Prime
Namba za Dube Yanga zinavyomtofautisha na Baleke, Musonda, Mzize

Muktasari:
- Musonda ambaye amekuwa hatumiki sana katika kikosi cha Yanga msimu huu, takwimu zinaonyesha ndiye mchezaji ambaye ana wastani mzuri wa kufunga mbele ya wenzake watatu.
Benchi la ufundi la Yanga, limekuwa likimpa nafasi kubwa ya kucheza Prince Dube kulinganisha na washambuliaji wengine, lakini tathmini ya takwimu za kufumania nyavu baina yao zina maajabu yake.
Kwa misimu mitatu Yanga imebeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikiwa na namba za kutisha, huku ikutanapo na timu pinzani zimekuwa zikicheza katika hali ya kuiogopa zaidi, kwani zikizubaa lolote linaweza kuzitokea.
Lakini katika suala la ufumaniaji nyavu, takwimu
zinaonekana kuwa kwa mshambuliaji raia wa Zambia, Kennedy Musonda akifuatiwa na Clement Mzize, Jean Baleke kisha Dube.
Musonda ambaye amekuwa hatumiki sana katika kikosi cha Yanga msimu huu, takwimu zinaonyesha ndiye mchezaji ambaye ana wastani mzuri wa kufunga mbele ya wenzake watatu.
Ukiondoa Ngao ya Jamii, Yanga imecheza mechi 13 hadi sasa ambapo tisa ni za Ligi Kuu na nne za Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo washambuliaji wake hao wote wanne wa kati wametumika kwa nyakati tofauti.
Mshambuliaji aliyecheza kwa dakika chache zaidi katika kikosi cha Yanga ni Kennedy Musonda ambaye ametumika dakika 102 katika mechi saba alizopewa nafasi, sita zikiwa za Ligi Kuu na moja Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo ana wastani wa kutumika kwa dakika 15.

Lakini, hata hivyo, nyota huyo wa Zambia takwimu za kufunga ndizo zinaonekana za moto kwani katika dakika hizo 102 ambazo Musonda ameitumikia Yanga ambapo dakika 82 ni kwenye Ligi Kuu na 66 za Ligi ya Mabingwa Afrika akifunga bao moja, hivyo ana wastani wa kufunga angalau bao 0.8 kwa mchezo ambao ni namba kubwa zaidi ya wengine.
Jean Baleke amecheza mechi tano za Yanga ambapo nne ni za ligi na moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika, katika mechi hizo tano ametumika kwa dakika 153 akifunga bao moja.
Bao hilo moja ambalo Baleke amefunga katika dakika 153 linamfanya Baleke awe na wastani wa kufunga bao 0.6 kwa mechi.
Prince Dube ndiye mchezaji ambaye ameonekana kuaminiwa zaidi na benchi la ufundi la Yanga kwani hadi sasa ndiye aliyecheza kwa dakika nyingi zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu ambapo katika mechi hizo amepewa dakika 592.

Dakika hizo 592 ni katika mechi 11 ambazo nane ni za Ligi Kuu na tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo nyota huyo wa Zimbabwe amezitumia kufunga mabao mawili yanayomfanya awe na wastani wa kufunga bao 0.3 kwa mechi.
Mshambuliaji anayemfuatia Dube kwa kucheza dakika nyingi ndani ya kikosi cha Yanga msimu huu ni Clement Mzize ambaye katika mechi 11 alizoitumikia Yanga, tisa zikiwa za Ligi Kuu na mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika, benchi la ufundi la timu hiyo limemtumia kwa dakika 485.
Katika dakika hizo 485, Clement Mzize ameziona nyavu za timu pinzani mara tatu, jambo linalomfanya awe na wastani wa kufunga bao 0.6 kwa mchezo kama ilivyo kwa Baleke.
Musonda hajawakimbiza wenzake ndani ya Yanga tu, kwani hata katika timu za mataifa yao ameonyesha kutoa mkubwa zaidi.

Msimu huu, Musonda ndiye mshambuliaji wa kati wa Yanga aliyehusika na idadi kubwa ya mabao kulinganisha na wengine.
Musonda amecheza mechi nne za Zambia ambazo zote ni za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 ambapo katika michezo hiyo, amehusika na mabao matatu, akifunga mawili na kupiga pasi moja ya mwisho.
Prince Dube amehusika na bao moja ambalo amelifunga katika mechi nne alizoichezea Zimbabwe kwenye mashindano hayo ya kufuzu Afcon.
Clement Mzize katika mechi nne alizochezea Taifa Stars hajahusika na bao lolote huku Baleke akiwa hajapata hata hiyo fursa ya kuitwa katika kikosi cha timu yake ya taifa ya DR Congo.

WASIKIE WAKONGWE
Akiwazungumzia washambuliaji hao, straika wa zamani wa Yanga, Jerry Tegete alisema anaamini Dube kuna sababu inayomfanya apewe nafasi kubwa ya kucheza na kuhusu kutofunga, anadhani muda utafika atakuwa hashikiki kufumania nyavu.
“Ingawa Dube bado hajafanikiwa kufunga anapaswa kuendelea kupambana kwa bidii na kuwa na uvumilivu, kwani mabao yatakuja tu,” alisema Tegete na kuongeza kuwa nyota huyo ana kipaji kikubwa na uwezo wa kufunga, hivyo ni suala la kujiamini na kutochoka.
Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema hana shaka na kipaji cha Dube.
“Kila mshambuliaji ana wakati mgumu katika kazi yake, lakini hatua za ziada katika mazoezi na juhudi za kutafuta mabao zitamsaidia kujijenga. Dube anapaswa kuendelea kutafuta nafasi kwenye mchezo na kuboresha umaliziaji wake ili hatimaye apate mafanikio anayoyatarajia,” alisema.