Serikali kujenga viwanja vya mazoezi Dar, Arusha, Zanzibar

Serikali imesema katika kuelekea michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2027) mbali na kujenga viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya mechi, pia imeweka mikakati ya kujenga viwanja vitano vya mazoezi vitakavyotumiwa na timu shiriki sambamba na waamuzi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Makete, Festo Sanga aliyetaka kufahamu mikakati ya Serikali ni ipi katika kujenga viwanja vingi vya mazoezi kuelekea michuano hiyo.

Naibu Waziri huyo amebainisha kwamba, viwanja hivyo vya mazoezi vitajengwa Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar sehemu ambayo michuano ya Afcon itachezwa mwaka 2027.

"Pamoja na kujenga viwanja ambavyo vitakuwa vinatumika kwa ajili ya mashindano katika majiji ya Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha, lakini miji yote mitatu hii itakuwa na viwanja vitano kwa ajili ya mazoezi, vinne kwa ajili ya timu zitakazokuwa zinashiriki kwa sababu kila kituo kitakuwa na timu nne na kimoja kitakuwa kwa ajili ya waamuzi kwa sababu na wao watatakiwa kufanya mazoezi.

"Pia tutafanya uboreshaji wa hoteli zetu kwa ajili ya kupokea ugeni mkubwa tunaoutarajia katika michuano ya AFCON 2027," alisema.

Mbali na hilo, Serikali imesema ujenzi wa viwanja vipya vya michezo kwa ajili ya michuano ya Afcon 2027 unatarajiwa kukamilika mwakani ili kupisha ukaguzi wa kikanuni, huku ukarabati wa viwanja vya Benjamin Mkapa, Uhuru na Amaan ukitarajiwa kukamilika mwaka huu.

Michuano hiyo ya Afcon 2027, inatarajiwa kuandaliwa na Tanzania, Kenya na Uganda ikiwa ni mara ya kwanza nchi hizo zinafanya hivyo.