Mtine amtega CEO mpya Simba

Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andrew Mtine (kushoto) na Mtendaji Mkuu mpya wa Simba, Francois Regis (kulis). Picha na Mtandao
Muktasari:
- Francois Regis, mtendaji mkuu mpya wa Simba, anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha timu inapata mafanikio uwanjani, kufuatia mafanikio makubwa ya Andrew Mtine wa Yanga.
Dar es Salaam. Licha ya mafanikio yanayoelekea kufanana katika upande wa utawala, mtendaji mkuu mpya wa Simba, Francois Regis ana kibarua kizito cha kuhakikisha timu hiyo inapata mafanikio ya uwanjani ili kufunika kile kilichofanywa na Andrew Mtine wa Yanga.
Wasifu wa wawili hao, unaonyesha kila mmoja amekuwa na historia nzuri upande wa utawala wa soka mahali walikopita kabla ya kutua nchini, timu na taasisi ambazo Mtine amepita zinaonekana kutamba ndani ya uwanja kulinganisha na Regis.
Wawili hao kwa nyakati tofauti wametumikia nafasi za utawala katika klabu za soka, vyama vya mpira wa miguu vya nchi na shirikisho la mpira wa miguu Afrika katika idara tofauti.
Mtine ambaye alijiunga na Yanga mwaka 2022 kwa ngazi ya klabu ameziongoza Power Dynamos ya Zambia kwa nafasi ya mjumbe wa kamati ya utendaji na pia amewahi kuwa mtendaji mkuu wa klabu za Zesco United na Bidco kwa nyakati tofauti.
Mbali na timu hizo za kwao Zambia, Mtine pia amewahi kuitumikia TP Mazembe akiwa ni mratibu mkuu.
Kwa ngazi ya taifa, Mtine amewahi kukitumikia chama cha mpira wa miguu Zambia (FAZ) katika nafasi ya msimamizi wa masuala ya fedha na pia amewahi kuwa mshauri wa masuala ya ufundi.
Mtine pia amewahi kuitumikia Caf hapo nyuma pindi alipokuwa mjumbe wa kamati ya fedha na uchumi ya shirikisho hilo.
Regis yeye kwa upande wa uongozi katika ngazi ya klabu ameihudumia APR ya Rwanda kwa nafasi ya makamu mwenyekiti na kwa ngazi ya taifa aliwahi kuwa mtendaji mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (Ferwafa).
Ni miongoni mwa waanzilishi wa Chama cha makocha wa soka Rwanda ambacho amewahi kuwa makamu wake wa rais.
Mnyarwanda huyo ambaye pia ni kocha kitaaluma, amewahi kuwa mratibu mkuu wa mechi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).
Hata kwa mafanikio ya uwanjani, Mtine ameonekana kutamba katika sehemu nyingi alikopita kuliko Regis jambo linalomlazimisha mtendaji huyo mkuu mpya wa Simba kuhakikisha anafanya kazi ya ziada ili kumkaribia Mzambia huyo.
Mtine akiwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Power Dynamos, timu hiyo ilitwaa mataji sita tofauti ambapo kati ya hayo, moja lilikuwa ni la ligi kuu ya Zambia.
Akiwa mratibu mkuu wa TP Mazembe, timu hiyo ilitwaa mataji 12 ya Ligi Kuu ya DR Congo, mataji matatu ya Congo Super Cup, mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mataji mawili ya Kombe la Shirikisho Afrika na mataji matatu ya Caf Super Cup.
Mafanikio hayo ni kama yalihamia Yanga kwani tangu ahamie, timu hiyo imetwa mataji mawili ya Ligi Kuu Tanzania Bara, mataji mawili ya Kombe la TFF, Kombe moja la Toyota na pia imetinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika huku kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikifuika hatua ya robo fainali.
Regis akiwa makamu wa rais wa APR, timu hiyo ilitwaa mataji matatu ya ligi kuu ya Rwanda, mafanikio ambayo ndio makubwa zaidi kwake akiwa kiongozi wa soka.
Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio' alisema kuwa Regis hatakiwi kupewa presha ya kulinganishwa na Mtine.
"Mtendaji mpya amepatikana nadhani aachwe afanye kazi kwa utulivu lakini kuanza kumuweka katika mzani mmoja na Mtine sioni kama ni sahihi kwa vile njia walizopita ni tofauti na nyakati pia zinatofautiana.
"Kama ambavyo Yanga imempa nafasi Mtine kuonyesha uwezo wake nadhani Simba nayo inapaswa kumpa fursa kuonyesha uwezo wake," alisema Julio.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba alisema kuwa ujio wa watendaji wa klabu kutoka nje unadhihirisha kuwa soka la Tanzania limepiga hatua.
"Kwa sasa Tanzania sio kama zamani na mpira wetu umesogea mbele kiasi cha kuzifanya timu zetu kuwaajiri wataalam kutoka nje ya nchi ambao kimsingi wanaongeza kitu kwenye soka letu na uthibitisho wa hilo uko wazi.
"Ukiangalia alichokifanya Mtine ndani ya muda mfupi utaona ni kikubwa na kinachohitaji pongezi na tunategemea kuona huyo wa Simba (Regis) naye akiongeza kitu," alisema Mziba.