimu, hapa Tanzania muhimu ni Ligi Kuu, katika Ligi unaonyesha ubora wako kwani tunacheza mechi 30, lakini katika vikombe unaweza kuwa na siku mbaya ukatolewa kwa sababu ni mechi za mtoano,” alisema Gamondi na kuongeza.
"Tunataka kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya kimataifa, tunataka kujaribu kufika mbali zaidi kwenye mashindano ya CAF zaidi ya msimu uliopita."
Huu utakuwa ni mtihani wa kwanza kwa Kocha Fadlu Davids ambaye anainoa Simba akichukua mikoba ya Abdelhak Benchikha.
Mwenzake Gamondi wakati anaanza kuinoa Yanga msimu uliopita, alishindwa kutetea Ngao ya Jamii iliyobebwa na Simba, safari hii Fadlu ana kazi ya kulitetea taji hilo Simba ililobeba msimu uliopita.
Fadlu amesema: “Kucheza dhidi ya Yanga ni sehemu ya mchezo tu kama michezo mingine, ni mchezo mkubwa n anaamini utakuwa mzuri upande wetu na kuondoka na ushindi. Tunataka kuona tunaanza vizuri.”
Azam vs Coastal
Azam katika ushiriki wao ndani ya Ligi Kuu Bara tangu mwaka 2008, imecheza Ngao ya Jamii sita na kushinda moja pekee dhidi ya Yanga mwaka 2016.
Kabla ya kubeba taji hilo, Azam ilicheza Ngao ya Jamii nne mfululizo na kupoteza zote kisha ile ya tano ikashinda kibabe.
Mwaka huu inaingia uwanjani ikisaka Ngao ya Jamii ya pili ikipambana na Coastal Union ambao kwao ni mara ya kwanza kushiriki mechi hizi.
Coastal Union waliomaliza msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara nafasi ya nne, wapo miongoni mwa timu nne zitakazoiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa msimu wa 2024-2025 ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika sambamba na Simba.
Kucheza kwao Ngao ya Jamii ni sehemu ya maandalizi kuelekea mechi za kimataifa zinazotarajiwa kuanza siku chache baada ya kumalizika Ngao ya Jamii.
Kati ya timu nne zinazoshiriki Ngao ya Jamii mwaka huu, Coastal Union inaonekana ndiyo timu isiyopewa nafasi kubwa zaidi kutokana na kwamba wanashiriki mara ya kwanza.
Hiyo ni kama ilivyokuwa mwaka jana walipocheza Singida Fountain Gate na kupoteza mechi zote mbili, nusu fainali na ile ya kusaka mshindi wa tatu iliyobebwa na Azam.
Majembe mapya ya Coastal Union ni Athuman Hassan Msekeni, Haroub Mohamed, Mukrim Issa, Ramadhan Mwenda, Abdallah Hassan na Anguti Luis.
Timu hiyo itaendelea kuwa chini ya Kocha David Ouma, huku golini wanaye Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara 2023-2024, Ley Matampi, katika maandalizi yao imeweka kambi kisiwani Pemba.
Azam iliweka kambi Unguja, kisha ikatimkia Morocco, wikiendi ilikuwa Rwanda kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon Sports.
Maingizo mapya ya Azam ni Mamadou Samake, Cheickna Diakite, Nassor Saadun, Adam Adam, Jhonier Blanco, Ever Meza, Franck Tiesse, Yoro Mamadou Diaby, kisha ikampa mkataba kipa Mohamed Mustafa ambaye awali alicheza hapo kwa mkopo.
MATOKEO NGAO YA JAMII
2001 Yanga 2-1 Simba
2002 Simba 4-1 Yanga
2003 Simba 1-0 Mtibwa
2004 HAIKUFANYIKA
2005 Simba 2-0 Yanga
2006-2008 HAIKUFANYIKA
2009 Mtibwa 1-0 Yanga
2010 Yanga 0-0 Simba (penalti 3-1)
2011 Simba 2-0 Yanga
2012 Simba 3-2 Azam
2013 Yanga 1-0 Azam
2014 Yanga 3-0 Azam
2015 Yanga 0-0 Azam (penalti 8-7)
2016 Azam 2-2 Yanga (penalti 4-1)
2017 Simba 0-0 Yanga (penalti 5-4)
2018 Simba 2-1 Mtibwa
2019 Simba 4-2 Azam
2020 Simba 2-0 Namungo
2021 Yanga 1-0 Simba
2022 Yanga 2-1 Simba
2023 Simba 0-0 Yanga (penalti 3-1)
Mabingwa wa Ngao Jamii hadi sasa:
Simba 10
Yanga 7
Azam 1
Mtibwa 1