Afcon 2027 yaipaisha bajeti ya michezo

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro

Dodoma. Hii ni bajeti ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano hiyo. Hivyo ndivyo unaweza kusema baada Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuongezewa fedha kutoka Sh35.4 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi Sh285.3 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, imewasilishwa bungeni na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro akiliomba Bunge liidhinishe Sh285.3 bilioni kutoka Sh35.4 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Fedha za miradi ya maendeleo zimeongezeka kwa asilimia 2,082 kutoka Sh11.8 bilioni hadi Sh258.2 bilioni.

Kuonyesha kuwa ni bajeti ya Afcon 2027 fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa soka wa Arusha ni Sh125.2 bilioni. Uwanja huo kwa ajili ya fainali za Afcon, utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000, unajumuisha miundombinu ya eneo la kukimbilia riadha, uwanja wa ndani (Indoor stadium), viwanja vya mpira wa mikono, pete na netiboli.

“Haya ni maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Afcon 2027 kama uwanja wa mashindano. Mkandarasi amepatikana na kazi ya ujenzi imeanza. Kiwanja hiki kinatarajiwa kuwa kimekamilika ifikapo Desemba 2025,” alisemwa Dk Ndumbaro kwenye hotuba yake.

Alisema pia, Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya CHAN yatakayofanyika nchini Septemba 2024.

“Mashindano haya ni ya maandalizi ya Afcon 2027. Mashindano haya ya Afcon yatachagiza kuwapo kwa fursa lukuki za ujenzi wa miundombinu, kujenga uchumi, kuvutia utalii, ajira na kuitangaza Tanzania kimataifa,”alisema.

Tanzania, Kenya na Uganda zitaandaa kwa pamoja fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) huko Cairo, Misri kutangaza kuwa ombi lao la pamoja limeshinda dhidi ya maombi ya Algeria, Misri na Botswana ambazo nazo ziliomba kuandaa fainali hizo.

“Mheshimiwa Spika, kupitia mafanikio ya kuwa wenyeji wa CHAN 2024 na Afcon 2027 tumeianza safari ya mafanikio ya kushiriki Kombe la Dunia 2030 kwa kuanza kujenga miundombinu na timu imara ya Taifa.

“Katika hili, timu imara ya Taifa itaandaliwa kwa kuwa na timu tatu za vijana chini ya miaka 17 (itakayotokana na UMISETA na UMITASHUMTA); chini ya miaka 20 na chini ya miaka 23, makocha wazoefu wataajiriwa na huduma za timu hizi zitasimamiwa kama programu maalumu ya Serikali,” alisema Dk Ndumbaro.

Kutumia wanamichezo wa Diaspora

Dk Ndumbaro alisema Tanzania tangu ipate Uhuru mwaka 1961, hatukuweza kuwatumia wanamichezo wa Diaspora kama ambavyo nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikinufaika na utaratibu wa kuwatumia wachezaji hao.

“Kwa mara ya kwanza katika historia katika hatua ya kufuzu Afcon ya 2023 tumefanikiwa kuwatumia wachezaji wa Kitanzania wanaoishi nchi nyingine ambao wana asili ya Tanzania (Diaspora). Wachezaji hao hakika wameleta tija na hamasa katika timu yetu ya Taifa Stars,” alisema Dk Ndumbaro.

Tanzania na Afcon

Tanzania imeshiriki michuano ya Afcon mara tatu, ambapo mwaka 1980, ilishiriki  michuano hiyo iliyofanyika Lagos, Nigeria.

Ambapo ilikuwa Kundi moja na Nigeria, Misri na Ivory Coast na kutolewa hatua ya makundi.

Nyingine ambayo Stars ilishiriki ni ya mwaka 2019, ambapo ilitolewa hatua ya makundi pia, ikiwa pamoja na Algeria, Senegal na Kenya, pia ikashiriki 2023 ikiwa kundi moja na Zambia, DR Congo na Morocco na sasa inatafuta nafasi ya kushiriki 2025 nchini Morocco kabla ya 2027 ambayo itakuwa mwenyeji.


Dabi ya kibiashara

Dabi ya Kariakoo ya watani wa jadi Simba na Yanga nayo imetinga bungeni baada ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupanga kuiendesha kibiashara.

Hayo yamesemwa bungeni na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro wakati anawasilisha bajeti ya wizara hiyo.

 Dabi hiyo ya watani wa Jadi, Simba na Yanga yenye historia tangu Juni 7, 1965, ndiyo mechi ambayo imekuwa ikiingiza mashabiki wengi kwa hapa nchini.

Yanga ndio timu kongwe zaidi Tanzania ilianzishwa mwaka 1935 wakati Simba ikianzishwa mwaka 1936, ikianza kwa kuitwa Sunderland.

Akizungumza bungeni Dk Ndumbaro, alisema moja ya kipaumbele cha wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 ni kuendesha kibiashara Ligi Kuu ya Tanzania na hususani michezo ya Dabi ‘Derby’ za watani wa jadi, Simba na Yanga ili kuhakikisha ligi inakuwa na thamani kubwa, timu zinatengeneza uchumi na zinafanikiwa katika mashindano ya kimataifa.

Pia, alisema vipaumbele vingine ni kufanya tamasha la utamaduni la kitaifa kuwa kubwa zaidi kwa kufanyika mikoa yote kwa kushirikiana na sekta binafsi, kwa ushindani, ambapo mkoa mshindi hufanya tamasha kwa mwaka unaofuata.

“Hii itaibua chachu ya kukuza na kulinda tamaduni zetu, kukuza sanaa mtaa kwa mtaa kupitia programu ya BASATA Vibes ili kufikia kila mtaa nchini kuibua, kuilea na kuipatia jukwaa la kutangaza na kuuza sanaa yetu, kuipeleka sanaa yetu kimataifa zaidi kwa  kuwaunganisha wasanii na masoko makubwa ya kimataifa ya sanaa,” alisema.