Prime
Ngoma afichua ramani ya kumchinja Mwarabu kwa Mkapa

Muktasari:
- Kutokana na deni hilo walilonalo Wekundu wa Msimbazi lililotokana na kichapo cha mabao 2-0 ugenini, mastaa wa timu hiyo akiwamo Jean Charles Ahoua na Elie Mpanzu kwa pamoja wameamua kufanya kikao kizito ambacho kiungo wa timu hiyo, Fabrice Ngoma amefichua namna walivyoweka mikakati ya kufanikisha malengo hayo.
Simba ina kibarua kizito Jumatano hii dhidi ya Al Masry huku ikifahamu kwamba ili kuvuka moja kwa moja kucheza nusu fainali, inapaswa kushinda kuanzia mabao 3-0.
Kutokana na deni hilo walilonalo Wekundu wa Msimbazi lililotokana na kichapo cha mabao 2-0 ugenini, mastaa wa timu hiyo akiwamo Jean Charles Ahoua na Elie Mpanzu kwa pamoja wameamua kufanya kikao kizito ambacho kiungo wa timu hiyo, Fabrice Ngoma amefichua namna walivyoweka mikakati ya kufanikisha malengo hayo.
Mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya robo fainali, unatarajiwa kuchezwa Aprili 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa Saa 10:00 jioni.
Ngoma ambaye amekuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza ndani ya Simba akicheza mechi zote nane za kimataifa msimu huu, ameliambia Mwanaspoti kuwa, wamezungumza wao wenyewe kuelekea mchezo huo na kugundua mambo mawili yamewaangusha, hivyo lazima wayafanyie kazi ili kuvuka kwenda nusu fainali.
Kiungo huyo raia wa DR Congo, amesema jambo la kwanza lililowaangusha zaidi ni kuondoka ugenini bila ya kufunga bao, huku jingine ni kukosa utulivu katika kuzima mashambulizi ya wapinzani wao na kujikuta wakiruhusu mabao mawili kule Misri.
Ngoma amesema, baada ya mazungumzo hayo, wachezaji wamekubaliana kwamba wanatakiwa kucheza kwa nguvu kubwa kama mnyama Simba anapokuwa mawindoni kwa kuhakikisha wanalinda heshima ya klabu na kuwafurahisha mashabiki wao kwa kupindua meza watakaporudiana na Waarabu hao.
“Kila mmoja aliumia kwa namna tulivyopambana lakini tukashindwa kufunga mabao, kama haitoshi tukaruhusu mabao ambayo kila ukiyakumbuka yanakuumiza moyo,” alisema Ngoma ambaye ni nahodha msaidizi wa kikosi hicho na kuongeza:
“Tunajua makocha watakuja na marekebisho yao, lakini kwanza sisi kama wachezaji lazima tujiandae tofauti, wao (Al Masry) walishinda kwao na sisi hapa ni kwetu tunatakiwa kulinda hadhi ya mashabiki wetu na viongozi wetu, tunatakiwa kuyapindua haya matokeo kwa nguvu yoyote, tunatakiwa kucheza kama alivyo mnyama Simba anapokuwa mawindoni.”
Wakati Ngoma akiyasema hayo, beki wa kikosi hicho Chamou Karaboue aliongeza kuwa kuelekea mchezo huo wa marudiano wana kazi mbili tu, kwanza kuhakikisha wanafunga mabao na wala hawatakiwi kucheza kwa presha kwani itawaharibia.
Chamou alisema mbali na kufunga mabao lakini pia kwenye ukuta wao wanatakiwa kuhakikisha hawaruhusu bao ambalo litawapa mlima mrefu zaidi kuupanda.
“Hii ni mechi muhimu ambayo tunakwenda kucheza, tukiwa ugenini tulishindwa kupata bao lakini hapa nyumbani ni lazima tubadilishe mambo kwa kuhakikisha tunapata mabao mengi,” alisema beki huyo raia wa Ivory Coast.
“Ukiacha kufunga, ni lazima tujiandae sawasawa, hatutakiwi kufanya makosa ya kuruhusu bao lolote, tunahitaji umakini mkubwa kule nyuma hili tutalihakikisha linafanikiwa. Mashabiki wetu ni watu muhimu, tunajua waliumizwa na matokeo ya mchezo wa kwanza lakini Simba ina rekodi kubwa nyumbani, waje kwa wingi uwanjani, tunataka sauti zao ili tubadilishe mambo tusonge mbele.”
Simba mechi 10 zilizopita za mashindano ya Afrika pekee imepoteza 1 dhidi ya Al Ahly.
Mechi hiyo dhidi ya Ahly ya Misri, Simba ililala kwa bao 1-0 la kiungo Ahmed Kouka, mchezo uliopigwa Machi 29, 2024. Mbali na hapo, Simba imeshinda mechi nane kati ya 10, ikitoka sare mara moja moja huku ikifunga mabao 17.
Rekodi hiyo ndio imerejesha mzuka wa mastaa wa Simba kuelekea kuikabili Al Masry huku pia msimu huu wakiwa vizuri kwa mechi za nyumbani tangu hatua ya pili hadi makundi walipomaliza kinara wa Kundi A ambapo mechi nne ilizocheza Benjamin Mkapa, imeshinda zote ikifunga mabao manane na kuruhusu mawili.
Simba kuanzia 2018-2019, licha ya kucheza robo fainali tano hii ikiwemo ya sita, imeshindwa kuvuka kwenda nusu fainali jambo ambalo limekuwa likiwaumiza vichwa.
Katika robo fainali tano zilizopita ambazo Simba imecheza nyumbani, imeshinda tatu, imepoteza moja na sare moja. Hata hivyo, ushindi wa mechi hizo haukuwa na faida kufuatia matokeo ya jumla kuwahukumu.