Robertinho aanza na sura mpya

Muktasari:

  • Mwanaspoti iliyokuwa kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena na kumshuhudia Mbrazili huyo aliyerejea kutoka kwao, aliwapigisha tizi mastaa wake wakiwamo wale waliokuwa majeruhi ambao huenda akaanza kuwatumia kwenye mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

KIKOSI cha Simba usiku wa leo usiku kitakuwa uwanjani kukabiliana na Singida Big Stars, huku kocha mkuu wa Wekundu hao, Roberto Oliveira 'Robertinho', akitarajiwa kuanza na sura mpya baada ya juzi kuwapigisha tizi mastaa wake kwa muda wa dakika 120.

Mwanaspoti iliyokuwa kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena na kumshuhudia Mbrazili huyo aliyerejea kutoka kwao, aliwapigisha tizi mastaa wake wakiwamo wale waliokuwa majeruhi ambao huenda akaanza kuwatumia kwenye mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika mazoezi hayo, Robertinho alikuwa na msaidizi wake Ouanane Sellami na benchi zima la ufundi kasoro Juma Mgunda aliyekuwa na ruhusa maalumu huku wachezaji wakiwa wote kasoro Israel Mwenda anayedaiwa kusalia kwao ila amepona majeraha na muda si mrefu atajiunga na timu.

Matizi hayo kwa ajili ya mechi dhidi ya Singida waliotoka nao sare ya 1-1 mjini Singida na juzi yalianza saa 10:30 jioni chini ya Kocha wa viungo, Kelvin Mandla aliyewasimamia mastaa hao kupasha misuli joto na kufanya mazoezi ya utimamu wa mwili yalidumu kwa dakika 15 tu.

Baada ya hapo Mbrazili aliingia kati na kutenga makundi ya watano watano kisha kuwagawia mipira mingi na kutaka wacheze 'Hangaisha bwege' kwa dakika tano kisha kuwakusanya tena na kuwabadilisha zoezi ambao alitaka wacheze kwenye eneo moja huku kila mchezaji akihitajika kugusa mpira mara mbili tu 'One Two'.

Zoezi hilo lilidumu kama kwa dakika tano hivi na kisha kocha Robertinho na Ouanane wakawagawa wachezaji katika timu tatu na kutaka wacheze wote.
Katika aina hiyo ya kucheza alisisitiza kupigwa kwa pasi chache eneo la katikati ya uwanja, kisha mpira uelekezwe pembeni na ndipo mawinga au mabeki wa pembeni wauwahi na kupiga krosi ndani ya boksi ambapo mastraika walikuwa wakisubiria mipira kufunga kwa vichwa na miguu.

Hilo lilionekana kufanywa kwa ustadi mkubwa na kumkosha zaidi Mbrazili kutokana na ubora wa wachezaji wake waliokuwa wakiuonyesha na washambuliaji Moses Phiri, Jean Baleke, Mohammed Mussa, John Bocco, Kibu Denis na Habib Kyombo kila mmoja alifunga zaidi ya mabao matatu.
Baada ya kufurahishwa na viwango vya mastaa wake kwenye mchezo huo uliochukua dakika 15 tu, Robertinho alimaliza mazoezi na kazi ikabaki kwa kocha wa viungo aliyewanyoosha misuli wachezaji kwa dakika 10 kisha kusali na kuondoka saa 11:50.

Kwa namna walivyojifua ni wazi leo kikosi cha Simba kitakuwa na mabadiliko kutokana na ubora waliounyesha wachezaji waliokuwa majeruhi siku chache zilizopita akiwemo Phiri na Henock Inonga.

Kama itakuwa hivyo basi Robertinho anaweza akaanza na, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Joash Onyango, Henock Inonga, Sadio Kanoute, Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Jean Baleke, Phiri na Saidi Ntibanzokiza 'Saido'.
Kuhusu mchezo huo, Robertinho alifunguka kutoihofia timu yeyote kwenye ligi na anaamini wachezaji wake watafanya kile atakacho waeleza na kuibuka na ushindi.

"Sina wasiwasi na timu yeyote kwasababu kila siku tunajipanga kushinda, sasa nasubiri muda ufike tuingie uwanjani na naamini wachezaji wangu hawataniangusha."

Pluijm ang'aka
Kwa upande wa Singida ambayo ipo jijini Dar es Salaam tangu majuzi, kupitia kocha wake, Hans Pluijm imesisitiza kwamba hawataki kurudia makosa yaliyowapa wapinzani wao hao sare ya 1-1 mjini Singida ama kuchezea kichapo kama ilichopewa na Yanga iliyowapiga 4-1.

"Tunaiheshimu Simba, ni timu nzuri na bora hususani ikiwa nyumbani, tumepata muda wa kutosha kujifua hapa Dar es Salaam na lengo ni kuondoka na alama tatu katika mechi hiyo," alisema Pluijm ambaye katika mechi tano zilizopita za ligi ameiongoza Simba kushinda mechi nne na kutoka sare moja kama ilivyo kwa wapinzani wao hao wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo.

Huu ni mchezo wa pili kwa timu hizi kukutana baada ya mechi ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Liti mkoani Singida Novemba 9, mwaka jana kufungana bao 1-1.
Moses Phiri ndiye kinara wa mabao kwa Simba katika Ligi Kuu Bara kwani hadi sasa amefunga 10 huku kwa upande wa Singida Big Stars anayeongoza ni Mbrazili, Bruno Gomes ambaye amefunga nane.

Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 50 huku Singida ikishika nafasi ya nne na pointi zake 43 baada ya timu zote kucheza jumla ya michezo 21.
Katika michezo hiyo Simba imeshinda 15, sare mitano na kupoteza mmoja wakati Singida imeshinda 13, sare minne na kupoteza minne.

Simba tano zilizopita
Dodoma 0-1 Simba
Simba 3-2 Mbeya City
Simba 7-1 Prisons
KMC 1-3 Simba
Kagera 1-1 Simba

Singida 5 zilizopita
Singida 1-0 Azam
Singida 1-0 Kagera
Singida 2-1 Geita
Dodoma 0-1 Singida
Mbeya City 1-1 Singida