Onana wa Everton dili Ulaya

Barcelona, Hispania. Ubora alionao kiungo wa Everton na Timu ya Taifa ya Ubelgiji, Amadou Onana umemfanya kuwa dili Ulaya baada ya vigogo wakubwa wa soka barani humo kupigana vikumbo kuiwania saini yake.

Imeripotiwa kwamba Barcelona ipo tayari kutunishiana misuli na Manchester United na Arsenal kwenye mchakamchaka wa kunasa huduma ya kiungo huyo ambaye pia Bayern Munich inamtaka ikiamini anafaa kwenda kuchukua nafasi ya Joshua Kimmich huko Allianz Arena.

Onana mwenye asili ya Senegal, amekuwa nguzo muhimu kwenye kikosi cha Ubelgiji kinachoshiriki michuano ya Euro 2024 inayoendelea nchini Ujerumani ambapo kesho Jumatatu watacheza dhidi ya Ufaransa hatua ya 16 bora akiwa amecheza mechi tatu za makundi kwa dakika zote.

Awali, Barcelona ilikuwa ikihusishwa sana na Kimmich baada ya kuripotiwa kwamba Bayern ipo tayari kuachana na kiungo huyo, ambaye amecheza mechi 390 kwenye kikosi chao na kushinda mataji 20 huku akiingia mwaka wa mwisho kwenye mkataba wake.

Lakini, ripoti ya mwezi uliopita ilibainisha kwamba Kimmich amekataa ofa ya Barcelona na tangu hapo hakuna kilichoendelea.

Hansi Flick, ambaye amechukua mikoba ya kuinoa Barcelona, anafahamu wazi miamba hiyo ya Nou Camp ipo sokoni kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kutafuta kiungo mpya hivyo baada ya kuripotiwa Kimmich kukataa ofa hiyo, sasa wamehamia kwa Onana wa Everton. Kiungo mwingine aliyepo kwenye rada yao ni Mikel Merino wa Real Sociedad.

Bayern chini ya kocha Vincent Kompany, ambaye ni Mbelgiji anahitaji saini ya Onana baada ya kuona kuna ugumu kwenye mpango wao wa kumsajili Joao Palhinha. Arsenal yenyewe pia inamtaka Onana kwa sababu bado haina uhakika juu ya hatima ya staa wa Ghana, Thomas Partey.

Onana bado ana mkataba hadi Juni 30, 2027 kwenye kikosi cha Everton, lakini tatizo la uchumi linaweza kuilazimisha klabu hiyo ya Goodison Park kufanya biashara ya kumpiga bei kiungo huyo kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi wakati thamani yake ikitajwa kuwa ni euro 50m.