Saa 5 za presha Ligi Kuu
Muktasari:
- Yanga inaingia katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kutopoteza mechi 24 mfululizo za Ligi Kuu ambapo imeshinda 22 na kutoka sare mbili tangu ilipofungwa na Tabora United (sasa TRA United) kwa mabao 3-1, Novemba 7, 2024.
Dar es Salaam. Ni saa tano zinazoweza kuwa tamu au chungu kwa vigogo vya soka nchini Yanga na Simba wakati zitakapokuwa na mechi muhimu za Ligi Kuu kwenye viwanja vyao vya nyumbani dhidi ya Fountain Gate na Mbeya City.
Kuvuna pointi tatu leo, kutafanya Yanga na Simba kila moja kupanda juu kwenye msimamo wa ligi na kujitengenezea mazingira mazuri katika mbili za ubingwa wa ligi msimu huu lakini kama mambo yakienda tofauti, kila moja itakuwa inapunguzwa kasi katika mbio za kulisaka taji.
Katika Uwanja wa KMC Complex, Yanga itakuwa nyumbani ikiikaribisha Fountain Gate katika mchezo ambao umepangwa kuanza saa 10:00 jioni.
Yanga inaingia katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kutopoteza mechi 24 mfululizo za Ligi Kuu ambapo imeshinda 22 na kutoka sare mbili tangu ilipofungwa na Tabora United (sasa TRA United) kwa mabao 3-1, Novemba 7, 2024.
Msimu huu, Yanga katika mechi nne ilizocheza za Ligi Kuu, Yanga imeibuka na ushindi mara tatu na kutoka sare moja, ikifunga mabao tisa na kuruhusu nyavu zake zitikiswe mara moja.
Fountain Gate wamekuwa na mwendo wa kusuasua ambapo katika mechi tisa walizocheza hadi sasa, wamepata ushindi mara tatu, kutoka sare moja huku wakipoteza mechi tano na wamefunga mabao manne tu huku wakifungwa mabao 10.
Yanga iliyo katika nafasi ya tano, ikipata ushindi leo itafikisha pointi 13 na kusogea hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na kama Fountain Gate iliyo nafasi ya sita ikipata ushindi leo, itafikisha pointi 13 na kusogea hadi nafasi ya nne.
Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema kuwa wamejipanga kwa ajili ya mchezo huo.
"Tunafahamu kuwa wapinzani wetu wamejiandaa vizuri pia. Tunahehsimu kila mpinzani anayekuja mbele yetu. Tutacheza kama vile tunacheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa. Falsafa yetu haitabadilika. Dhamira yetu ni ushindi tu,” alisema Goncalves.
Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mohammed Laizer alisema,"Tunawaheshimu Yanga ni timu nzuri lakini sisi tumekuja kushindana ili kupata matokeo,”
Baada ya mchezo huo, kuanzia saa 1:00 usiku, Simba itakuwa mwenyeji wa Mbeya City katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni Dar es Salaam.
Zinakutana timu mbili ambazo zinapitia hali inayofanana kwani zote zimetimua wakuu wao wa benchi la ufundi wiki hii.
Mbeya City ndio ilianza kumtimua Kocha wake Mkuu, Malale Hamsini baada ya kupoteza mechi yake iliyopita ya Ligi dhidi ya namungo FC nyumbani na kisha juzi, Simba ikamtimua Meneja wake Mkuu, Dimitar Pantev baada ya timu hiyo kufungwa na Stade Malien katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo Simba inaingia katika mechi hiyo ikiwa imepata ushindi katika mechi zote tatu za ligi ilizocheza msimu huu, matokeo yaliyoifanya iwe nafasi ya saba ikiwa na pointi tisa wakati huo Mbeya City katika mechi tisa ilizocheza, imekusanya pointi nane na ipo katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Kocha wa Simba, Selemani Matola alisema,"kwenye ligi hakuna timu nyepesi. Mbali ya ugumu huo tumejipanga na kufanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kushinda na kupata pointi tatu kwenye mchezo wa kesho.”