Simba, Yanga kumaliza ubishi Aprili 20

WAKATI mijadala ya kung'olewa kwa Simba na Yanga kung'oka katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa bdo haijapoa, huku mashabiki wa timu hizo wakikejeliana, Bodi ya Ligi (TPLB) imekata mzizi wa fitina kwa kuitangaza mechi ya marudiano kwa timu hizo hadharani na sasa itapigwa Aprili 20.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara awali ilikuwa ikuionyesha ilikuwa inasikilizia matokeo ya timu hizo katika michuano ya CAF, lakini kutolewa kwao zikiwa ugenini zimetoa nafasi kwa Bodi kutangaza tarehe mpya ya kumaliza ubishi kwa timu hizo kuvaana Kwa Mkapa zikiwa katika vita ya ubingwa wa msimu huu.
Mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana, Yanga iliishindilia Simba mabao 5-1 na kusababisha aliyekuwa kocha wa Wekundu, Roberto Oliveira 'Robertinho' kufutwa kazi na kuanza mchakato uliomleta Abdelhak Benchikha ambaye atakutana na Yanga kwa mara ya kwanza.
Bodi katika tarifa iliyoitoa mchana huu wa Jumapili (Aprili 7) imesema tayari Simba na Yanga pamoja na wadau wengine wa Ligi Kuu wamepatiwa taarifa zote kuhusiana na mchezo huo na maandalizi yanaanza mara moja ili kuhakikisha unafanyika katika kiwango cha juu kinachoendana na hadhi ya michezo mikubwa ya Ligi ya Sita kwa Ubora barani Afrika.
Katika mchezo huo, Yanga ndio itakuwa mwenyeji baada ya Simba kuhodhi mechi ya duru ya kwanza na kuchapwa 5-1 kwa mabao ya Pacome, Zouzoua, Stephane Aziz Ki, Kennedy Musonda na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili huku lile la kufutia machozi kwa Simba likiwekwa nyavuni na Kibu Denis.
APRIL YA SIMBA
Tangu mwaka 2010, rekodi zinaonesha timu hizo mbili zimekutana mara nne katika mwezi huo wa Aprili, huku Simba ikionekana kuwa wababe zaidi ya watani wao.
Katika mechi hizo nne Simba imeshinda mbili na kutoa sare mbili huku Yanga ikiwa haijashinda mechi hata moja.
Mchezo wa kwanza ulipigwa April 19, 2014 na kuisha kwa sare ya mabao 1-1 ambapo Simba ilianza ilitangulia kufunga bao kupitia Haruna Chanongo dakika ya 75 na Yanga kuchomoa dakika ya 86 kupita kwa Simon Msuva wachezaji ambao kwa sasa hawapo na timu hizo.
Gemu nyingine ilikuwa msimu wa 2017/2018 ikapigwa April 29, 2018 na Simba kushinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Erasto Nyoni kwa kichwa dakika ya 37 na mechi kuisha hivyo.
Mechi nyingine iliyowakutanisha wakali hao wa Dar es Salaam ilikuwa April 30, 2022 na kumalizika kwa suluhu wakati huo kocha wa Yanga alikuwa Cedric Kaze, huku Simba ikiwa chini ya Pablo Franco na .
mchezo wa mwisho ulipigwa April 16, 2023 na Simba kushinda 2-0, bao la kwanza lilifungwa na beki Henock Inonga kwa kichwa dakika ya kwanza tu kabla ya Kibu Denis kushindilia msumari wa pili dakika 32 na nyota wote hao bado wapo Msimbazi.
Hata hivyo, mechi hiyo haitakuwa kinyonge kwani kutokana na rekodi za timu hizo hivi karibuni kwani mechi tano za mwisho walipokutana, Simba ilishinda mbili, Yanga ikashinda moja na mbili kumalizika kwa sare.
Simba na Yanga zote kwa sasa zipo katika mbio za ubingwa Yanga ikiongoza ligi na alama 52 baada ya mechi 20 huku Simba ikiwa nafasi ya tatu na alama 45 ilizovuna baada ya michezo 19 huku nafasi ya pili ikishikwa na Azam yenye pointi 47 baada ya mechi 21.
Mechi za Aprili
19.4.2014 Yanga 1-1 Simba
29.4.2018 Simba 1-0 Yanga
30.4.2022 Yanga 0-0 Simba
16.4.2023 Simba 2-0 Yanga