Usajili wa Mukwala na siri iliyojificha Simba

Mshambuliaji mpya wa Simba, Steven Mukwala raia wa Uganda.

Muktasari:

  • Mukwala aliyetambulishwa leo Jumanne, ni mshambuliaji kinara ambaye anatarajiwa kuongoza idara ya ushambuliaji ya Simba kutokana na kile ambacho alichokifanya msimu uliopita akiwa na Asante Kotoko ya Ghana, ambapo alipachika mabao 14.

Dar es Salaam. Utambulisho wa washambuliaji wapya ndani ya Simba, Steven Mukwala raia wa Uganda na Joshua Mutale raia wa Zambia wenye umri chini ya miaka 25, umebeba taswira ya safari mpya ambayo Wekundu hao wa Msimbazi wanaianza msimu ujao bila ya kuwa na baadhi ya wachezaji waandamizi ambao wameonyeshewa mlango wa kutokea.

Mukwala aliyetambulishwa leo Jumanne, ni mshambuliaji kinara ambaye anatarajiwa kuongoza idara ya ushambuliaji ya Simba kutokana na kile ambacho alichokifanya msimu uliopita akiwa na Asante Kotoko ya Ghana, ambapo alipachika mabao 14 alishika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji katika ligi hiyo akiwa na idadi sawa ya mabao na Agyenim Boateng Mensah.

Kabla ya Mukwala, jana Jumatatu Simba ilimtambulisha Mutale ambaye ni kiungo mshambuliaji. Mchezaji wa kwanza kutambulishwa alikuwa beki wa kati Lameck Lawi. Utambulisho wake ulikuwa Juni 20 mwaka huu akitokea Coastal Union.

Wachezaji wote hao wamepewa mikataba ya miaka mitatu kila mmoja kitu ambacho kinadhihirisha kwamba Simba ina malengo nao ya muda mrefu ndiyo maana wameangalia umri wao na muda wa mikataba waliyowapa.

Simba inaonekana kudhamiria kukisuka upya kikosi chake baada ya kuangushwa kwa ufalme wao na Yanga huku mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji 'MO' akionekana kuwa mbele katika mchakato huo, alianza kwa kubariki kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wakongwe akiwemo Hennock Inonga, Saidi Ntibazonkiza 'Saido' na hata John Bocco.

Kisha akahusika kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji muhimu ambao wamewaongeza mkataba ambao ni Kibu Denis, Shomary Kapombe, Israel Mwenda na Mzamiru Yassin kabla ya kumwaga fedha za usajili na bado inaelezwa kuna majina mengine makubwa yatashushwa katika dirisha hili la usajili.

Mukwala ambaye amesaini Simba mkataba wa miaka mitatu, ana urefu wa futi 5.9 na ana uwezo wa kufunga mabao ya aina tofauti lakini pia ni mzuri kwenye mipira ya juu na mipira ya krosi ambayo Fredy Michael na Pa Omar Jobe walioingia wakati wa dirisha dogo walishindwa kuitumia vyema.

Moja ya eneo ambalo lilikuwa na upungufu msimu uliopita ni katika safu ya ushambuliaji na ujio wa Mukwala utaongeza uimara wa timu. Nyota huyo amewahi kuzitumikia timu za Vipers FC, Maroons FC zote za Uganda kabla ya kutimkia Asante Kotoko ya Ghana.

Katika dirisha hili la usajili, Simba ilianza kwa kumtambulisha beki wa kati, Lameck Lawi (18) kutoka Coastal Union ya Tanga kisha akafuta Mutale ambaye amesajiliwa kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Power Dynamos ya Zambia.

Mutale mwenye miaka 22, anamudu nafasi ya winga ya kulia, kushoto na wakati mwingine anacheza nyuma ya mshambuliaji yaani namba 10. Uwezo wake wa kumudu kucheza nafasi nyingi uwanjani pamoja na umri ni miongoni mwa vigezo viliwavutia Simba kuwasajili wachezaji hao kwa mujibu wa Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally.

"Simba inayokuja itakuwa bora na imara zaidi, tutaendelea kushusha vyuma (wachezaji) kulingana na mipango tuliyonayo, Wanasimba wanatakiwa kuwa na imani ya kile ambacho kinafanyika," alisema.

Gazeti hili linafahamu kuwa Mutale, Mukwala na Debora Fernandes ambaye bado hajatambulishwa kutoka Mutondo Stars ya Zambia, walifichwa kwenye moja ya hoteli kubwa jijini Dar es Salaam siku chache zilizopita baada ya kumalizana nao.

Mara baada ya kutambulishwa kwa Lawi, Mutale na Mukwala huenda anayefuata akawa ni Debora ambaye ni kiungo mkabaji huku ikielezwa kwamba bado vigogo wa Simba wanahaha kupata mbadala wa Inonga aliyejiunga na FAR Rabat ya Morocco, majina yaliyopo mezani kwao ni Nathan Idumba wa Cape Town City na Chamou Karaboue wa Racing Club d'Abidjan. Karaboue anatazamwa kama chaguo la pili ikiwa dili la kumnasa Idumba litakwama ingawa bado mazungumzo yanaendelea.

Akimzungumzia Mukwala, kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm ambaye yupo Ghana ambako mchezaji huyo ametoka, amesema anaweza kuwa msaada kwa Wekundu hao wa Msimbazi kutokana na ubora ambao ameuonyesha akiwa na Asante Kotoko.

"Sidhani kama anaweza kuathirika na mazingira kwa sababu ni mchezaji ambaye ametokea ukanda huo (Afrika Mashariki), nimemuona mara kadhaa ni mshambuliaji mzuri, mwenye nguvu na maarifa," alisema kocha huyo.

Kwa upande wake, Richard Mensah ambaye ni mwandishi na mchambuzi wa michezo Ghana, naye amemuongelea mshambuliaji huyo kwa kusema msimu uliopita alionyesha utofauti mkubwa licha ya Asante Kotoko kutokuwa katika kiwango bora.

"Sote tunajua huku kuwa Asante haikuwa katika kiwango bora, lakini amejipambanua na kuonyesha kuwa yeye ni mshambuliaji hatari, ana uwezo mzuri wa kutumia mwili na amefunga sana mabao ya kichwa, anaweza kutuliza timu na kutoa nafasi kwa wachezaji wenzake kusogea akiwa na mpira mbele," alisema na kuongeza;

"Kama wachezaji wenzake watajua namna gani anapaswa kucheza naye basi tunaweza kumuona akiendelea kufunga kama ilivyokuwa msimu uliopita."

Wachezaji wapya ndani ya Simba waliotambulishwa mpaka sasa ni Lameck Lawi (18), Joshua Mutale (22) na Steven Mukwala (24). Waliopo kwenye rada zao ni Fasika Idumba (25), Agustine Okejepha (20), Debora Mavambo (24), Elie Mpanzu (22), Jean Charles Ahoua (22) na Valentino Nouma (24).


ANGALIZO

Hata hivyo, siku zote usajili wa mchezaji unachukuliwa kama ni kubahatisha kutokana na uwezekano wa kufanikiwa au kufeli, kitendo cha kuwapa mikataba ya miaka mitatu wachezaji hao inaweza kuwagharimu katika kuivunja pindi mambo yakienda tofauti.

Tumeshuhudia mchezaji baada ya kusajiliwa anaondolewa muda mfupi kutokana na kushindwa kuonyesha uwezo uliotarajiwa, mwisho wa siku wanavutana katika kuvunja mkataba jambo linalosababisha baadaye kufikishana kwenye mamlaka husika kudaiana.

Lakini akili kubwa ambayo Simba inaweza kuitumikia ni kwamba katika mikataba hiyo ya miaka mitatu, kipengele cha kuvunja ikitokea mchezaji hajafikia malengo kinaweza kuokoa na matatizo hayo.