Simba yapigwa Kwa Mkapa
Muktasari:
- Azam imeanza vibaya hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kufungwa mabao 2-0 na AS Maniema Union, katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Stade des Martyrs, huko jijini Kinshasa DR Congo.
Simba imefikisha mechi nne mfululizo bila kushinda kwenye uwanja wa nyumbani baada ya jana kuchapwa bao 1-0 na Petro de Luanda ya Angola kwenye mchezo wa kwanza wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wakati Simba ikichapwa nyumbani, Azam ikiwa ugenini nayo ililala kwa mabao 2-0 dhidi ya AS Maniema kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya makundi.
Hii ina maana kuwa sasa ni timu moja tu ya Tanzania Yanga ambayo imefanikiwa kushinda mchezo wa hatua ya makundi baada ya Singida BS nayo kupoteza juzi kwa kulala kwa mabao 2-0 dhidi ya CR Beloazidad ya Algeria.
Simba ikiwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam ilionyesha kiwango cha chini huku kocha wa timu hiyo Dimitar Pantev akianza na kikosi ambacho hakikuwa na mshambuliaji hata mmoja.
Timu hiyo ambayo ilicheza bila kuwa na muunganiko mzuri na wachezaji wakionekana wamechoka ilimaliza kipindi cha kwanza kwa suluhu huku sehemu kubwa ya mchezo huo ikitawaliwa na Pedro.
Simba ilipoteza nafasi mbili za wazi kwenye mchezo huo, moja ikiwa ni ya Morrice Abraham ambayo aliipata kipindi cha kwanza akiwa amebaki la lango alipiga mpira ambao uligonga mwamba na kutoka nje.
Lakini nyingine aliipata Ellie Mpanzu kipindi cha pili cha mchezo huo ambapo alimpiga kipa chenga na kupiga mpira nje ya lango.
Wageni hao ambao walipiga mashuti mawili yaliyolenga lango walifanikiwa kujipatia bao la pekee kupitia kwa Jonathan Toro ambaye alipiga shuti kali dakika ya 78 ya mchezo likambabatiza beki wa Simba Rushine de Reuck na kujaa wavuni.
Baada ya bao hilo, Simba ililiendelea kucheza bila maelewano mazuri huku wachezaji wake wakipoteza mipira mingi pamoja na sapoti kubwa waliyokuwa wakiipata kutoka kwa mashabiki bado walishindwa kuonyesha makali.
Katika mchezo huo Simba walipiga pasi zilizofika 326 huku wapinzani wao wakipiga pasi 239. Sasa Pedro inaongoza msimamo wa Kundi D ikiwa na pointi tatu ikiwa ndiyo timu pekee iliyoshinda kwenye kundi hilo baada ya Esperance de Tunis na Stade Mallien kutoka suluhu juzi.
Azam Hoi
Azam imeanza vibaya hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kufungwa mabao 2-0 na AS Maniema Union, katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Stade des Martyrs, huko jijini Kinshasa DR Congo.
Katika mechi hiyo ya kwanza, wenyeji walifunga kupitia kwa Christian Panzi, huku la pili likifungwa na Clement Pitroipa.