Mbappe apunguza kilo sita adaiwa kula chakula chenye sumu

Muktasari:
- Mbappe alipoteza kilo sita jambo linalohatarisha maandalizi yake kuelekea msimu mpya.
New Jersey, Marekani. Nyota wa Real Madrid, Kylian Mbappe ameripotiwa kupungua uzito kwa kiasi kikubwa kufuatia kuugua maumivu ya tumbo baada ya kula chakula chenye sumu ya akiwa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu, hali iliyoibua hofu kubwa ndani ya klabu hiyo.

Kwa mujibu wa jarida la L’Equipe la Ufaransa, Mbappe alipatwa na maumivu makali ya tumbo na kuonyesha dalili za upungufu wa maji mwilini kuanzia Juni 14, siku ambayo kikosi cha Real Madrid kilisafiri kutoka Hispania kwenda Miami, Marekani kwa ajili ya mashindano hayo.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 alikosa mechi zote tatu za hatua ya makundi na alilazwa hospitalini mara baada ya mechi ya kwanza dhidi ya Al-Hilal kutokana na maumivu makali ya tumbo, hali iliyotokana na kula kuku waliokuwa na bakteria hatari.

Ripoti zinasema Mbappe alipoteza kilo sita jambo linalohatarisha maandalizi yake kuelekea msimu mpya, kwani wachezaji wa kiwango chake huwa na uzito wa kudhibitiwa kwa uangalifu mkubwa.
Ingawa aliweza kuingia kipindi cha pili na kufunga bao dhidi ya Borussia Dortmund, Mbappe bado yupo mashakani kushiriki mchezo wa nusu fainali dhidi ya PSG timu yake ya zamani aliyoondoka kwa sintofahamu kubwa mwaka jana.
Real Madrid wameandika barua kwa Shirikisho la soka Hispania (La Liga) wakiomba tarehe ya kuanza msimu mpya wa ligi icheleweshwe kutoka Agosti 19, wakieleza hofu kuwa wachezaji wao hawatapata muda wa kutosha kupumzika baada ya mashindano haya ya Kombe la Dunia la Klabu.

Kwa mujibu wa makubaliano ya mwaka 2023 kati ya La Liga na chama cha wachezaji (AFE), kila mchezaji anapaswa kupata mapumziko ya wiki tatu kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya (pre-season) jambo ambalo kwa sasa linaonekana kuwa gumu kwa wachezaji wa Madrid.
Ikiwa Real Madrid watafika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu, watacheza dhidi ya Chelsea Julai 13, hivyo kuwa na takribani wiki tano tu kabla ya msimu mpya wa La Liga kuanza.
Mbali na masuala ya kiafya, Mbappe pia bado anabeba mizigo ya mvutano wake na PSG, ambapo licha ya kuacha kufuatilia kesi ya kisheria aliyowasilisha dhidi ya klabu hiyo kwa tuhuma za unyanyasaji wa kimaadili, bado anadai malipo ya €55 milioni (Sh154 bilioni) ambazo anadai ni mishahara na bonasi alizostahili kabla ya kuondoka.

PSG kwa upande wao wanadai kuwa Mbappe alikubali kuacha fedha hizo alipokuwa akiondoka, na wamefungua madai ya kupinga wakitaka alipwe Pauni milioni 84 (Sh277 bilioni) kwa mujibu wa mkataba wao wa mwisho.
Mbappe aliondoka PSG baada ya misimu saba ya mafanikio, lakini uhusiano wake na uongozi wa klabu hiyo ulivunjika vibaya, huku akilazimishwa kufanya mazoezi na wachezaji wa akademi msimu uliopita kama sehemu ya adhabu ya kutotaka kusaini mkataba mpya.