Mtihani wa United kesho EPL, ikifungua pazia

Muktasari:
- Manchester United itacheza kesho saa 4 usiku dhidi ya Fulham katika ufunguzi wa EPL
Manchester. Baada ya mapumziko ya majira ya joto Ligi Kuu England, inarejea tena rasmi hapo kesho Agosti 16, 2024, huku mashabiki wa soka wakisubiri kwa hamu kuziona timu zao.
Ligi hiyo itaanza na mchezo utakaowakutanisha vigogo Manchester United wakiwa uwanja wao wa nyumbani Old Trafford dhidi ya Fulham, mchezo utakaopigwa saa 4:00 usiku.
United wataingia uwanjani wakiwa chini ya kocha wao Erik Ten Hag, (54) wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri tofauti na msimu uliopita, ambapo msimu huu wamesajili wachezaji wapya ambao wanaamini wataisaidia kupata matokeo mazuri.
Licha ya kufanya vibaya kwenye michezo ya maandalizi, yaani Pre-season, pamoja na kupoteza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wao Manchester City, mashabiki wanaamini hiyo siyo sababu ya kufanya vibaya msimu huu.
Hata hivyo, vigogo hao wa Jiji la Manchester wanaendelea kufanya usajili ili kukiboresha zaidi kikosi chao, United wapo ukingoni kuinasa saini ya Matthijs de ligt (25) pamoja na Noussair Mazraoui (26) wote wakitokea kwenye klabu ya Bayern Munich ya nchini Ujerumani kuja kuziba pengo la Leny Yoro ambaye alipata majeruhi ya muda mrefu pamoja na Aaron Wan Bissaka aliyetimkia West Ham United.
Pia inaelezwa kuwa timu hiyo ipo kwenye mazungumzo na klabu ya Brentford ili kuinasa saini ya mshambuliaji Ivan Toney (28), aliyeonyesha kiwango bora kwenye michuano ya Euro akiwa na timu ya Taifa ya England.
Mara ya mwisho ilikuwa ni msimu wa 2018/2019 Manchester United walifungua msimu wa ligi kuu ya England dhidi ya Leicester City ambapo walichomoza kwa ushindi wa mabao 2-1 katika uwanja wao wa Old Trafford.
Katika msimu huo wa 2018/2019, Mancheter City walitwaa ubingwa, huku Man United wakimaliza katika nafasi ya sita ambapo walikusanya jumla ya pointi 66 wakibaki nyuma ya Man City, Liverpool, Chelsea, Tottenham Hotspurs, na Arsenal.
Ijumaa ya kesho Agosti 16 itakuwa ni mara ya kwanza kwa mashetani wekundu kucheza mchezo wa ufunguzi tangu Agosti 10 mwaka 2018.
Baada ya mchezo huo wa ufunguzi, ligi ya England itaendelea tena Agosti 17 ambapo viwanja sita vitatimua vumbi huku majogoo wa Jiji la London Liverpool, wakicheza saa 8:30 mchana kwenye uwanja wa Portman Road wakiwa wageni wa Ipswich Town iliyopanda daraja msimu huu.
Michezo mingine itawakutanisha Arsenal dhidi ya Wolves, Everton dhidi ya Brighton, Newcastle dhidi ya Southampton, Nottm Forest dhidi ya Bournamouth na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya West Ham dhidi ya Aston Villa.