Siku ya kilio, kicheko Kwa Mkapa, Amaan

Muktasari:
- Ni mchezo ambao pasipo shaka yoyote unabeba matumaini kwa kila timu kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa taji la kwanza ili iwe katika hali nzuri kisaikolojia kiwa ajili ya msimu mpya wa 2024/2025.
Tanzania leo inasimama kwa muda kupisha mechi kubwa ya watani wa jadi, Yanga na Simba ambao ni wa nusu fainali ya pili ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam baada ya nusu fainali nyingine itakayozikutanisha Azam na Coastal Union kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Ni mchezo ambao pasipo shaka yoyote unabeba matumaini kwa kila timu kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa taji la kwanza ili iwe katika hali nzuri kisaikolojia kiwa ajili ya msimu mpya wa 2024/2025.
Litakuwa ni taji la nne mfululizo kwa Yanga kulichukua ndani ya muda wa miezi mitatu baada ya kufanya hivyo katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la CRDB msimu uliopita na kisha kuchukua lile la Toyota huko Afrika Kusini, wiki mbili zilizopita.
Simba itakuwa ikisaka taji la pili mfululizo la ngao ya jamii baada ya kuchukua la msimu uliopita wakati mashindano hayo yalipofanyika Tanga.
Mechi hiyo ya leo itachezeshwa na refa wa kati Elly Sasii ambaye atasaidiwa na Mohammed Mkono, Kassim Mpanga na mwamuzi wa akiba akiwa ni Amina Kyando.
Sura mpya mtegoni
Nyota wapya waliosajiliwa na Yanga na Simba kwa mara ya kwanza wataonja joto la mechi ya watani wa jadi ama kwa kupata nafasi ya kucheza katika vikosi vyao au kukaa benchi na hata kutazama mechi wakiwa jukwaani.
Kwa Yanga, wachezaji wapya ni Abubakar Khomein, Prince Dube, Aziz Andabwile, Clatous Chama, Chadrack Boka, Jean Baleke na Duke Abuya.
Simba nyota wake wapya ni Augustine Okejepha, Debora Mavambo, Chamou Karabou, Valentine Nouma, Valentino Mashaka, Mousa Camara, Kelvin Kijiri, Charles Ahoua, Yusuph Kagoma, Awesu Awesu, Steven Mukwala, Joshua Mutale na Omary Omary.
Aziz na rekodi ya Tambwe, Kichuya
Ikiwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki atafunga bao katika mechi hiyo, ataifikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Shiza Kichuya na Amissi Tambwe ya kufunga bao katika mechi tatu mfululizo za watani wa jadi.
Aziz alifunga bao moja katika mechi ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Simba na kisha akafunga tena kwenye mechi waliyoshinda mabao 2-1, zote zikiwa za Ligi Kuu ya NBC.
Mabao yanukia
Takwimu bora za kufumania nyavu ambazo timu hizo zimekuwa nazo katika mechi zao za kujipima nguvu zilizocheza katika maandalizi ya msimu mpya, zinatoa ishara kuwa huenda mechi ya leo ikawa na mvua ya mabao ikiwa safu za ulinzi zitashindwa kujipanga vyema.
Katika mechi nne zilizopita, Yanga imefunga mabao nane ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa mchezo huku yenyewe ikiruhusu mabao matatu.
Simba katika mechi nne zilizopita, imefunga mabao tisa ikiwa ni wastani wa mabao 2.25 kwa mechi na yenyewe pia imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.
Makocha, wachezaji tambo kibao
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kuwa licha ya kutopata nafasi ya kuitazama vya kutosha Simba, haimpi presha kwa vile kikosi chake kina ubora wa hali ya juu.
“Hakuna siri kwenye mpira kila kitu lazima kiwe hadharani. Kesho ni siku muhimu sana kwani ni mechi ya mtoano. hatupaswi kufanya makosa tunapaswa kuwa makini kwenye kila idara ili kupata matokeo mazuri, naamini mashabiki wetu watajitokeza kwa wingi kwa lengo la kutupa hamasa.”
“Naheshimu sana wapinzani wote ninaokutana nao. Kesho ni mchezo wa dabi hakuna 'underdog' (timu isiyopewa nafasi) kwenye mchezo huo kwani ni mchezo maalumu sana. Najua mpinzani wetu ana timu mpya, wachezaji wapya, wote kwa pamoja watachukua fursa hii kuonesha ubora wao.
"Tupo imara kiakili na kimwili. Tumejianda vya kutosha hakuna tunachohofia. Sijapata wasaa mzuri wa kuwatazama wapinzani kwani mechi zake nyingi hazikuoneshwa, lakini hiyo sio changamoto kubwa kwani naanda timu yangu kwa asilimia 75, asilimia 25 ndio natumia kumchunguza mpinzani," amesema Gamondi.
Kipa wa Yanga, Abubakar Khomein amesema kwa upande wao wachezaji wapo tayari kwa mechi hiyo.
“Tumejiandaa vizuri sana na tuko tayari, wachezaji wana ari na wote tunawahakikishia kuwa wachezaji tunakwenda kupambana, naamini kesho tutafanya vizuri," amesema Khomein.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi ya leo.
“Tunaichukulia mechi hii kama mechi nyingine. Tunajua kwamba Yanga ina miaka mitatu na kocha wao ana mwaka mmoja katika projekti yao na sisi tuna wiki nne hii ni mechi ambayo itatuonyesha tupo wapi.
“Sio rahisi kuwaingiza wachezaji 14 kwenye timu kwa wakati mmoja. Vipaji vingi na kuviweka pamoja. Ni mechi ambayo tunahitaji kushinda. Nina uzoefu wa mechi za ‘derby’ (watani wa jadi). Hii bila shaka ni moja ya mechi kubwa za watani wa jadi ndani ya Afrika.
“Yanga ni timu iliyonolewa vizuri. Sio tu wana wachezaji wazuri lakini wana kocha aliyeshiba mbinu na katika mechi zao za maandalizi walikuwa na mbinu tofauti za kukabiliana na wapinzani tofauti. Tutakuwa makini na ubora wao. Kama tutakuwa na balansi nzuri nina uhakika tutafunga mabao na kupata ushindi,” amesema Davids.
Beki na nahodha wa Simba, Zimbwe amesema kuwa hawana hofu na mechi hiyo dhidi ya Yanga.
“Sio mara ya kwanza kucheza na watani zetu na ukizingatia msimu uliopita hatukuwa na matokeo mazuri dhidi yao. Kuwa hiyo tuna mwalimu mpya nafikiri mbinu zake ndio zitatufanya katika mchezo wa kesho zitatusaidia kupata matokeo mazuri,” amesema Zimbwe.
Katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Azam na Coastal Union zitaumana katika nusu fainali nyingine itakayoanza saa 10:00 jioni.
Kocha wa Coastal Union, David Ouma alisema kuwa wanafahamu watakutana na timu ngumu kwenye nusu fainali lakini watahakikisha wanafanya vizuri.
"Tunahitaji kufanya kila kitu kilichokuwa bora ili tupate matokeo mazuri. Azam ni timu nzuri yenye wachezaji wenye uwezo wa kuamua mechi hivyo kwetu ni kipimo kizuri pia kwa sababu tumepata michezo mingi ya kirafiki ambayo imetujengea hali ya kujiamini zaidi.
"Tofauti na Anguti (Luis) ambaye tutamfanyia tathmini ya mwisho kesho kabla ya mchezo, mwingine anayeweza kukosekana ni kipa, Ley Matampi ila waliobaki wote wako katika hali nzuri ya kiafya na utimamu wa kimwili na kiakili," alisema Ouma.
Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo ametoa tahadhari kwa wachezaji wake kuwa wasiidharau Coastal Unio.
"Tumecheza na Coastal Union mara tatu msimu uliopita na licha ya kupata matokeo mazuri lakini imekuwa timu inayotupa wakati mgumu sana kimbinu. Wachezaji wanahitaji kuonyesha jinsi gani wanauhitaji mchezo ili tupate kilichokuwa bora," amesema na kuongeza;
"Unapocheza hatua kama hizi maana yake kila mmoja anahitaji ubingwa na hata sisi pia kama Azam FC ndio kiu na shauku yetu kwa sababu tuna wachezaji bora wanaoweza kuipigania timu, tunaiendea mechi moja baada ya nyingine hivyo mawazo na akili zetu kwa sasa ni mchezo dhidi ya Coastal Union."
Timu hizo mara ya mwisho zilikutana Mei 18, mwaka huu ambapo Azam ilishinda mabao 3-0, katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la FA, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.