Arsenal yambeba Raya jumla

Muktasari:

  • Raya ni miongoni mwa wachezaji 26 wanaounda kikosi cha Hispania kinachoshiriki Fainali za Euro 2024 huko Ujerumani.

London. Arsenal inaripotiwa imelipa kiasi cha Pauni 27 milioni kwa Brentford ili kumsajili moja kwa moja Kipa David Raya katika dirisha linaloendelea la majira ya kiangazi.

Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta amefanikiwa kuushawishi uongozi wa timu hiyo kumsajili moja kwa moja Raya baada ya kukoshwa na kiwango chake katika msimu uliomalizika.

Raya ambaye aliichezea Arsenal kwa mkopo wa msimu mzima akitokea Brentford alitoa mchango mkubwa katika kuifanya timu hiyo kuwa na ukuta imara ambao uliruhusu idadi ndogo zaidi ya mabao kuliko nyingine ambapo ilifungwa mabao 29 tu.

Katika mkataba huo wa mkopo, kulikuwa na kipengele cha Arsenal kumnunua Raya moja kwa moja ikiwa ingeridhika na kiwango chake jambo ambalo limefanywa rasmi na uongozi wa timu hiyo.

Inaripotiwa kwamba kinachochelewesha kutambulishwa kwa mkataba wa moja kwa moja wa Raya ndani ya Arsenal ni uwepo wa Kipa huyo kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Hispania nchini Ujerumani inakoshiriki fainali za Euro.

Raya aliibuka mshindi wa tuzo ya Kipa bora wa Ligi Kuu ya England msimu uliomalizika baada ya kucheza idadi kubwa ya michezo bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa (clean sheets).

Kipa huyo hakuruhusu bao katika mechi 20 kati ya 32 alizoichezea Arsenal kwenye EPL msimu uliomalizika.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 ni miongoni mwa wachezaji ambao Arsenal imewatumia katika utambulisho wa jezi mpya za msimu ujao jambo linalothibitisha kipa huyo atakuwepo msimu ujao.