Mwanariadha amwagiwa petroli, kuchomwa moto na mpenzi wake

Mwanariadha wa Uganda, Rebecca Cheptegei. Picha na Al Jazeera
Muktasari:
- Mwanariadha Cheptegei alishiriki mbio za marathon za wanawake katika Michezo ya Olimpiki ya Paris mwezi uliopita.
Kenya. Mwanariadha wa Uganda wa mbio za Marathon, Rebecca Cheptegei yuko mahututi hospitalini baada ya kuchomwa moto na mpenzi wake Dickson Marangach huku sababu ikitajwa ugomvi uliosababishwa na mgogoro wa kiwanja pamoja na nyumba.
Kwa mujibu wa tovuti ya Nation ya Kenya, tukio hilo limetokea juzi Jumapili ya Septemba 1, 2024 eneo la Kinyoro, Kaunti ya Trans Nzoia Kenya.
Mpenzi wake alimmwagia petroli kisha kumuwasha moto kwa kutumia kiberiti.
Taarifa zaidi zinasema moto ulimuunguza pia na mpenzi wake huyo Mkenya, ambao kwa sasa wote wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Moi huko Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.
Hata hivyo, Al Jazeera imesema Cheptegei ambaye alishiriki katika mbio za marathon za Olimpiki Paris mwezi uliopita, ameungua robo tatu ya mwili wake.
Inaelezwa Cheptegei alirejea kutoka kanisani na kumkuta Marangach akimsubiri kisha kumchoma.
Aidha, ripoti za awali zinaonesha wawili hao wamekuwa wakizozana mara kwa mara kwasababu ya nyumba na kiwanja.
Chifu wa eneo hilo, Rose Chebet amesema tukio hilo lilitokea saa mbili usiku wakati Marangach alipoingia kinyemela nyumbani na baada ya ugomvi aliwasha moto ingawa na yeye pia alishikwa na moto huo.
Majirani waliuzima moto huo, na kuwakimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kitale ambako walilazwa wakiwa na majeraha kabla ya kuhamishiwa Moi Teaching kwa matibabu.
Naibu Kamanda wa Kaunti ya Trans Nzoia, amethibitisha kisa hicho na kusema kuwa uchunguzi unaendelea.