Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sakata la Sh400 milioni za bodaboda Arusha, aliyekuwa mwenyekiti mbaroni

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo

Muktasari:

  • Kati ya fedha zilizochangwa na wadau, Sh280 milioni zinadaiwa kuchotwa kwenye akaunti ya Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha (Uboja) na viongozi wa umoja huo waliokuwa madarakani.

Arusha. Sakata la ‘upigaji’ wa Sh400 milioni zinazodaiwa kuchotwa kwenye akaunti ya Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha (Uboja), limeingia sura mpya baada ya mtuhumiwa mmoja kati ya watatu kukamatwa.

Aliyekamatwa ni aliyekuwa mwenyekiti wa umoja huo, Maulid Makongoro.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Aprili 8, 2025, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kwamba uchunguzi unaendelea, ikiwemo kuwasaka viongozi wenzake wawili.

“Ni kweli tunamshikilia aliyekuwa mwenyekiti wa umoja huo, watuhumiwa ni watatu tunaendelea kuwatafuta wengine. Uchunguzi unaendelea,” amesema Zawadi.

Februari 27, 2025 viongozi wa sasa wa umoja huo waliiomba Serikali iingilie kati ili fedha hizo zipatikane na kuimarisha mfuko wao na kuwasaidia kukua kiuchumi.

Kati ya fedha hizo, Sh280 milioni zinadaiwa kuchotwa benki kwa nyakati tofauti na waliokuwa viongozi wa umoja huo, huku Sh120milioni zikidaiwa kutolewa kama mikopo kwa kinamama, ambapo hadi sasa hatima ya fedha hizo haijajulikana kutokana na akaunti yao kufungwa kwa ajili ya uchunguzi.

Kilio hicho kilitolewa na viongozi hao katika kikao maalumu cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kujadili makadirio ya mpango wa bajeti ya mwaka 2025/2026.

Kutokana na malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, aliagiza Takukuru mkoani humo mpaka Machi 27, 2025 itoe ripoti ya uchunguzi wa suala hilo lilipofikia.

Mwaka 2018, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (sasa mbunge wa Arusha Mjini), wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara walichangia Sh400 milioni ambazo ziliwekwa kwenye akaunti maalumu ya umoja huo.

Akizungumza kikaoni hapo, Katibu wa umoja huo Mkoa wa Arusha, Hakim Msemo, alihoji kwanini kumekuwa na kigugumizi cha kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani.

Alisema mwaka 2018, Sh120 milioni zilitolewa kama mikopo kwa kinamama na kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2020, Sh280 milioni zilitolewa benki bila utaratibu na mpaka wafadhili kutotaka kuwasaidia tena.

Alisema upotevu wa fedha hizo ulibainika mwaka 2022 baada ya kuingia madarakani na kukuta akaunti ikiwa haina fedha, huku nyaraka za benki zikionyesha namna fedha hizo zilivyochukuliwa katika matawi mbalimbali ya benki katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Takukuru, mkoani humo, Daniel Kapakala akijibu hoja hizo kikaoni hapo, alisema wameshachunguza suala hilo ila tatizo walilopata ni kuwapata watuhumiwa hao na walikuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi kuwatafuta.