Simba ilivyoungana na Yanga kupigania Uhuru

Muktasari:
- Young Africans, ikiwa tawi la Tanu kupitia umoja wa vijana tangu zama za African Association mwaka 1926, ilitumika kama moja ya silaha za mapambano ya kutafuta uhuru.
Mchezo wa mpira wa miguu uliingia nchini baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, pale Waingereza walipotawala wakichukua nafasi ya Wajerumani.
Wakaanzisha timu zao katika mitaa waliyokuwa wakiishi kama sehemu ya kujifurahisha.
Mwaka 1921 wakaanzisha mashindano ya soka yaliyoitwa Ligi ya Dar es Salaam, iliyokuwa na timu sita pekee.
Timu hizo zilikuwa 6th Battalion KAR ( timu ya jeshi la kikoloni), Gymkhana Club iliyokuwa ya Wazungu na uwanja walioutimia ukiwa Gymkhana, Tanganyika Territorial Police ( timu ya Jeshi la Polisi), Tanganyika Railways ( timu ya Mamlaka ya Reli) Government School ( timu ya shule ambayo sasa ni Shule ya Uhuru) na Government Services ( timu ya ofisi ya utumishi).
Timu zote hizo zilikuwa za Wazungu na ama zilimilikiwa moja kwa moja na idara na taasisi za serikali, au watu binafsi wanaofanya kazi serikalini kama Gymkhana.
Kuanzia miaka ya 1930 timu za kutoka uraiani zikaanza kushiriki, japo nyingi ziliundwa na raia wa kigeni zaidi Wazungu.
Ikaanzishwa timu iliyoitwa New Strong, maskani yake yakiwa New Street, mtaa ambao sasa ni Lumumba. Baba yake mzee Idd Mshangama wa TFF aliichezea timu hii. Timu iliundwa na raia mchanganyiko, Waarabu na Waafrika wazawa.

Pia kulikuwa na timu kama Arab Sports ya Kariakoo, timu ya Waarabu. Sudanese Team- timu ya raia wa Sudan. Khalsas - timu ya Wahindi wa jamii ya Sikh (Singasinga).
Mwaka 1935, ikaanzishwa timu ya wazawa watupu iliyoitwa New Young. Timu hiyo iliundwa na watu walioleta vuguvugu la kisiasa la African Association (AA) lililoanza mwaka 1926. Vuguvugu hilo lilikuwa na harakati za kupigania haki za Waafrika kutoka serikali ya kikoloni.
Wakati huo serikali ya kikoloni iliwaruhusu watu wote kwa jamii zao kuwa na vuguvugu la aina hiyo. Kulikuwa na European Association, Indian Association, Arab Association na kadhalika.
Kwa hiyo mwaka 1926, Waafrika nao wakaunda vuguvugu lao. Kwa kuwa wao walikuwa wengi, wakaanzisha na timu ili ishiriki Ligi ya Dar es Salaam na ndio hiyo New Young. Wakati huo ligi ilikuwa na madaraja mawili tu, la kwanza na la pili.
New Young ikashiriki daraja la pili mwaka1935 na kupanda kwa kishindo. Mwaka 1936 ikashiriki daraja la kwanza na kuwakuta wakubwa waliotangulia, wakiwamo New Strong waliokuwa na Waswahili wengi, wakatengeneza utani wa jadi.
Bahati mbaya mwaka huohuo, New Young ikashuka daraja, kurudi la pili. Baadhi ya mashabiki wao walikerwa na uongozi wakisema ulishindwa kuisimamia timu.
Wakajitenga na kuanzisha timu mpya. Timu hiyo ilianza kwa jina la Stanley SC kwa sababu iliasisiwa katika Mtaa wa Stanley ambao sasa ni Aggrey.
Baadaye ikabadili jina na kujiita Queens SC na baadaye Knight Eagles. Mwaka 1936 timu ya Sunderland ya England ilishinda ubingwa wa ligi ya nchi hiyo na kupata umaarufu.
Knight Eagles ikaamua kuchukua jina la Sunderland na kuanzia hapo ikawa Sunderland SC.
Wale waliobaki New Young nao wakabadili jina na kujiita Young Africans, ndiyo hawa Yanga ya leo. Ligi iliendelea na New Young na Sunderland kama timu za wazawa kwa asilimia 100 zilipata wakati mgumu kwenye mashindano.
Zikapanga kuanzisha ligi nyingine ndogo ya wazawa watupu, ili waitumie kama sehemu ya maandalizi ya ligi kubwa ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, serikali ya kikoloni ilikataa wazo hilo ikihofu kuwa wazawa wakianzisha ligi ya peke yao, itakuwa kubwa na kuvutia wengi kwa sababu wako wengi na ile ligi rasmi ya Dar es Salaam ingekosa msisimko.
Lakini wazawa walishikilia msimamo wao na serikali iliendelea kuupinga. Serikali ikamtuma Liwali wa Dar es Salaam aliyeitwa Mokhsin, kuhakikisha ligi hiyo inakwama.
Liwali Mokhsin, aliyekuwa Mwarabu, ‘akawatongoza’ Sunderland waliokuwa na uchumi mdogo, ili waungane na Arab Sports wawe na nguvu.
Sunderland wakakubali na kuungana na huo ndio mwanzo wa uhusiano wa Waarabu na Simba.
Lengo la Mokhsin lilikuwa kuwagawanya wazawa, ili wasiendelee na wazo la kuanzisha ligi yao, akawa amefanikiwa, kwani Young Africans wakabaki peke yao, wakakosa nguvu ya hoja.
Mwaka 1939 ikazuka Vita Kuu vya Pili vya Dunia na taasisi nyingi zilifunga ofisi zake na raia wengi wa kigeni walirudi makwao.
Hapo ndipo timu zote kubwa zilipokufa kabisa au kuishiwa nguvu na kuzorota. Young Africans na Sunderland pekee ndizo zilizobaki kama timu kubwa.
Hapo ndipo upinzani wa jadi ukahama kutoka kwa Young Africans na New Strong ambayo ilikufa na kuhamia kwa Sunderland. Ule usaliti wa kuungana na Waarabu pamoja na vita vya kuwania mataji, vikaongeza upinzani.

Baada ya Vita Kuu vya Pili vya Dunia, vuguvugu la AA likabadilika na kuwa Tanganyika African Association (TAA), ikiwa na lengo la kuchukua muundo wa kisiasa na mwaka 1954, ikawa chama kamili cha siasa cha Tanu (Tanganyika Africans National Union).
Yanga, Simba na harakati za uhuru
Young Africans, ikiwa tawi la Tanu kupitia umoja wa vijana tangu zama za African Association mwaka 1926, ikaendelea kutumika kama moja ya silaha za mapambano kwa kuhamasishana kufanya mikutano ya ndani, kwa sababu mkoloni alipiga marufuku mikutano ya hadhara.
Watu wa Sunderland ambao kimsingi zamani na wao walikuwa Young Africans tangu zama za New Young, wakaungana na harakati hizo.
Hapo ndipo timu hizi mbili zilipotumika katika harakati za uhuru.
Kwa mfano, klabu iliitisha mkutano mkuu wa wanachama, kupitia huo mkutano wanachama wanahamasishwa kukata kadi za Tanu, viongozi wa chama hicho wanakuja kimyakimya kuhutubia.
Wazo la uhuru lilivutia wengi, hivyo wakajificha kwenye timu hizo, huku wakiendesha harakati za siasa.
Hali hiyo iliendelea hadi uhuru ulipopatikana mwaka 1961. Mwaka 1971, Sunderland ikabadili jina na kuwa Simba SC kwa ushauri wa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amaan Karume, siku ya uzinduzi wa jengo jipya la klabu hiyo la Mtaa wa Msimbazi.
Karume aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa jengo hilo, alisema: "Haipendezi timu za wazawa kutumia majina ya wageni, mnaweza kujiita hata Simba SC.” Wanachama walilipitisha jina hilo moja kwa moja hadi leo.
Sio Sunderland pekee waliobadilisha jina, bali timu kadhaa zilibadili majina.