Simba yaichakaza Kagera Sugar ikirejea kileleni Ligi Kuu

Muktasari:
- Simba imeshinda mechi zote sita za ugenini kwenye Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Azam FC, Dodoma Jiji, Tanzania Prisons, Mashujaa FC, Pamba Jiji na Kagera Sugar, ikifunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.
Steven Mukwala na Ladack Chasambi wamekuwa mwiba kwa Kagera Sugar leo baada ya kuiongoza Simba kuibuka na ushindi wa mabao 5-2 kwenye mechi baina yao iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Mukwala alifunga mabao mawili kati ya hayo matano huku Chasambi akipiga pasi tatu za mwisho kwenye mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Tatu Malogo.
Aliyefungua karamu ya mabao kwa Simba jana alikuwa ni beki Shomari Kapombe katika dakika ya 13 ambaye aliunganisha kwa mguu wa kulia mpira wa krosi kutoka kwa Mohamed Hussein na baadaye yakafuata mabao yaliyofungwa na Charles Ahoua, Fabrice Ngoma na Steven Mukwala aliyepachika mawili.
Bao la Ahoua lilitokana na mkwaju wa faulo iliyokwenda langoni mwa Kagera Sugar moja kwa moja baada ya nyota huyo wa Ivory Coast kufanyiwa faulo na Abdallah Mfuko nje kidogo ya eneo la hatari na baadaye Ngoma alifunga la tatu kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na Ladack Chasambi.
Mukwala alihitimisha ushindi huo mnono wa Simba kwa kufunga mabao mawili yote akimalizia pasi za Ladack Chasambi na mabao mawili ya Kagera Sugar yalipachikwa na Datius Peter aliyemalizia pasi ya Abdallah Mfuko na lingine la Cleophace Mkandala aliyeunganisha kwa shuti pasi ya Tariq Kilakala.
Huo ni ushindi wa kwanza mkubwa kwa Simba kuupata dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba huku pia wakishinda kwa mara ya kwanza dhidi ya wapinzani hao kwenye Uanja huo baada ya kucheza hapo mara tatu mfululizo bila kupata ushindi.
Katika mchezo huo Simba ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Fabrice Ngoma, Elie Mpanzu, Debora, Kapombe, Awesu ambao nafasi zao zilichukuliwa na Yusuph Kagoma, Mzamiru Yassin, Kelvin Kijili, Chasambi na Joshua Mutale.
Kagera Sugar iliwatoa Peter Lwasa, Kassim Feka, Salehe Seif na Jofrey Manyasi ambao nafasi zao zilichukuliwa na Tariq Seif, Samuel Onditi, Cleophace Mkandala na Joseph Mahundi.
Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 34 na kuongoza msimamo wa ligi huku ikiishusha Azam FC yenye pointi 33.
Kagera Sugar imeshuka hadi nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikibaki na pointi zake 11.