Simba yatangulia robo fainali FA

Muktasari:
- Mechi hiyo ni kipimo kizuri kwa Simba iliyoondoka leo kwenda Misri kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, utakaochezwa Jumatano ijayo ya Aprili 2, kwenye Uwanja wa New Suez Canal.
Dar es Salaam: Timu ya Simba imetangulia hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya jana kuichapa Bigman FC inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mabao 2-1, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge.
Mabao ya Simba yalifungwa na Joshua Mutale dakika ya 15, akipokea pasi ya Valentin Nouma, huku Leonel Ateba akifunga la pili dakika ya 31 kwa penalti baada ya beki wa Bigman FC, Aboubakar Ally kumfanyia madhambi, Elie Mpanzu katika eneo la hatari.
Hata hivyo, wakati mchezo huo ukielekea mapumziko, Bigman FC ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 45, baada ya nyota wa timu hiyo, Joseph Henock kupiga shuti kali nje ya eneo la 18 na kumshinda kipa wa Simba, Hussein Abel.
Mechi hiyo ni kipimo kizuri kwa Simba iliyoondoka leo kwenda Misri kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, utakaochezwa Jumatano ijayo ya Aprili 2, kwenye Uwanja wa New Suez Canal.
Bigman FC yenye makazi yake Lindi, inashika nafasi ya saba na pointi 41, katika Ligi ya Championship baada ya kucheza michezo 24, ikishinda 11, sare minane na kupoteza mitano, ikipambana kuisaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Simba ilianza michuano hii hatua ya 64, baada ya kuitoa Kilimanjaro Wonders ya Kilimanjaro kwa mabao 6-0, kisha hatua ya 32, ikakutana na TMA FC ya Arusha na kuitupa nje pia kwa kuichapa 3-0, mechi zote ikicheza Uwanja wa KMC Complex Mwenge.
Kwa upande wa Bigman FC ilianza kampeni zake hatua ya 64, kwa kuitoa Soccer City ya Dar es Salaam kwa penalti 3-2, baada ya sare ya bao 1-1, kwenye dakika 90, kisha ikaitoa Tanzania Prisons kwa penalti pia 3-2, kufuatia sare ya kufungana 1-1.
Simba inakuwa timu ya tano kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya Singida Black Stars iliyoitoa KMC FC kwa bao 1-0, ikafuatiwa na Mbeya City iliyoichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1, huku JKT Tanzania ikiitandika Mbeya Kwanza 3-0.
Nyingine iliyofuzu hatua ya robo fainali ni Stand United 'Chama la Wana' iliyoichapa Mabingwa wa Mkoa wa Katavi, Giraffe Academy mabao 3-1, hivyo kuzifanya timu za Ligi Kuu kufuzu tatu, huku zile za Championship zikiwa ni mbili tu hadi sasa.
Ratiba ya michuano hiyo itaendelea tena leo Ijumaa kwa mchezo mmoja kupigwa ambapo Tabora United itakuwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora kuikaribisha Kagera Sugar, huku miwili ya kuhitimisha hatua hiyo ikipigwa kesho Jumamosi.
Yanga itaikaribisha Songea United huku Mashujaa FC ikicheza na Pamba Jiji, mechi ikipigwa Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma.