Rekodi tamu za Yanga ikiipa kichapo Mbeya City
Muktasari:
- Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 47 ilizokusanya katika mechi 19.
Yanga imeendelea kuwa tishio katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya leo, Alhamisi, Aprili 16, 2026 kuishushia Mbeya City kipigo kikali cha mabao 6-0 katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam ikiandika rekodi mbili za kuvutia.
Ushindi huo unaifanya Yanga kuendelea kutamba juu ya msimamo wa Ligi ikifikisha pointi 47 baada ya kucheza mechi 19.
Ushindi huo mkubwa wa Yanga umetokana na mabao ya Pacome Zouzoua na Prince Dube ambao kila mmoja amepachika mabao mawili huku mengine yakifungwa na Maxi Nzengeli na Mohamed Hussein 'Tshabalala’.
Yanga imeweka rekodi ya kwanza ya kuwa timu iliyoshinda kwa ushindi mkubwa msimu huu wa mabao sita, ikifanya hivyo mara mbili ambapo awali iliichapa Mashujaa FC, mabao 6-0, Januari 19,2026.
Rekodi ya pili ya Yanga iliyoandika kwenye ushindi huo ni kuwa timu iliyoipiga kipigo kikali zaidi Mbeya City, iliyopoteza 6-0 kwa mara ya kwanza tangu timu hiyo ianzishwe.
Mara ya mwisho City ambayo haipo kwenye kiwango kizuri msimu huu kupoteza vibaya ilikuwa Desemba 31,2022 ilipochapwa 6-1 dhidi ya Azam FC ugenini.
Yanga imeipeleka City eneo gumu ikiwa timu nyingine iliyoruhusu mabao mengi,ikilinganisha na KMC ambapo zote zimefungwa jumla ya mabao 30 Kila moja mpaka sasa msimu huu.