Raphinha akataa tuzo La Liga

Muktasari:
- Raphinha ameichezea Barcelona jumla ya michezo 51 katika mashindano yote msimu huu akiwa amehusika katika mabao 51 huku akifunga 33.
Barcelona, Hispania. Staa wa Barcelona, Raphinha ameonyesha hali ya kushangazwa baada ya kupewa tuzo ya mchezaji bora wa mechi katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania wa El Clasico dhidi ya mahasimu wao Real Madrid.
Baada ya mchezo huo kumalizika ilishuhudiwa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo ikienda kwa mshambuliaji huyo raia wa Brazil ambaye alionekana kushangazwa na tuzo hiyo huku akisema hakustahili kupokea tuzo hiyo.

“Sijacheza vizuri katika mchezo wa leo, sistahili kuwa mchezaji bora wa mechi. Ninaweza kumpa hii tuzo mchezaji mwingine,” amesema Raphinha mchezaji wa Barcelona.
Raphinha ameichezea Barcelona jumla ya michezo 51 katika mashindano yote msimu huu akiwa amehusika katika mabao 51 huku akifunga 33.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Olimpic Luis Companys ilishuhudiwa Barcelona ikitoka nyuma na kupata ushindi baada ya kutanguliwa kwa mabao mawili ambayo yalifungwa na mshambuliaji wa Madrid, Kylian Mbappé.
Barcelona ilianza kurudisha mabao baada ya beki, Eric Garcia kufunga la kwanza katika dakika ya 19 akimalizia kwa kicha krosi iliyopigwa na Ferran Torres kabla ya Lamine Yamal kufunga bao la kusawazisha katika dakika ya 32.

Raphinha ambaye alifunga mabao mawili yaliyoihakikishia timu yake kuondoka na ushindi alianza kuingia wavuni katika dakika ya 34 akimalizia pasi ya Pedri kabla ya kufunga lingine mwishoni mwa kipindi cha kwanza akimalizia pasi ya Ferran Torres ambaye alitoa pasi tatu za mabao.
Katika kipindi cha pili Barcelona haikuweza kufunga bao lingine huku nyota wa Madrid, Kylian Mbappé akifunga mabao matatu (Hat trick) baada ya kumalizia pasi ya Vinicius Junior katika dakika ya 70.

Hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika Barcelona ilichomoza na ushindi wa mabao 4-3 ikiwa ni kwa mara ya nne mfululizo wanaifunga Real Madrid ndani ya msimu mmoja.