Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SIO ZENGWE: Yanga, Gamondi wamewajibu ‘wa kiwango kushuka’

Zengwe Pict

Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akifurahia na mashabiki.

Muktasari:

  • Kwa nini? Ni kwa sababu klabu hizo zina ukubwa uliokithiri hivyo hata robo tu ya Watanzania wakifuatilia hata mjadala wenyewe usiwe na afya kimpira, ni mafanikio makubwa.

Sijui mijadala mingine huibukia wapi? Labda kutokana na kukosa maudhui yanayoweza kukubaliwa na wengi na hivyo kutafuta kuhusisha mjadala wowote au kuibua jambo lolote lile kuhusu klabu za Simba na Yanga ili mjadala huo ufuatiliwe.

Kwa nini? Ni kwa sababu klabu hizo zina ukubwa uliokithiri hivyo hata robo tu ya Watanzania wakifuatilia hata mjadala wenyewe usiwe na afya kimpira, ni mafanikio makubwa.

Kwa sababu ya mitandao ya kijamii kufuatiliwa na yeyote yule, basi mjadala wowote unaopingana na hali halisi, au kusababisha utata, utakuwa na nguvu kubwa. Ndiyo maana kila kukicha ni habari na mijadala kuhusu Simba na Yanga.

Katika moja ya mijadala iliyodumu kwa muda mrefu ni ule wa kushuka kwa kiwango cha Yanga. Sina hofu hata huu ulitokana na waanzishaji mjadala kukosa maudhui muhimu katika mwenendo wa mabingwa hao wa Bara msimu huu.

Mjadala umejikita katika matokeo ya ushindi finyu wa Yanga baada ya msimu uliopita kushusha vipigo vilivyoipa ubingwa mapema na kusababisha mechi za mwisho ziwe za kukamilisha ratiba na hata kutoa nafasi kwa wachezaji kufikia malengo yao binafsi, kama ilivyokuwa kwa Stephane Aziz Ki aliyejitangazia ufalme wa kupachika mabao katika siku ya mwisho.

Siku hiyo ilikuwa kama mchezaji huyo wa Burkina Faso hakujikita kukamilisha mafanikio hayo binafsi, lakini msukumo wa mashabiki na mbinu za kocha zilimfanya aongeze bidii na kuimaliza mechi kwa kufikisha mabao 21.

Lakini msimu huu akasema lengo lake uwanjani si kuwa mfungaji bora bali kuisaidia timu yake kushinda na akaeleza furaha yake kwa timu kumpata Prince Dube, akisema ndiye atakayebeba mzigo huo wa ufungaji.

Mjadala huo wa kushuka kwa kiwango cha Yanga ukajikita pia kwa Aziz Ki, amechangia kushuka kiwango kwa Yanga kwa kushindwa kupachika mabao mengi hadi sasa, licha ya klabu hiyo kuwa na washambuliaji watatu kwa sasa, Clement Mzize, Kennedy Musonda na Jean Baleke.

Haiwezekani timu ambayo kiwango chake kimeshuka, ilikuwa inashinda mechi zake zote za awali bila ya kutetereka. Ungetegemea timu inayoshinda, inatoka sare, ndiyo ielezewe imeshuka kiwango kwa kukosa mlolongo wa matokeo mazuri. Hapo hapo timu ambayo imetoka sare, ikafungwa na baadaye ikahangaika kupata ushindi, ndiyo ikaelezewa imepanda kiwango.

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Maxi Nzegel akikokota mpira wakati wa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC katika uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam. 

Hata wale Singida Black Stars waliokuwa hawajakubali kipigo, bado walionekana wako chini kwa kiwango. Kama timu iliyokuwa ikishinda kwa bao 1-0 imeshuka kiwango, vipi timu zilizokuwa zikuikubali vipigo hivyo? Mambo ya ajabu kabisa.

Kipigo cha kwanza kwa Yanga msimu huu cha bao 1-0 walichopewa na Azam FC kinaweza kuwapa ahueni waendesha mijadala hiyo, wakijipa moyo angalau kimethibitisha hoja yao, Yanga imeshuka kiwango msimu huu.

Ni kipigo kilichotokana na bao lililofungwa na Gibril Sila kipindi cha kwanza, ikiwa ni dakika chache baada ya beki imara wa kati wa Yanga, Ibrahim Bacca kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumvuta mshambuliaji wa Azam, Nassor Hamoud Saadun wakati akienda kumuona kipa Djigui Diarra.

Kwa hiyo kwa takriban dakika 70, Yanga ilicheza pungufu ya mchezaji mmoja, lakini hali haikuwa dhahiri uwanjani. Ilikuwa ni kama hakuna mchezaji aliyetolewa kwa kadi nyekundu na kuna wakati ilionekana kama Azam FC ndio wako pungufu kutokana na kupoteza muda kila wakati hadi kipa akaonywa na baadaye kuonyeshwa kadi ya njano.

Mchezo wa kushambulia, mbinu ya kuua upande mmoja wa kulia na kutumia zaidi wa kushoto, umiliki wa mpira – ambao kiufundi ulitakiwa uwe juu kwa upande wa Azam, ukawa upande wa timu ambayo ilikuwa pungufu na utengenezaji nafasi za wazi kwenye lango la Azam, ulitosha kuwa majibu kwa waendesha mijadala yote iliyohusu kushuka kiwango kwa timu hiyo.

Kwa mtu ambaye aliingia uwanjani dakika ya 50 asijue kilichotokea kipindi cha kwanza, angeamini hakuna mchezaji aliyepungua kwenye timu hizo mbili na zaidi angedhani kwa jinsi Azam ilivyozidiwa pengine ndiyo ilikuwa pungufu.

Hili ni somo tosha kwa wachambuzi na waendesha mijadala isiyo na takwimu za kutosha na tafsiri sahihi kuhusu hali ya timu. Kama ni vichwa ngumu, wataendelea na hoja hiyo wakijikita kwenye matokeo takwimu ambazo hazionyeshi hali halisi ya mchezo wala kukupa ubora wa timu.

Ndiyo maana timu yaweza kuwa inapiga mashuti kutoka katikati ya uwanja na mpira ukafika umepoa golini lakini ikahesabiwa imepiga mashuti mengi yaliyolenga lango, kumbe ilitokana na kubanwa kulifikia lango la wapinzani. Mchezo huo ukiisha kwa sare, mchambuzi wa aina hii atakwambia timu iliyopiga mashuti mengi yaliyolenga lango ndiyo ilikuwa bora Zaidi.

Ni muhimu sana kwa mijadala yetu ilenge kuwaambia watu kinachoendelea kwenye michezo na si kinachoendelea Simba na Yanga. Kufuatilia vitu hata visivyo na maana, vinavyoendelea Simba na Yanga eti kwa sababu zinafuatiliwa na wengi, ni kulipumbaza taifa hadi kufikia kiwango cha juu cha ujinga.

Wachezaji kama Yusuf Kagoma, Saadun na Adolph Mutasingwa walifanya vizuri sana msimu uliopita, lakini ilikuwa vigumu kukuta waendesha mijadala wakiweka masuala yao watatu hao na wengine kwenye mijadala yao. Kwa nini? Kwa sababu tu hawakuwa Simba na Yanga.

Ni afadhali Kagoma alikuwa katikati ya mijadala mwanzoni mwa msimu na anaweza kuendelea kuwa mjadala kwa sababu ya uhamisho wake kwenda Simba. Lakini Saadun, Mutasingwa na wengine wataendelea kuonekana siku Azam FC ikicheza na Simba au Yanga tu.

Hata Silla alipofunga bao la aina yake msimu uliopita, halikuwa mjadala sana kama ambavyo angefunga Aziz Ki, Pacome Zouzoua au Kibu Dennis. Shukrani ziende kwa watoaji tuzo walioliona na kumuenzi.

Umaarufu, kusikilizwa na kusomwa kusitokane na kuzungumzia timu zilizo maarufu, bali hoja iliyojengwa ndani ya safu yako, kipindi chako au taarifa yako.

Kwa hiyo tusirahisishe mambo kwa kutaka kusikilizwa au kusomwa au kuonekana kwa kuzungumzia mambo ya Simba na Yanga kila kukicha.

Tukiendelea na tabia kama hiyo, timu, makocha na wachezaji watatujibu uwanjani kama ilivyofanya Yanga na kocha wao Miguel Gamondi Jumamosi. Timu pungufu, lakini inacheza katika ubora uleule na pengine hata kuizidi timu iliyokamilika.