Saa ya Messi bei yake unaweza kununua kununua V8 tano
Muktasari:
- Mshindi huyo mara nane wa tuzo ya Ballon d’Or alikaa jukwaani pamoja na mtoto wake Thiago (12), akiwa amevalia shati jeupe lenye mvuto na kaptura ya beige akini kiliteka shoo kilikuwa ni saa yake ya ajabu ya Rolex Barbie.
Florida, Marekani. Staa wa Inter Miami na Argentina, Lionel Messi ameonekana akiwa amevaa saa ya kifahari ya rangi ya waridi aina ya Rolex Daytona “Barbie”, yenye thamani ya takribani Pauni 700,000 (zaidi ya Sh2.3 bilioni).
Kiasi hicho cha fedha kinaweza kununua magari ya kifahari aina ya Toyota Land Cruiser 300 matano ambayo bei yake ni kuanzia Sh 450 milioni na Sh 520 milioni.
Nyota huyo wa Inter Miami alionekana na saa hiyo ya bei ghali Jumamosi usiku wakati timu yake ikitoka suluhu dhidi ya FC Cincinnati.
Messi (38), hakuwa uwanjani kwani alikuwa anatumikia adhabu ya kufungiwa kucheza mechi moja.
Mshindi huyo mara nane wa tuzo ya Ballon d’Or alikaa jukwaani pamoja na mtoto wake Thiago (12), akiwa amevalia shati jeupe na kaptula ya beige lakini kiliteka shoo kilikuwa ni saa yake ya ajabu ya Rolex Barbie.
Saa hiyo ya kipekee imetengenezwa kwa madini ya pink sapphire yanayolingana na rangi ya jezi ya nyumbani ya Inter Miami, na pia ina dhahabu ya kiwango cha juu cha karati 18.
Ripoti zinaeleza kuwa ni saa 10 tu kama hiyo ndizo zimetengenezwa na Rolex na hazipatikani madukani, wala hazijawahi kutangazwa rasmi na kampuni hiyo.
Badala yake, Rolex inadaiwa kuwasiliana binafsi na wateja wao wa kipekee waliotathminiwa kuwa na kuzitengeneza kwa ajili yao.
Inaaminika kwamba watu mashuhuri wenye saa hizo wamelipia karibu Pauni 310,000 (takribani TSh 1 bilioni), lakini ikiwa mojawapo ya saa hizo itauzwa tena sokoni, thamani yake inaweza kufikia au kuzidi Pauni 700,000.
Mtu pekee aliyewahi kuonekana na saa hiyo kabla ya Messi ni muigizaji Mark Wahlberg.
Baada ya kushuhudia mechi ya Inter Miami kwenye Uwanja wa Chase mjini Fort Lauderdale, Messi na familia yake walienda kuhudhuria tamasha la Coldplay.
Aliandamana na mkewe mrembo Antonela Roccuzzo pamoja na watoto wao watatu.
Messi pia aliingia kwenye vichwa vya habari alipokuwa kwenye tamasha hilo baada ya yeye na Antonela kuonyeshwa kwenye skrini maalumu wakiwa wamekumbatiana.